Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Maryam Omar Said

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Pandani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia ili nami niweze kusema neno katika maazimio haya mawili yaliyopo Mezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawapongeza Wenyeviti wa Kamati zetu zote mbili kwa kazi kubwa wanazozifanya katika kuhakikisha Wajumbe tunafanya kazi zetu pamoja nao kwa weledi. Pia, nawapongeza Wajumbe wenzangu wa Kamati ya Sheria Ndogo. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendeleze pale ambapo amefikia mwenzangu, Mheshimiwa Hamida; na nitajielekeza kwenye utekelezwaji wa maazimio ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba katika Mkutano wa Kumi na Tatu, tulipitisha Maazimio ya Bunge ya Kamati ya Sheria Ndogo. Kati ya maazimio yaliyopita, ilikuwemo Sheria ya Ada na Ushuru ya Wilaya ya Mafinga, Tangazo Na. 211, inayomhusu mpara samaki kutoa ushuru wa shilingi 200.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili tulilisemea sana, na mwisho tukaazimia kwamba hii haikubaliki. Ule ulikuwa ni Mkutano wa Kumi na Tatu, leo tunazungumza ndani ya Mkutano wa Kumi na Nane. Tulizungumza na tukakubaliana vizuri na Mheshimiwa Waziri, lakini mpaka leo hii hii sheria bado ipo na inafanya kazi. Ni kumaanisha kwamba, Azimio la Bunge halikufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nataka niiambie Serikali, mara zote sheria mama zinakuja Bungeni zinafanyiwa kazi na zinakwenda kufanya kazi zikiwa ziko vizuri, lakini mara nyingi kanuni ndizo zinazowaumiza wananchi. Hii ni kwa sababu zinatoka mtaani, zinafanya kazi, na zinapokuja kwetu, tayari kule zinakuwa zimeshaanza kufanya kazi. Kwa nini Azimio la Bunge likishaelekeza, Wizara isichukue hatua? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi huwa naumiza kichwa hapa. Siyo hilo tu, pia lilikuwepo Tangazo la Serikali, Sheria Ndogo ya Ada na Ushuru ya Halmashauri ya Mafinga, inayoelekeza kwamba watakusanya ushuru kuanzia saa 12.00, na mwisho kukusanya ushuru ni saa 12.00 jioni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii haina uhalisia, kwani wengi wanaweza kukwepa ushuru kwa kuona kwamba, mimi nimefika sehemu saa 11.30, ngoja ni-delay kidogo, nikiingia saa 12.01 siwezi kudaiwa tena ushuru. Tunapoteza mapato mengi ya Serikali hapa. Kwa nini Serikali msiwe pamoja na sisi? Hili ni tatizo. Hii sheria ilikuja kwenye azimio wakati wa Mkutano wa Kumi na Tatu, lakini leo hii tunavyozungumza, ni Mkutano wa Kumi na Nae, lakini bado sheria hii haijafanyiwa marekebisho na haijafanyiwa kazi. Hili jambo linatusikitisha sana kama Kamati. Ni vizuri tunapotoa maazimio ya Bunge Mawaziri wawe tayari, tuwe pamoja katika kuhakikisha yanafayiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mengi yamesemwa na wenzangu waliopita na hivyo hakuna haja ya kuyarudia. Naendelea kuwapongeza viongozi wetu, akiwemo Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya, pia Rais wa Zanzibar kwa kazi nzuri anayoifanya. Nawaambia tu, CCM hawakukosea kuwaweka kama ni wagombea mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya machache hayo, naunga mkono hoja zote mbili zilizopo Mezani. Ahsante sana, nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)