Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kuipongeza Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na ninazipongeza Wizara zote chini ya Kamati yetu ya Utawala, Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Kamati pia tulifanikiwa kutembelea miradi mbalimbali, tumeona kwa asilimia kubwa imetekelezwa japokuwa ipo michache iliyotekelezwa chini ya kiwango. Hiyo ni kutokana na ucheleweshaji wa kulipwa wakandarasi kwa muda. Hivyo, tunaiomba Serikali kuwalipa wakandarasi kwa wakati ili miradi ikamilike kwa wakati na iweze kuleta tija iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza Serikali kwa kutekeleza maazimio tuliyoyafikia kama Bunge. Kipekee naipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwani imeboresha miundombinu ya watu wenye ulemavu katika mchakato wa usaili wa ajira nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, e-Utendaji ni mfumo wa kuimarisha utendaji kazi wa watumishi wa taasisi za umma unaotegemewa kuleta tija katika kufuatilia na kutoa mrejesho wa utendaji kazi na kuimarisha uwazi na uwajibikaji itakayohakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuishauri Serikali, ubunifu huu uendane na kupeleka mtandao ya vijijini ili watumishi waliopo huko pembezoni, wasawazwe kwa uwiano ili wasiwepo ambao wanakuwa na mzigo mkubwa wa majukumu hivyo kushindwa kujaza mifumo hiyo kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira kuendelea kusaili kidigitali. Kwa sasa baada ya mfumo wa kupima uelewa na ufahamu ambao mpaka sasa umesaili zaidi ya wasailiwa 28,143 katika taasisi 19 na kada 60, na sasa wamekuja na mfumo wa kupima haiba na tabia, umefikia 60%.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasisitiza Serikali iwekeze mifumo hii kwenye vituo vyote vya usaili katika mikoa yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya machache, naunga mkono hoja.