Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru nami kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika ripoti hii ya Kamati ya PAC. Niungane na Wabunge wenzangu kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais, na vilevile kukipongeza Chama cha Mapinduzi kwa kumteua mapema kuwa mgombea wa Urais kwenye uchaguzi ujao na mgombea mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi, lakini bila kumsahau Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Watanzania wanaamini kazi walizozifanya kwa kipindi hiki cha miaka mitano, vilevile, nina imani kubwa watakwenda kupata kura za kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tumekuja kujadili Kamati hii ya PAC ambayo imefanya kwa kipindi cha mwaka mmoja, nami kama Mjumbe wa Kamati hii namshukuru Mheshimiwa Spika kwa kuniamini, na nimekuwa kwenye Kamati hii ya kusimamia mashirika na mali za Serikali kwa kipindi cha miaka mitano. Kwa hiyo, amenipa heshima kubwa sana, na nimejua vitu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, leo nikitaka kukutajia watu wanao-temper na fedha za Serikali, ninawajua kwa majina na sura zao, lakini wanaofanya kazi vizuri kwenye mashirika nawajua kwa majina na sura zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali, tumekuwa tukisema sana juu ya upotevu wa fedha, lakini kwa kipindi hiki kilichopita, naona sasa kuna mwelekeo mzuri sana, matumizi ya Serikali yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa changamoto, bado zipo, lakini kuna ongezeko kubwa la ufanisi katika majukumu na usimamizi wa fedha za Serikali. Kwa hiyo, nawapongeza sana na hapa leo nilitaka kama wangekuwa wamevuruga tungewataja wezi wote ambao wanaiba hela za Serikali, lakini kwa hapa tulipofikia tumeona hatua zimechukuliwa na mambo yameenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi yetu kubwa ilikuwa ni kuisimamia Serikali, lakini CAG ana kaguzi mbili. Kaguzi ya kwanza ni ya Hesabu za Serikali na kaguzi ya pili ni ya Ufanisi. Kaguzi ya Ufanisi ina maana kwamba, kama tulitenga fedha za kwenda kuhudumia miradi ya REA na REA imekwenda kupewa fedha, tunahitaji tuone wananchi wananufaika na nishati ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kumekuwa na changamoto moja ndogo ya kuchelewa kwa miradi. Ucheleweshwaji wa miradi, kwanza unasababisha lengo la kuwafikishia wananchi huduma kwa wakati linachelewa. Hiyo ni hasara kwa wananchi, na pili, inaongeza gharama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tulikwenda kutembelea mradi mmoja wa Kahama, mradi ule umechelewa kwa kipindi cha muda wa zaidi ya miezi kadhaa. Sasa pale tumekuta kuna variation iliongezeka kwa sababu ya ucheleweshwaji wa mradi. Moja, kuna matatizo upande wa Serikali na mengine yalikuwa upande wa mkandarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naiomba Serikali, kwa kuwa tunakwenda kwenye kudhibiti fedha za Watanzania ambazo tunazitoa, ni lazima tuwe tunaangalia ni namna gani ya kwenda kuhakikisha, kama tumesaini mikataba kwa miaka miwili, tunahitaji mikataba ile ikasimamiwe kwa ukaribu, ili ikamilike kwa wakati na wananchi wetu wapate huduma. Hii inasababisha mradi kuchelewa na baadaye wananchi wanaingia kwenye hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwatolee mfano. Kuna miradi ya REA ambayo tulipewa sisi kule, ikaenda kwenye kila Kijiji, na Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwamba mwananchi ataunganishiwa umeme kwa shilingi 27,000. Miradi ikiwa kwenye kipindi cha REA, mkandarasi anapochelewa kukamilisha kwa wakati wanakwenda kuwakabidhi TANESCO, wakati muda ukiwa umebaki mchache. Wanapohamisha tu kwenda TANESCO, kuna baadhi ya vijiji wamevi-term kama miji. Kwa hiyo, wanakwenda kuwatoza wananchi shilingi 321,000 kutoka shilingi 27,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi walikuwa na nia njema, na walikuwa wanahitaji kuunganishiwa umeme, lakini mkandarasi aliwachelewesha kwa makusudi. Kwa hiyo, tunapopeleka tu TANESCO, wanaenda kuwatoza gharama kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii kelele ya vijiji, kwenye vijiji vyangu kama Goweko, Kingwa na Nsololo ambavyo vinasomeka kama vijiji, lakini wananchi wameshindwa kupata matunda na huduma nzuri ya nishati ya umeme kwa sababu ya ucheleweshaji wa wakandarasi, leo wanatozwa shilingi 320,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, nilishampelekea Mheshimiwa Waziri majina ya hivi vijiji. Kule Kingwa wanahitaji walipe kwa shilingi 27,000 kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Ile shilingi 320,000 itakuja baada ya miaka 15 huko, sisi tukiwa tumeenda kupumzika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengi ambayo Mheshimiwa Songe ameyazungumza hapa. Kuna changamoto ya umwagiliaji katika maeneo yetu, Serikali inahitaji kubadilisha kilimo chetu ili kiwe cha kisasa. Tumesaini mikataba mingi ya umwagiliaji kwenye maeneo yetu, likiwemo Bwawa langu la Goweko pale, tangu mwaka 2023. Maelekezo yalikuwa, mwaka 2023, mwezi wa Tisa, uwe umekamilika. Ule mradi mpaka leo uko chini ya 50%. Sasa huu ndiyo ule ucheleweshaji ambao tunauzungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesaini mkataba na tumepeleka fedha za advance payment, lakini leo ni miaka miwili, bado miradi hii haijakamilika. Naiomba Serikali ikamilishe miradi hii kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante.