Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Dr. Jasson Samson Rweikiza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha hoja yangu ambayo nimeitoa leo hapa muda mchache uliopita. Nawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wote, Mawaziri na Naibu Mawaziri waliochangia hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, jumla tumepata wachangiaji 13, Wabunge tisa na Naibu Mawaziri na Mawaziri wanne. Wote kwa umoja wao wameunga mkono hoja na kukubali kwamba hoja ina mashiko na inatakiwa iwe ndiyo maazimio ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya Kamati hii ya Sheria Ndogo ni kama jicho la Bunge au ni kama watchdog. Ndiyo chombo cha Bunge hili kuhakikisha kwamba kazi yake inafanyika vizuri. Ibara ya Nne ya Katiba kama nilivyoisema pale awali inaeleza bayana kwamba kazi za kutunga sheria ni ya Bunge, chombo pekee chenye uwezo wa kutunga sheria ni Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Ibara ya 97 (5) inatoa tena nafasi kwa Bunge hili kukasimu madaraka yake kwa watungaji wengine, ambao ni Wizara, Idara za Serikali au watu mbalimbali Serikalini kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Kamati hii ya Sheria Ndogo inatazama kama hawa waliokasimiwa madaraka ya Bunge, je, wamefanya vizuri au kuna dosari na kasoro? Ndiyo kazi hiyo pekee kubwa tunayoifanya. Sasa baada ya kufanya kazi hiyo tunakaa, tunachambua sheria ndogo hizo na kutoa maelekezo ambayo yanakuja hapa, yanakuwa maazimio ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba maazimio hayo mengi yanatekelezwa kama yanavyotolewa. Nitataja hapa Wizara chache ambazo zimefanya maazimio hayo vizuri bila kupindisha kwa kufuata maelekezo na maazimio ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Fedha imetimiza maazimio au kwa kurekebisha sheria ndogo mbili vizuri na kwa ufasaha mzuri. Wizara ya Viwanda na Biashara imetekeleza maazimio ya Bunge kwa kurekebisha kabisa sheria ndogo moja, na Wizara ya Uchukuzi imetekeleza kwa kurekebisha na kutangaza sheria ndogo tisa, na tayari zinafanya kazi vizuri kwani kasoro zimeondolewa na zipo sawa sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI pia, imetekeleza kwa kurekebisha sheria ndogo 24 vizuri bila mabaki yoyote na zinafanya kazi vizuri, lakini wapo wachache ambao hawakufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wa TAMISEMI katika Manispaa ya Mtwara kwa mfano kuna sheria ndogo nne hawajazifanyia kazi. TAMISEMI hiyo hiyo, Halmashauri ya Manispaa ya Singida sheria ndogo tatu hawajazifanyia kazi na bado zinabaki kuwa kero na zina dosari ambazo zinasumbua wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ile kazi ya Bunge ya kuhakikisha kwamba wananchi wasipate sheria ambazo zina kero na matatizo, haijafanyika kwenye maeneo hayo mawili au matatu ambayo nimeyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kusisitiza kwamba hao ambao wamebainika wafanye kazi hiyo vizuri haraka na tumeeleza kwenye taarifa kwamba kwenye vikao vya Kamati mwezi Machi, taarifa zije tuone kama wametekeleza au kama kuna upungufu. Hiyo ndiyo kazi ya Kamati ya Sheria Ndogo ambayo tunaifanya kwa niaba ya Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)