Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. STEPHEN L. BYABATO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza naanza kwa kuunga mkono hoja. Pia, naunga mkono hoja za wachangiaji wenzangu walionitangulia, Wajumbe wa Kamati wenzangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, namshukuru sana Mheshimiwa Spika, pamoja na wewe, kwa kunipa nafasi ya kuhudumu katika Kamati hii nyeti kabisa, ambayo inaendelea kutazama namna ambavyo Serikali inatumia fedha za wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naungana na wenzangu kumpa pongezi nyingi sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi yetu ambayo tuliifanya tarehe 19 kwake yeye, Dkt. Nchimbi, pamoja na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii imetokana na kazi ya Bunge hili kuisimamia Serikali na miradi ikatekelezwa. Mwisho wa siku, sasa tunaona Watanzania wote kwa ujumla, sisi tukiwa wawakilishi na wajumbe, tunasema Mheshimiwa Dkt. Samia aendelee, na hiyo mitano tena, inasemwa na kila mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninao mchango mmoja tu kwa leo. Katika Bunge la Bajeti, mojawapo ya eneo ambalo nitachangia ni kuomba fedha ya CAG iongezwe, ili aweze kufanya kazi yake vizuri zaidi kwa kuwa sasa hivi kazi aliyonayo ni kubwa, kwa sababu ya mambo makubwa ambayo Serikali ya Awamu ya Sita inayafanya. Sasa ni lazima pia tumwongezee nguvu ya kuhakikisha anafika kwenye kila eneo na kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tunafahamu, sasa hivi zaidi inafanywa technical na performance audit ambayo tunaizungumzia hapa. Nadhani sasa tunahitaji kwenda kwenye kufanya real time audit ambayo Mheshimiwa Hasunga ameisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tuhame kutoka kwenye utaratibu wa sasa wa mkandarasi kupewa ushauri na mshauri. Tuwe na design and build ya mtu mmoja, ambaye tutaweza kumbana yeye mwenyewe kirahisi. Hii itatusaidia kupunguza matatizo mengi ambayo Kamati tumeyaona kwenye ucheleweshaji wa miradi, miradi kutokukamilika kwa wakati na mmoja kumsingizia mwingine kwamba kazi haijafanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa tunafanya design and build, maana yake ni atabeba mzigo wote mtu mmoja, lakini tukiwa na real time audit, auditor atakuwa anakwenda hatua kwa hatua na kuona ni wapi ambapo tunachelewa na tunaweza kukamilisha kazi kwa wakati. Kwa kufanya hivyo, itatusaidia sasa miradi mikubwa mizuri ambayo tukonayo kwenye maeneo mbalimbali, iweze kuwa na tija na kuwafikia wananchi kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hapa kwenye Uwanja wetu wa Msalato, tuna ucheleweshwaji wa mradi. imeongeza mpaka na fedha zinazodaiwa. Tutakuja kupata shida ya kuzilipa na fedha hizo zingeweza kufanya mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo hiyo, pale Bukoba Mjini, mimi nimepata kujengewa control tower, lakini bado haijaanza kwa sababu ya mazingira haya haya ya kuchelewesha, lakini Mheshimiwa Dkt. Samia tayari ameshatoa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye eneo la mwisho, ili nikimbizane na muda. Mimi kwetu nimepata miradi mingi sana ambayo imetokana na azma kubwa ya Mheshimiwa Dkt. Samia ya kuwahudumia wananchi. Ni jana tu Mheshimiwa Mchengerwa ametupa jeuri na afya mpya, nami nasema, kule kwetu umetangazwa mradi wa ujenzi wa soko jipya, Mradi wa Ujenzi wa Kingo za Mto Kanoni, Mradi wa Ujenzi wa Barabara na Mradi wa Kujenga Stendi ya kisasa, ambayo kwa miaka mingi sana imekuwa ni miradi ambayo haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inshaallah, ninaamini Bunge linalokuja nitarudi hapa, kwa sababu, wananchi wangu tayari wameshaona nimefanya kazi vizuri. Sasa, ili niweze kurudi kirahisi na Mheshimiwa Dkt. Samia ametoa fedha na ameshampa CAG fedha ya kuanzia, basi tuwawezeshe fedha ya kufanya real time audit, ili hii Miradi ya Bukoba Mjini niliyoisema, ambayo niliiahidi kupitia kwa Mheshimiwa Dkt. Samia iweze kutekelezwa na kukamilika, ili wananchi waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwetu sasa slogan ni mpya. Kama unataka kuwa Mbunge wa Bukoba Mjini, utueleze Byabato ameshindwa nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii ni jeuri ya Mheshimiwa Dkt. Samia. Mimi nasema tumwongezee nguvu CAG ili mimi pamoja na wenzangu turudi tuendelee kuwatumikia wananchi kwa misingi ambayo tuliiahidi tangu mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, naunga mkono hoja, na Mwenyezi Mungu atubariki sote. Ahsante sana. (Makofi)