Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Madaba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata fursa hii ya kuhitimisha hoja ya Kamati ambayo ililetwa mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote tisa na Mawaziri na Naibu Mawaziri wanne ambao wamepata fursa ya kuchangia hoja hizi za Kamati zetu zote mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kwa sehemu kubwa au kwa 100% wachangiaji wote waliopata fursa hii wameitumia hii fursa kukubaliana na hoja za Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge na Waheshimiwa Naibu Mawaziri waliopata fursa ya kuchangia eneo linalohusu Utawala, Katiba na Sheria wamejielekeza kwenye hoja za Kamati moja kwa moja na wameweka mkazo kwa Waheshimiwa Wabunge. Pia, Waheshimiwa Mawaziri wameonesha namna bora ambayo wataenda kutekeleza maazimio haya ya Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nasoma, yapo maeneo mawili ambayo nilidhani ni muhimu sana hayakupata mkazo sana, mkazo ambao unastahili ukilinganisha na umuhimu wake. Kwa hiyo, tunapohitimisha hoja hii, nilitamani maazimio haya mawili yawe sehemu ya maazimio ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza, inahusu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji. Naamini unakubaliana nami kwamba tunayo sera nzuri sana ya uwekezaji nchini na sasa tunaboresha sheria kwa ajili ya kutengeneza sheria bora kabisa ya uwekezaji. Hata hivyo, Kamati imebaini kwamba hakujafanyika utafiti au kama utafiti umefanyika haujawekwa vizuri ili kubainisha kwanza, uwezo wetu wa ndani wa kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi na pili, uwezo wa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini tukiwa na sera ya uwekezaji na sheria ambazo zitawasaidia Watanzania, kwanza kuelewa maeneo ya uwekezaji yanayoendana na uwezo wao wa kifedha, kimtaji na kiujuzi yakawekwa sambamba na maeneo ya uwekezaji ambayo labda yanahitaji ujuzi na mitaji mikubwa ambayo inawataka wageni wawekeze.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini yapo maeneo mengi sana kama Serikali yetu itaongeza nguvu ya kuwawezesha Watanzania, basi tutapata Watanzania wengi sana watakaowekeza katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa natoa mfano eneo la Kilimo, eneo la Mifugo na maeneo mengine mengi ambayo kama nchi tutaamua kuwekeza nguvu, basi tutawasaidia Watanzania wengi na hatutahitaji wageni kuwekeza katika maeneo ambayo Watanzania wenyewe tunaweza kufanya. Kwa hiyo basi, kwa sababu hili lilijadiliwa sana kwenye Kamati, naomba liwe sehemu ya maazimio ya Bunge lako na azimio lisomeke kama ifuatavyo: -
KWA KUWA, imebainika kuwa uvutiaji wa wawekezaji nchini hauzingatii vipaumbele vya maeneo ya uwekezaji baina ya yale ambayo Watanzania wana uwezo nayo na yale ambayo hawana uwezo nayo kwa kuzingatia viwango vya mitaji, ujuzi na teknolojia;
NA KWA KUWA, kuacha hali ilivyo kunawaingiza Watanzania kwenye ushindani usio sawa wa kibiashara;
NA KWA KUWA, hali hii inaweza kuwaongezea Watanzania wengi umasikini;
KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kuwa Serikali isimamie Sera ya Uwekezaji kwa kubainisha maeneo ya vipaumbele kwa wageni na kwa Watanzania na kuwajengea uwezo Watanzania kuwekeza kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo naomba kuliwasilisha kama azimio la Kamati na ninaomba sasa ligeuke kuwa pia azimio la Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili inahusu Wizara ya Katiba na Sheria. Utakubaliana nami kwamba tuna changamoto sana ya uendeshaji wa mashauri katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Tuna changamoto ya watumishi, lakini pia tuna changamoto ya kibajeti. Yapo mashauri mengine tunalazimika kutafuta consultants kutoka nje ya nchi ili kuyafikia kuyafanyia kazi. Ipo mikataba mbalimbali ambapo tunatumia fedha nyingi sana kupata watu toka nje kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili pia limejadiliwa kwenye Kamati na ninaomba liwe pia sehemu ya maazimio ya Bunge lako na maazimio haya yasomeke kama ifuatavyo: -
KWA KUWA, Kamati imebaini kuwepo kwa changamoto ya bajeti na upungufu wa rasilimali watu kwenye Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali;
NA KWA KUWA, upungufu huu unakwamisha jitihada za Serikali na Ofisi hii kushughulikia mashauri muhimu yenye maslahi makubwa kwa Taifa letu;
KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba, Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2025/2026 ihakikishe inatenga bajeti ya kutosha ili kuiwezesha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutekeleza wajibu wake kikamilifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba tena kukushukuru wewe na wote waliochangia hoja hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.