Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupewa nafasi ya kuweza kuchangia katika ripoti hii ya Kamati. Naanza kwa kuunga mkono maazimio yote yaliyotolewa kwenye Ripoti ya Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambayo ameifanya. Imeonesha utendaji wake, ndiyo maana hata Hoja za CAG zimekuwa zikifanyiwa kazi vizuri na Maagizo ya Bunge yamekuwa yakitekelezwa vizuri kiasi kwamba, mambo yamepungua na yanaendelea kuwa mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Spika, pamoja na wewe na timu kwa ujumla, kwa kutenga muda wa Bunge kuweza kujadili kwa kina Taarifa za Ukaguzi za CAG. Taarifa ya ukaguzi wa fedha tuliijadili mwezi Novemba kwa kina kwa karibu siku tatu na leo tunajadili Taarifa ya Ufanisi pamoja na Taarifa ya Ukaguzi wa kiufundi. Ninaweza nikasema hii ni kwa upekee kabisa kwa Tanzania na kwa Bunge kutenga muda maalum kujadili ripoti za kiufundi na za kiufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaiweka Tanzania katika rekodi za dunia kwamba, Tanzania ndiyo moja ya nchi pekee ambazo zinajadili taarifa za kiufanisi. Nchi nyingi hazipati muda wa kujadili taarifa za kiufanisi, lakini sisi tunapata muda wa kujadili taarifa za kiufundi na za kiufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ripoti zote za kiufanisi na kiufundi, sisi kama Kamati, tumezijadili kwa undani na tumeona yale yote ambayo yamependekezwa na CAG na tayari Serikali inaenda kuyafanyia kazi. Kwa kweli, tuna haja ya kuipongeza Serikali na kumpongeza CAG kwa namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuhusu teknolojia. Sasa hivi ukaguzi ule wa kifedha umebadilika, na hesabu zinafungwa kwa teknolojia. Sasa hivi nchi nyingi zinahama kutoka kwenye ukaguzi wa kifedha kwenda kwenye ukaguzi wa kiufanisi. Kwa hiyo, naomba CAG na timu yake waendelee kuweka uzito zaidi kwenye kufanya ukaguzi wa kiufanisi, kiufundi na ule ukaguzi wa real time audit ambao ndiyo utatupa picha ya nini kinaendelea na nini kifanyike, ili Serikali iweze kuboresha katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, hiyo kazi kwa kweli, inafanywa vizuri, lakini ziwekwe resources zaidi katika eneo hilo, ili tupate ufanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, nichangie tu kwenye upande wa ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe ambacho sisi tuliamini kwamba, kikikamilika vijana wengi ambao hawana ujuzi na ambao wanahitaji kujiajiri wangepata maarifa na ujuzi katika chuo kile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Wizara ya Fedha watoe fedha wakakamilishe kile chuo kabla ya uchaguzi. Maana yake, kama kitakwenda mpaka baada ya uchaguzi, itakuwa ni disaster kwa kweli na tutashindwa kujenga hoja. Ili kusudi mambo yaweze kwenda vizuri, ni vema wakatoa fedha katika kipindi kilichobaki, ili kile chuo kijengwe, kikamilike, vijana waende kusoma pale na kupata aina mbalimbali za ujuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la nne ambalo nataka kupendekeza ni kwa kuwa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Marekebisho yake, Ibara ya 143, inamtamka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, angalau mara moja kwa mwaka, kufanya ukaguzi wa masuala ya fedha katika Wizara, Mashirika ya Umma, Wakala za Serikali na taasisi zinazojitegemea. Ibara hiyo inaposema angalau mara moja, maana yake nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kila taasisi lazima CAG aipitie angalau mara moja kwa mwaka. Sasa basi, kwa kutekeleza ibara hiyo na sisi Bunge tunahitaji angalau mara moja kwa mwaka kuhakikisha zile ripoti alizozileta CAG tunazipitia, kuzichambua, tunaleta mapendekezo na kuishauri Serikali namna ya kutekeleza hoja mbalimbali ambazo zitakuwa zimebainika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi sisi kama Bunge tumekuwa tukifanya uchambuzi, tunachagua taasisi chache, na kanuni zetu zinasema, tunachagua maeneo yenye matumizi mabaya ya fedha za umma ambayo yamebainishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, sasa hivi hatutakiwi kuzungumzia tu maeneo yenye matumizi mabaya ya fedha za umma, bali tunatakiwa tuhakikishe kwamba tunapitia kwa undani ili kuhakikisha yale malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa, kuhakikisha ufanisi unakuwepo na kukakikisha kwamba kila taasisi ambayo inatakiwa ipitiwe na Bunge, inapitiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumetekeleza takwa la Kikatiba ambalo Katiba yetu inalitaka. Kwa hiyo, napendekeza Bunge litenge muda wa kutosha kuhakikisha kwamba, kila taasisi ambayo inaguswa na Ripoti za CAG, basi Bunge lipate kuzipitia, kuleta mapendekezo yake hapa Bungeni na kuishauri Serikali namna ya kuboresha utendaji. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumetekeleza masuala ya utawala bora na mambo yatakwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono Hoja za Kamati. Ahsante sana. (Makofi)