Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Hamida Mohamedi Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Lindi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambazo ziko Mezani kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwapongeza Waheshimiwa Wenyeviti wa Kamati zote mbili kwa uwasilishaji wa taarifa za Kamati zao kwa weledi mkubwa sana. Nawapongeza Kamati ya Sheria Ndogo kwa namna ambavyo wameweza kujikita katika kuchambua sheria mbalimbali na kuweka mambo sawa ili kuhakikisha kwamba wanaokwenda kusimamia sheria hizi, basi waende kusimamia vizuri, kuhakikisha tunaleta ustawi wa wananchi wetu katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo imeainisha mambo mbalimbali baada ya kufanya uchambuzi wa sheria hizi, na kuona kwamba kuna dosari mbalimbali ambazo zimeonekana kwamba ni kero kwa watumiaji wa sheria hizi, ama katika usimamizi wa sheria hizi. Kwa hiyo, nawaomba katika maeneo yote yaliyoonekana yana dosari, basi wahusika waende wakayafanyie marekebisho ili twende vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Sheria Ndogo ya Ada na Ushuru wa Halmashauri ya Mafinga, TS Na. 211. Sehemu ya 10 ya Jedwali la kwanza inahusu ushuru wa mazao ya uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika kipengele hiki, kuna tatizo. Kipengele kina tatizo la kuweka ada ya shilingi 200/= kwa wapaaji wa samaki, na ukiangalia samaki huyo anaanza kulipiwa tozo kuanzia kwa mvuvi mwenyewe. Mvuvi husika anamuuzia mteja mwingine ambaye anakwenda kuuza hadi kwa huyu mtu mdogo kabisa ambaye ameacha kuwa kibaka mtaani akaamua kwenda katika maeneo haya na kutafuta ajira ya kupaa samaki ili kumfanya mteja atoke katika eneo hili akiwa na samaki ambao wakosafi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani tukafanyie marekebisho eneo hili ili kutenda haki kwa wananchi wetu na vilevile kuendelea kuleta ustawi kwa wananchi wetu na kuongeza ajira kwa vijana ambao wanakosa ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye Sheria Ndogo ya Ushuru wa Mazao ya Uvuvi, Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Tangazo la Serikali Na. 815, Sheria ya Mwaka 2020, Jedwali la Tatu linahusu kibali cha kusafirisha mazao ya uvuvi. Katika maeneo haya, tumeona kwamba kuna tatizo; na niseme tu kwamba, jedwali limeweka sharti la kuomba kibali cha kusafirisha mazao ya uvuvi kwa matumizi ya nyumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kila mtu anavyokwenda kununua samaki kwa ajili ya matumizi ya nyumbani akaombe kibali halmashauri? Naona hii haijakaa sawa. Kwa hiyo, halmashauri husika ama Wizara ya TAMISEMI wakahakikishe kwamba eneo hili wanalitazama vizuri ili kuhakikisha kwamba linafanyiwa marekebisho ili tafsiri yake iweze kukaa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile nawapongeza Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ambao umefanyika wiki moja iliyopita na kuridhia Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ndiye Mgombea wa Urais wa Chama cha Mapinduzi pamoja na mgombea mwenza wake Balozi Emmanuel John Nchimbi. Pia Rais wa Zanzibar kuwa ndiye mgombea wa Urais wa mwaka huu wa 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa pamoja nawatakia kila la heri. Mwenyezi Mungu awaweke salama, awaweke katika afya njema ili maazimio yetu yaweze kutekelezwa kwa sababu bado tunawahitaji kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. Bado Watanzania tunahitaji Marais hawa waendelee kuwa Marais wetu ili mambo yetu yaweze kuwa safi. (Makof)

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii kumpongeza Mwanasheria Mkuu kwa sababu anasimamia masuala yote ya sheria na kuharakisha kwenda kwenye utekelezaji wa matumizi ya sheria hii. Mwisho, nawapongeza Katibu wetu wa Kamati ya Sheria Ndogo, pamoja na msaidizi wake kwa namna ambavyo anatufanya sisi Wajumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo kuendesha shughuli zetu kwa weledi mkubwa. Tunawashukuru na tunawapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)