Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie Taarifa hii ya Kamati ya PAC kama ilivyowasilishwa na Mheshimiwa wa Kamati. Kwanza, nawapongeza sana Kamati kwa taarifa nzuri ambayo imeletwa hapo leo yenye msisitizo kwa maeneo ambayo Serikali inatakiwa kuyaboresha zaidi ili kufika kwenye usanifu na kuona thamani ya fedha kwa miradi ambayo tunaendelea nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami naungana na Wabunge wenzangu waliopita kwenye michango yao ya nyuma kupongeza sana Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi uliokaa tarehe 19 Januari kwa kumpitisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea pekee wa Urais 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, naungana nao, na kwenye hili Wajumbe waliona hamna haja ya kusubiri kwa sababu maendeleo yamefanyika na sisi tumeyaona kwa kweli yamefanyika hatukutaka kusubiri na sisi tunaungana nao, na Busega tupo tayari kwa ajili ya kazi ya kuhakikisha kwamba Mama Samia anashinda tena mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa imezungumzwa hapa na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati, nami nataka nichangie eneo moja tu juu ya ujenzi wa vyuo vya VETA, vyuo 64. Kwa maana, vyuo 63 ambavyo ni vyuo vya wilaya ambazo hazikuwa na VETA pamoja na chuo kimoja cha Mkoa wa Songwe kule kwa Mheshimiwa Hasunga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyekiti kazungumza hapa kwamba baada ya CAG kwenda kuangalia ukaguzi huu, kuna changamoto ambazo zimebainika katika ukaguzi uliofanywa na CAG ikiwemo ucheleweshwaji wa miradi hii ya ujenzi wa VETA. Miradi hii imecheleweshwa kwa sababu ya upatikanaji wa fedha kutoka Wizara ya Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii 63 ya vyuo vya wilaya na hiki kimoja cha mkoa, fedha za kwanza ambazo tuliweka kwenye mpango wa 2022/2023 kwenye bajeti ilikuwa shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa VETA hizi, na ujenzi huu ulikuwa ni wa haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mpaka kufikia Januari, 2025 fedha ambazo zilikuwa zimeshatoka tayari ambazo zilikuwa ni shilingi bilioni 54 sawa na 54% ambapo sasa kuna baadhi ya VETA hizi ambazo ujenzi wake umeanza, zimekaa muda mrefu zikiwa na maboma bila kuwa na vifaa kwa ajili ya kuezeka na vifaa vingine kwa ajili ya kumalizia, ambapo ilikuwa ni kwa ajili ya majengo tisa na awamu ya pili ni majengo nane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tukichukulia pale Busega tayari tumeshaletewa fedha za ujenzi wa majengo, lakini ni muda sasa umepita takribani miezi sita hatujapata fedha za kuendeleza miradi, na majengo yamejengwa kwa maana ya maboma, yamekaa pale, lakini miradi hii ilikuwa ni miradi ya kimkakati. Tulipowahoji Wizara ya Elimu, kwa unyenyekevu kabisa walionesha jitihada ambazo zimefanyika kwa ajili ya upatikanaji wa fedha, lakini walikuwa hawajapelekewa fedha na Wizara ya Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale mwanzoni walielekezwa wanunue vifaa kwa mara moja (bulk) ikiwemo cement; na ilishanunuliwa kwa muda mrefu. Kwa mfano, kuna baadhi ya maeneo mpaka sasa hivi tunavyozungumza tayari maboma yameshakamilika na cement ya kuendeleza ipo, lakini hawawezi kuendeleza kwa sababu maboma yale bado hayajaezekwa na ile cement sasa inaharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mifano, kama kwa pale Busega, tuna mifuko 718; ukienda kule Songwe, kuna zaidi ya mifuko 1,000; ukienda kule Mlele, kuna zaidi ya mifuko 800 ambayo ipo na sasa muda wowote inaweza kuharibika kama hatutapata fedha za haraka kwa ajili ya kunusuru miradi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuja na wazo la ujenzi wa VETA kwenye wilaya ambazo hazikuwa na VETA. Ni wazo jema na lina tija kwa Watanzania kwa ajili ya wale Watanzania ambao sasa wanaweza kujiendeleza kwenye VETA zetu kwa shughuli ndogo ndogo zikiwemo shughuli za upishi, fundi cherehani na kazi nyingine, kupata elimu kwenye VETA zetu… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante. Dakika tano tayari, ahsante.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa uwe na nidhamu ukiwa kwenye Bunge, naomba sana. Kwanza hurusiwi kuzungumza na mimi kwa mujibu wa Kanuni.
MHE. ESTHER N. MATIKO: (Aliongea nje ya mic)
NAIBU SPIKA: Nawe Mheshimiwa Esther ni Mbunge wa siku nyingi sana, lakini unapenda tu chokochoko. Ukinizingua nitakuzingua. Behave yourself. Kama una tatizo na mimi, unamwandikia barua Katibu, that is how it works. Kaa chini, kaa kimya. (Makofi)
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, Wizara ya Fedha ipeleke fedha Wizara ya Elimu ili miradi hii ikamilike kwa wakati. (Makofi)