Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Tunapoelekea kukamilisha muda wa Bunge hili la Kumi na Mbili, napenda kukishukuru sana Chama changu cha CCM kwa kunipa heshima ya kuwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nakipongeza chama changu kwa maboresho makubwa ya demokrasia ndani ya chama ambayo hasa tunaenda kuyaona zaidi mwaka huu kwa kuongeza Wajumbe. Mimi peke yangu nitakuwa na Wajumbe zaidi ya 15,000 ambao watanipigia kura za maoni. Kwa hiyo, nawaomba Wajumbe wajiandae muda utakapofika watimize wajibu wao na wale jamaa zangu nawaambia kwamba mwaka huu chama kitarudisha majina kwa hiyo, wawe watulivu waache fujo fujo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana wateule wetu wa ngazi ya Taifa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu; Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi; na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa uteuzi ambao tuliwapa kwenye Mkutano Mkuu tayari kwa kupeperusha bendera kwenye Uchaguzi Mkuu. Ninawapa hongera sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, nalipongeza Bunge lako Tukufu pamoja na Serikali kwa kusimamia vizuri uwajibikaji kama ambavyo amekuwa anashauri CAG. Kwa hiyo, kwenye hilo, hongera sana. Katika jukumu hilo, Bunge limetekeleza wajibu wake kwa weledi mkubwa na Wabunge tuna haja ya kujipongeza sana, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, dalili za ubora katika uwajibikaji tumeziona tulipotembelea miradi, na mwenzangu Mheshimiwa Songe ametaja miradi ya VETA, na tulitembelea na Kiwanja cha Ndege cha Msalato ambapo ujenzi wake unaendelea vizuri. Kwa hiyo, kwa kweli tunawapongeza sana kwa hatua hiyo, hongera sana Serikali na Bunge kwa kusimamia vizuri uwajibikaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri katika maeneo machache. Kwanza, mifumo yetu ya udhibiti wa matumizi ya fedha za umma bado tunahitaji kuendelea kuiboresha. Mafunzo ya mara kwa mara ya uzingatiaji wa Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu ikiwemo Mifumo ya Kiuhasibu ya Kielekroniki ni muhimu sana tuiendeleze.
Mheshimiwa Naibu Spika, upo umuhimu wa kuimarisha ufuatiliaji na tathmini na mpaka sasa hivi hatujaambiwa pengine Mheshimiwa Waziri husika wakati anachangia, naye anaweza akatuambia kwamba Serikali imefikia hatua gani katika kuandaa sera ya ufuatiliaji na tathmini pamoja na sheria yake? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta ya uvuvi pia ningependa nichangie kidogo. Inaajiri Watanzania zaidi ya milioni nne. Kwa hiyo, ni sekta muhimu sana. Ukaguzi wa Ufanisi ulionesha kwamba kuna shida ya upatikanaji wa takwimu na shida ya usajili. Napenda kushauri mambo machache kwenye sekta hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, iboreshe ushirikiano na wadau wengine kama vile Wizara ya Maliasili na Utalii. Kuna baadhi ya mito na mabwawa pamoja na baadhi ya maziwa yapo ndani ya hifadhi ili Mtanzania aingie kule kwenye hifadhi kuvua, lazima alipe tozo kubwa sana kwenye TFS na TAWA. TFS ni shilingi elfu mbili kwa siku. Ina maana miezi mitatu ni shilingi 180,000. Halmashauri ikilipa shilingi 72,000 maana yake ni shilingi 252,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, huyu Mtanzania akilipa shilingi 252,000 ni nyingi sana; na TAWA ni zaidi kidogo inafika shilingi 382,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama wadau wa maliasili na utalii wangeshirikishwa vizuri, wakashauriwa, pengine wengeweza kupunguza hizo tozo ili Mtanzania akapunguziwa mzigo wa gharama za kulipa anapoingia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho, nashauri sekta ya uvuvi ianzishe ushirika wa uvuvi kama ambavyo kuna ushirika wa wakulima ili kurahisisha usajili wao na ufuatiliaji na upatikanaji wa takwimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kwa hayo machache kwa dakika hizi tano, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)