Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia mchango wangu wa kwenye hoja zilizowekwa Mezani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia kuwepo hapa leo. Kwa namna ya pekee nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya, hasa katika eneo hili la utumishi wa umma na utawala bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mambo mengi makubwa yanafanyika, na kweli anastahili tuzo nyingi, na ninaamini atapata tuzo nyingi zaidi na zaidi, kwa sababu kazi kubwa anayoifanya inaleta hamasa kubwa kwa watu wengi kumpa tuzo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo, naomba pia nijielekeze kwa mambo machache yaliyosemwa. Kwanza, naipongeza Kamati yetu ya Utawala, Katiba, na Sheria kwa namna ambavyo wanafanya kazi nzuri chini ya Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Dkt. Mhagama pamoja na Makamu Mwenyekiti na Kamati yote kwa ujumla, wanafanya kazi nzuri. Tumekuwa tukishirikiana nao, na kwa kweli ushauri wao umekuwa ni msaada mkubwa wa kuhakikisha kwamba tunakuwa na ufanisi katika kazi yetu ambayo tumekabidhiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo tumepewa ushauri na kwa kweli tumelifanyia kazi ambalo nitaanza nalo ni kuhusu upandishaji wa vyeo watumishi. Kweli nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais. Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024, alipandisha vyeo watumishi 232,532, na mwaka huu wa fedha katika bajeti hii, fedha imetengwa kwa ajili ya kupandisha vyeo watumishi zaidi ya 219,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niihakikishie Kamati yako kwamba, ushauri wao waliotupa tutahakikisha tunawasimamia vizuri maafisa utumishi katika maeneo yote, kwamba wahakikishe wanaleta taarifa kwa wakati ili kupitia bajeti iliyoidhinishwa na Bunge hili watumishi wale wanaostahili kupanda vyeo, ambapo kumekuwa na malalamiko mengi, tuhakikishe kwamba tunapomaliza mwaka huu wa fedha tuwe tumetekeleza jukumu hili kadri mlivyotupitishia bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili lililoongelewa ni suala la kutangaza kazi ya Kituo cha Ubunifu (Research and Innovation Centre), inayokuwa chini ya e-GA. Naomba jambo hili nilisemee angalau maneno machache.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kituo chetu hiki, kwa takribani kipindi cha miaka miwili e-GA imekuwa ikiandaa vijana takriban 400 hivi ambao wanafanya ubunifu katika teknolojia ya habari (TEHAMA). Mambo ambayo wanayafanya ni mambo ambayo ni makubwa kwa manufaa ya Taifa letu. Kwa mfano, wanafanya tafiti kwenye mambo ya Blockchain Technology Crypto Currency pamoja na mambo ya Artificial Intelligence. Wameweza kubuni vitu vingi ambavyo vimetupelekea kama nchi kupata sifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi katika maonyesho yaliyofanyika kwenye African Digital Platform iliyofanyika nchini Zambia, tuliweza kupata nchi mbalimbali ambazo zimeweza ku-develop interest ya kuja Tanzania kujifunza namna vijana wetu wanavyofanya ubunifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ubunifu ule umeweza kufanya pia nchi yetu ipate tuzo mbalimbali. Kwa mfano, mwaka 2024 katika maonyoshe ya UN, kwenye Digital Palatiform iliyoandaliwa na UN nchini Korea Kusini tuliweza kupata tuzo ya kuanzisha mfumo wa e-Mrejesho ambapo nchi ya Tanzania iliibuka kinara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sifa zote hizi ni jitihada kubwa na uwekezaji mkubwa anaofanya Mheshimiwa Rais. Kama Kamati ilivyoshauri, tutaendelea kutangaza kazi hizi ili tuwavutie nchi nyingi zije kwenye kituo chetu zijifunze namna ambavyo vijana wetu wanafanya ubunifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo tu hilo, baadhi ya vijana wetu wamepata ajira. Kwa mfano, kuna baadhi ya vijana wameajiriwa Singapore, wengine wameajiriwa UK, na baadhi ya wengine wameleta maombi ya kuwachukua vijana wetu kutoka kwenye kituo hiki. Kwa hiyo, ni habari njema ambayo kama Wizara tutaendelea kushirikiana na Kamati, na maazimio yote haya manne waliyotushauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Kamati tumeyapokea chini ya usimamizi wa kiongozi wetu wa Wizara, Mheshimiwa George Boniface Simbachawene. Tutahakimisha kwamba Kamati; na tumwombe sana Mwenyezi Mungu ili Bunge lijalo; na ninaamini kwa kazi kubwa tulifofanya Wabunge humu; Mwenyezi Mungu atanyoosha mkono wake, tutakutana tena Novemba ili tuone kazi kubwa ambayo tutakuwa tumetekeleza maazimio hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)