Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, pamoja na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha Sekta ya Elimu, bado mfumo wetu wa elimu hautengenezi wahitimu wenye weledi na umahiri mkubwa kwa sababu hauzingatii shauku ya kujifunza kwa wanafunzi na vilevile hauzingatii vipaji vya wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Profesa Howard Gardner wa Chuo Kikuu cha Harvard ameandika kitabu kinaitwa Frames of Mind. Katika kitabu chake anasema wanadamu wana vipaji vya aina tisa, mimi nitavitaja sita ambavyo ni:-
(i) Uwezo wa kuzungumza na kuandika;
(ii) Kutunza mazingira;
(iii) Kucheza michezo ya aina mbalimbali;
(iv) Sanaa ya ubunifu;
(v) Ushirikiano na mahusiano katika jamii; na
(vi) Kazi za mikono na ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya mifumo yetu ya elimu na malezi inadumaza vipaji, uwezo na karama za wanafunzi kwa sababu inawalazimisha wasome masomo yasiyoendana na shauku zao pamoja na vipaji. Uzoefu unaonesha watu waliofanya mambo makubwa duniani wamefanya mambo wanayoyapenda moyoni na yanayozingatia vipawa vya asili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni nini? Tukiwalazimisha kwa mfano, kama mzee ni daktari anataka na mwanaye awe daktari, kama ni mhasibu anataka mwanaye awe mhasibu; hatari yake ni nini? Inaathiri ari ya kujifunza na ubunifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Serikali imezindua sera mpya ya elimu. Hata hivyo kwa maoni yangu, utekelezaji wake unahitaji kiwango kikubwa sana cha fedha ili kuwaandaa walimu wenye ujuzi, ujenzi wa maabara za kisasa na karakana za ufundi. Ili tuweze kukabiliana na tatizo hilo napendekeza tufanye mambo mawili ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza; Serikali itumie ipasavyo Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuandaa walimu kwa mafunzo hasa katika mbinu za kisasa za kufundishia na hapa ninasisitiza matumizi makubwa ya teknolojia ya kisasa na ubunifu katika elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wanaweza kutumia projector, wanaweza kutumia kompyuta na wanaweza kutumia mitandao kuwaonesha watoto majaribio mbalimbali ya kisayansi na kiufundi bila ya gharama kubwa. Unaweza kuwaonesha watoto jinsi damu inavyotembea kwenye mwili, unaweza kuonesha jinsi mimea inavyotengeneza chakula kwa kutumia nishati ya jua na unaweza kuonesha jinsi miti inavyosaidia kutengeneza mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ninaiomba Serikali ihimize matumizi ya mazingira ya shule na sayansi ya nyumbani katika ufundishaji. Kwa mfano, tunaweza kufundisha masomo ya sayansi kwa kuonesha watoto jinsi nishati ya jua inavyotumika katika shughuli mbalimbali za binadamu kama vile usafi wa mwili na utunzaji wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kujenga Taifa linalojitegemea elimu yetu inapaswa kujengwa kwa misingi ya kujitegemea kama alivyosema baba wa Taifa hili. Misingi ambayo inazingatia si mafunzo ya ufundi peke yake bali mafunzo ya sayansi na teknolojia, ubunifu, ugunduzi, na ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalisema hili suala la elimu la kujitegemea kwa sababu ninasikitika sana kwamba tuna vitivo vya kila aina vya uhandisi lakini bado haviwezi kutoa majibu ya masuala ya msingi ya matatizo ya Taifa letu. Nitatoa mifano mitatu. Mfano wa kwanza, tuna mwanga wa jua kila mahali wahandisi hawatusaidii kubuni teknolojia inayoweza kuvuna mwanga ili nishati ya mwanga itumike katika kilimo cha umwagiliaji maji na kuendesha pampu za kusukumia maji na matumizi ya nyumbani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa pili, tunaagiza mitungi ya gesi kutoka nje, tunaagiza majiko sanifu wakati tuna wahandisi wa kila aina. Mfano wa tatu, tuna wahandisi wengi lakini bado madaraja na mejengo mbalimbali katika nchi yetu yanajengwa na watu kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natafakari nikasema, kwa nini katika anga kuna hewa ya Hydrogen ya kutosha lakini wahandisi hawaivuni tukaweza kuitumia kama nishati? Ninalisema hili kwa sababu hivi karibuni kuna kijana mmoja Zimbabwe amebuni teknolojia ya kuvuna mawimbi ya redio yanayotumika kuendesha gari badala ya mafuta. Kwa nini lisiwezekane hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwa maoni yangu kuna haja ya kuangalia muundo wa vyuo vikuu vyetu vya Tanzania ili visisitize mafunzo ya vitendo zaidi kuliko nadharia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapendekeza tuwe na vyuo vya aina tatu. Kwanza tuwe na vyuo vikuu vya utafiti (research universities), pili tuwe na vyuo vikuu vya mafunzo ya kazi mbalimbali (professional studies), na mwisho tuwe na vyuo vikuu vya sayansi na teknolojia (universities of applied sciences and technology).
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)