Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na shukrani na pongezi kwa taarifa nzuri sana ya Kamati yenye kurasa 57, naomba nichangie mambo mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, sisi kama Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji tumeyapokea na tunakubaliana na mapendekezo ya maazimio matatu yote yaliyopo katika ukurasa wa 44 mpaka ukurasa wa 45.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiambie tu Kamati kwamba kwenye Muswada mpya wa sheria ambao tumependekeza kuuleta hapa, Sheria ya Uwekezaji, baadhi ya mambo yatashughulikiwa kule pamoja na mapitio ya mpango mpya wa kuboresha mazingira ya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili katika mchango wangu nataka nichukue nafasi hii katika muktadha wa utawala bora kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa tuzo ambayo ameipata jana, tarehe 4 Februari, 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani watu wengi hawajaelewa vizuri ile tuzo, niieleze kidogo. Hii tuzo kwa Kiswahili inaitwa Tuzo ya Dunia ya Golikipa (Global Goalkeeper Award). Unaweza ukaifananisha na wanamichezo hapa, na tuzo ambayo huwa inatolewa kwa golikipa bora katika mashindano ya FIFA ya World Cup. Kila mwaka huwa inatolewa kwa kila mashindano ya kipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mwaka 2022 mtakumbuka Emmy Martinez wa Argentina ndiyo aliyeshinda hii tuzo. Huwa inatolewa kwa golikipa bora sana. Ndivyo hii Foundation ya Gates iliiga kutoka kwenye FIFA ikaanzisha tuzo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu ni wa saba kuipokea jana. Inatolewa tuzo kwa nani? Inatolewa tuzo kwa viongozi ambao wamechangia katika kufanikisha utekelezwaji wa malengo ya dunia endelevu (Sustainable Development Goals 2030). Ukitaka kujua uzito wake, angalia waliopita ni akina nani? Wa kwanza aliyepata tuzo hii mwaka 2019 Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India ndio wa kwanza kuipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, nisikutajie wa pili na wa tatu, nikutajie wa nne Ursula von der Leyen, Rais wa European Commission (Tume ya Ulaya). Yule mama mnamfahamu, lakini wa tano alikuwa nani? Mtu wa tano alikuwa Fumio Kishida, Waziri Mkuu wa zamani wa Japan, 2021 mpaka 2024. Mtu wa sita alikuwa ni Luiz InĂ¡cio Lula da Silva, Rais wa Brazil, mwaka jana hiyo; na wa saba aliyepata ndiye anaitwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini kapewa tuzo hii? Kwa kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Sekta ya Afya Tanzania specifically, mchango wake katika kupunguza vifo vya akinamama wakati wa kujifungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulijiwekea lengo kwamba ifikapo mwaka huu, 2025 tuwe tumepunguza vifo kutoka 565 mpaka 225, lakini tume-achieve 104, mwaka 2022. Kwa hiyo, duniani hapa indicator kubwa ya kupima maendeleo ya afya na maendeleo ya watu ni afya ya akina mama na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama ulikuwa unatilia shaka uthabiti na ubora wa uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tafadhali bwana, waliotoa tuzo hii ni taasisi inayoheshimika duniani, lakini ligi yake waliyopata wengine ndio hawa akina Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India. Tafadhali Bwana; Lula, Rais wa Brazili ambaye anasifiwa sana kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Fumio Kishida, Waziri Mkuu mwenye mafanikio makubwa sana Japan. Amekaa miaka minne kule Japan, Waziri Mkuu anakaa miezi kadhaa, mwaka mmoja; huyu kakaa miaka minne, kapata tuzo, na huyu Mama Ursula.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka kuwaomba Watanzania watembee kifua mbele, kwani tunaye kiongozi thabiti, Rais imara ambaye anasimamia ajenda zake. Mafanikio haya pia ni mafanikio ya uongozi wa Chama cha Mapinduzi ambacho leo kinaazimisha miaka 48. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, mafanikio haya ni ya Serikali. Mafanikio haya ni ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, naunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)