Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Songea Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue fursa hii kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Chama Cha Mapinduzi kwa kuweza kuwapata wagombea watatu katika uchaguzi wa mwaka 2025. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Balozi Emmanuel John Nchimbi ambaye anaenda kuwa mgombea mwenza, na Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi anaenda kuwa mgombea Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa safu hii ambayo imepatikana wakati Chama Cha Mapinduzi kinatimiza miaka 48, itawafanya watu wasiingize timu uwanjani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria chini ya uongozi wa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, pamoja na Kamati ya Sheria Ndogo chini ya uongozi wa Dkt. Wakili Msomi, ambao umetuwakilisha leo hapa na taarifa zetu mbili. Ni taarifa nzuri ambazo Serikali kwanza tunazipokea na kuziunga mkono, lakini pili tunachukua maelekezo yao yote na maazimio yote ili kwenda kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu niseme mambo machache ambayo yamesemwa kwenye Kamati na sisi tunayaunga mkono. Jambo la kwanza, Kamati imeongea kuhusiana na umuhimu wa uwepo na ufanisi wa Tume ya Kurekebisha Sheria ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Serikali inaunda Tume hii ilikuwa na makusudi kwamba kila sheria itakayotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano lazima ifanyiwe utafiti kwanza na Tume ya Kurekebisha Sheria. Kamati imetoa maazimio hayo, sisi tumeyapokea na tuahidi kwamba nikiwa Waziri mwenye dhamana ya haki nitakwenda kutekeleza jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu ambaye Mheshimiwa Prof. Kitila amemwaga sifa nyingi, lakini katika suala la haki tunafahamu ya kwamba aliunda Tume ya Haki Jinai ambayo imetoa mapendekezo ya kufumua mfumo mzima wa haki jinai, nasi Serikali tumeanza kuyafanyia kazi. Hata hivyo, juzi wakati wa Sherehe ya Siku ya Sheria ambapo yeye, Mheshimiwa Rais alikuwa Mgeni Rasmi, alisema sasa anapeleka nguvu katika haki madai. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa haki jinai huku tayari gari limeshika mwendo, sasa tunakwenda kwenye hakimadai. Huku napo tayari tuna maelekezo ya Mheshimiwa Rais, tusimamie vizuri eneo hilo ili wananchi pia wapate haki zao katika masuala ya madai. Katika kutekeleza hayo, Mheshimiwa Rais amekuja na mpango ambao umepewa jina lake, kwa heshima yake unaitwa Mama Samia Legal Aid Campaign.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la mpango huu ambao Kamati imeelezea vizuri na kuipongeza Serikali; mosi, ni kutoa elimu ya sheria kwa wananchi wote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na pili, kutoa msaada wa kisheria hususan kwa wananchi wanyonge waliopo vijijini ambao hawawezi kumudu gharama za juu za Mawakili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango huu umeshakwenda katika mikoa 17 mpaka sasa, na mpango ni kwamba tukifika Aprili, 2025 mikoa yote 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa imefikiwa na mpango huu. Mpaka hivi sasa mpango huu umeshatatua migogoro zaidi ya 7,000 na tunaendelea kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu zaidi, tarehe 01 - 08 mwezi Machi katika wiki ya wanawake duniani mpango huu unakwenda kuungana na sherehe za wiki ya wanawake duniani na tunahamia mkoa wa Arusha kuhakikisha tunaufanya vizuri kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, niseme naishukuru sana Kamati. Tumepokea maazimio yote na Serikali, tunakwenda kuyashughulikia na kuyatekeleza. (Makofi)