Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Muda hautoshi, lakini naomba niongee machache.

Mheshimiwa Naibu Spika, namna pekee ambayo tunaweza kuisaidia Serikali ni kwa kuishauri mambo kadha wa kadha. Namshukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kunichagua kuwa mmoja kati ya Waheshimiwa Wabunge ambao tumekuwa tukishiriki katika hii Kamati ya PAC, kwani imenipa nafasi ya kuona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mjumbe mmoja hapa ameeleza akasema, leo naweza kujua ni wangapi na akina nani wamekuwa wakitumia au wameshindwa kusimamia vizuri fedha za umma au ni wangapi wamefanya vizuri. Namshukuru Mungu nami ni kati ya wale. Kwa hiyo, naweza pia kujua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, kwa sababu ya muda, changamoto kubwa tuliyoiona katika ukaguzi tulioufanya au katika taarifa mbalimbali za CAG ambazo tumekuwa tukizisoma ni changamoto ya usanifu wa miradi. Kumekuwepo na tatizo kubwa sana katika miradi ambayo Serikali imekuwa ikiifanya, imekuwa ikikosewa, na eneo hili ndiyo limekuwa liki-attract riba.

Mheshimiwa Naibu Spika, humu ndani tungekuwa tumeongelea ku-accumulate interest, miradi na nini, lakini changamoto kubwa ya gharama za miradi kuongezeka, imetokana na changamoto ya usanifu. Mpaka wakati nasoma ripoti, kwa interest ya muda, nikajiuliza, hivi wataalam wetu wana shida gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakupa mfano mdogo kwa Mradi wa Msalato. Wanasema wakati wanafanya usanifu, walivyokuwa wanafanya survey walitumia drones na walivyotumia zile drones, wakati zinapita juu kuangalia lile eneo na kufanya estimate kulikuwa na vichaka. Eneo lilikuwa halijasawazishwa na halijalimwa. Kwa hiyo, zile drones zikakosa accurate information na huo mradi ukaongezeka thamani. Sasa najiuliza, hao wataalam wetu walisoma vizuri kuhusu namna ya kufanya hizo studies? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni lazima tulifanye kazi hili eneo. Kwa sababu hiyo ya kutumia drones, wakati hawajasafisha eneo, imeongeza gharama ya zaidi ya shilingi bilioni tatu kwenye huo mradi na mkandarasi akiwa ameongeza fedha zaidi ya shilingi bilioni tano ambapo, hizo fedha tungeweza kufanya usanifu vizuri, zingeenda kuwasaidia wananchi wa Kyerwa ambao kila siku nimekuwa nikiongelea changamoto yao ya maji. Hilo ni eneo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu eneo la pili ni la usanifu wa miradi. Tumefanya ziara na CAG tukaona Miradi ya Maji ya Mwanza (MUWASA). Unakuta thamani ya mradi, let us say ni shilingi bilioni 30 au mpaka shilingi bilioni 70, lakini wameshamaliza kutengeneza, maji yanapaswa kutoka. Kumbe hayo maji jinsi walivyokuwa designed walitegemea umeme wa kawaida wa TANESCO ambao una mgao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mradi umekamilika, lakini chanzo cha maji kina mgao, na wananchi hawawezi kupata maji. Sasa katika usanifu wa mradi, hao watu walijiuliza kwamba, ili mradi uweze kurudisha thamani ya fedha, ni lazima tuwe tumeweka source ya power ili maji yaweze kuwa generated? Hiyo ni changamoto nyingine ya usanifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hiyo tu, kuna mradi mwingine ambao unatoa maji Ziwa Victoria kuleta Singida na Shelui, nao una changamoto zilezile, usanifu mbovu. Kwa hiyo, kama naweza kuishauri Serikali kwa neno moja, hebu kama kuna changamoto ya wataalam wa kusanifu miradi, basi tuangalie namna nzuri ya kuwaelimisha ama kuwafundisha ili tupunguze gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni kuhusu usimamizi wa mikataba. Ukija kuangalia eneo ambalo Serikali imepigwa pakubwa na imepoteza fedha nyingi ni kwenye eneo la usimamizi wa mikataba. Sisi haya mambo tunayasema kila siku na tunachoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia masuala yanayotokana na riba nyingi za wakandarasi ambazo tunaongelea ni kwa sababu, wakati unapofika wa kulipwa fedha, hawalipwi kwa wakati, hivyo kunakuwa na gross interest. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia mfano mmoja wa Mradi wa Msalato, kwa sababu ya kucheleweshewa malipo, huo mradi ume-attract interest ya zaidi ya shilingi bilioni 300. Kwa hiyo, sasa ni lazima Serikali isimame vizuri. Kama tunataka kutumia fedha na tupate thamani ya fedha, ni lazima tujipange vizuri kwenye eneo la mikataba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni kuhusu taratibu za manunuzi. Humu ndani kichaka kikubwa cha matumizi ya fedha za umma kinachofanya miradi isikamilike na ipigwe, ni kukiukwa kwa Sheria ya Manunuzi. Serikali imekuja na utaratibu, na Maafisa Masuuli wanajua ni utaratibu gani wanapaswa kuutumia kwa ajili ya kufanya manunuzi, lakini taarifa nzima ya mwaka mzima kila tunakopita ni Afisa Manunuzi hajafuata Sheria za Manunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nishauri katika haya maeneo matatu. Kama tunataka tufanye vizuri na kama Serikali imekuwa ikikopa fedha ambazo zinalipwa na walipakodi, ikiwa haya maeneo matatu hayawezi kusimamiwa vizuri tutapigwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sijajua kama muda wangu umebaki, lakini tumekuwa na special audit mbalimbali na mojawapo ambayo nitaisema, na kwa sababu ya interest ya muda, ni special audit inayohusiana na vifaatiba. Serikali ilitoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 68 kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya zahanati kwenye local government zaidi ya 22.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za walipakodi shilingi bilioni 68, lakini CAG alivyoenda kufanya hiyo special audit aligundua mashine kadha wa kadha hazifanyi kazi, hazijafungwa na hakukuwa na wataalam husika. Kilichoniumiza zaidi, hizi mashine tangu zimetoka huko nje, zimeshushwa bandarini na zimeenda kufungwa kwenye vituo, hazikuwahi kufanyiwa calibration au kuwa tested kuona effectiveness na efficiency ya hizo mashine, ukiachana na kwamba bado kuna maeneo mengine yana hivyo vifaatiba, lakini hakuna wataalam. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Haya, ahsante Mheshimiwa.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, muda ni mchache. (Makofi)