Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa pili katika hotuba hii ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kipekee niungane na Watanzania wenzangu kuipongeza Klabu ya Simba, benchi la ufundi, uongozi na mashabiki wote waliokuwa nyuma ya timu na hatimaye jana timu ya Simba imetuheshimisha kwa kiwango kikubwa maana ilikuwa ni timu pekee inayotoka ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati iliyokuwa imebaki kwenye mashindano haya, kwa hiyo imevuka imetupa heshima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai na kuiomba Serikali. Jana baada ya mechi nadhani ndani ya saa moja tuliona tangazo linazunguka wakisema kwamba Uwanja wa Benjamini Mkapa umefungiwa na hautatumika katika mechi tena. Sasa kama Ulega ameishi njiani kule Mikoa ya Kusini ikafunguka, tunachoomba Serikali ifanye jitihada zinazowezekana ili uwanja ule urejee kwenye hali yake na mechi za tarehe 20 zichezwe pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amekuwa champion mkubwa na motisha hiyo wanayoipata wachezaji wakafanya vizuri katika klabu zetu ni kwa sababu yuko nyuma yao. Itakuwa ni jambo la ajabu na aibu nusu fainali hii ikachezwe kwenye nchi nyingine wakati nchi nyingine zimekuwa zinakimbia kucheza mechi zao. Kwa hiyo, tuombe hilo Serikali ilifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo naomba nirejee katika mchango wangu. Mtunga Zaburi anasema, “Wako wapi wazee na watu wenye busara waliyoyaona matendo makuu haya ya bwana na hatimaye wawakumbushe vijana na watu wengine ambao hawakuyaona wayafanyie kazi na hatimaye wapate kuyajua.” Kwa nini ninayasema haya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021 Mheshimiwa Rais Samia alipoingia madarakani mpaka sasa ametimiza miaka minne. Yapo mambo ambayo yamefanyika mwaka 2021, wazee na watu wenye hekima wasipowakumbusha ambao hawakuyaona wakati ule au waliosahau tutakuwa hatumtendei haki Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu yamesemwa mengi, yamefanyika mengi na tunaenda kwenye uchaguzi; haikosi kuna watu wamesahau. Kwa hiyo, ninataka nichukue wito huu nikumbushe baadhi ya mambo makubwa ambayo yamefanyika katika wakati huu. Hata hivyo, licha ya haya mambo kufanyika na yametajwa katika Hotuba ya Waziri Mkuu bado mambo mengine makubwa yamefanyika kwenye majimbo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na miradi mikubwa ya kitaifa kama Bwawa la Mwalimu Nyerere, reli ya kisasa ya SGR, tukawa na Daraja la Kigongo Busisi, tumekuwa na Daraja la Tanzanite, tumekuwa na Daraja la Mto Wami na flyover nyingi zimejengwa. Pia tuna key issues ambazo zimefanyika katika kipindi hichi cha miaka minne. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, 2022 tulikuwa na sensa ya watu na makazi. Sensa haijitokezi kila wakati lakini pesa nyingi ambazo zimeenda huko, ambazo zingeweza kufanya miradi mingine, lakini zimetumika kwenye hili zoezi. 2024 tumekuwa na uchaguzi, vyote hivi vinafanyika kwa fedha za ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023/2024 tulipata janga la El-Nino na hatimaye nchi wakaweza ku-stabilize ikarudi kwenye mahali pake. Sasa mambo yote haya makubwa ambayo yamefanyika huenda watu wameyasahau na leo tunapoelekea kwenye uchaguzi mwingine anaweza akaangalia kiti kimoja akasema hiki, hiki na hiki. Ni lazima tuelewe nchi imekuwa engaged kwenye vitu vikubwa. Pia, tuko tunajenga viwanja kwa ajili ya AFCON na mambo mengine makubwa yanayoendelea katika Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo yote haya, Wabunge katika kipindi cha miaka minne tumesimama ndani ya Bunge tukifanya uwakilishi wetu kwa wananchi waliotutuma. Yaliyo mengi yamefanyika kwa sababu Serikali pamoja na kuwa na miradi mikubwa haikutuacha Wabunge, ilitusikiliza. Sasa kwa sababu naongea kwa niaba ya wananchi wa Biharamulo ninataka nitaje baadhi ya vitu ambavyo ninaamini hata Wabunge wengine kwenye maeneo yao vimetajwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwakumbushe ile habari ya mtunga Zaburi akihusia watu wazee na wenye busara waliyoyaona yale yanafanyika wakumbushwe. Haikosi kuna mtu mwingine aliona barabara haikuwepo, lakini sasa hivi akipita hajui kama kulikuwa na shida ya barabara. Mara nyingi nimekuwa nawakumbusha watu hata ule Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Terminal Three ulipojengwa pale zamani kilikuwa ni kijiji cha kipawa kile. Watu waliondoka pale, mtu mpya akiingia pale anaona uwanja ha-imagine kwamba kuna watu waliwahi kuishi pale miaka ya 2000 mpaka 2005. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa mfano kwangu tu miradi ya maji ambayo imefanyika kwangu kwenye habari ya vijijini. Katika muda wa miaka hii minne tumepokea shilingi bilioni 8.8 katika miradi ambayo imeshatekelezeka na nina miradi mingine ya takribani shilingi bilioni 5.19 inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Biharamulo Mamlaka ya Maji nina 3.3 billion. Ukipiga tu hesabu hapo ni karibu shilingi bilioni 17 ambazo Biharamulo peke yake tumepokea kwenye miradi ya maji. Tumeongeza idadi ya distribution ya watu ambao walikuwa hawapati maji na hatimaye wamepata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea habari ya shule. Mwaka 2020 shule za msingi nilikuwa nazo 98, lakini leo nina shule za msingi 117, ongezeko la shule mpya 19 za msingi; sio kazi ndogo. Nakumbuka nilipoingia nilikuwa nina Shule moja ya Msingi Nemba - Biharamulo ilikuwa na wanafunzi 5,259 shule moja ina madarasa tisa. Leo ninapoongea tumetoa shule nne mpya pale. Kwa hiyo, yote hayo ni mambo makubwa ambayo yamefanywa na Serikali na ni lazima tujivunie nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda katika habari ya afya. Nilikuwa na zahanati 18 sasa hivi nina zahanati 26, ongezeko la zahanati nane mpya katika miaka hii minne. Vituo vya afya nilikuwa navyo sita sasa hivi ninavyo saba. Sikuwa na Hospitali ya Wilaya lakini tayari ninayo moja. Unaweza ukaona commitment ya Serikali, pamoja na kufanya mambo makubwa, lakini bado kwenye majimbo tumeendelea kuhudumiwa na miradi ile ya kiwilaya na kimajimbo imeendelea kuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee habari ya barabara katika jimbo langu la Biharamulo, wakati Mheshimiwa Rais anaingia pesa niliyokuwa napokea Biharamulo ilikuwa ni milioni 670 tu kwa ajili ya barabara, leo hii naposimama hapa na 2.467 billion ninayoipokea kutoka milioni 670.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kuona commitment barabara za lami tulizokuwa nazo Biharamulo ilikuwa ni kilometa 4.59, leo nina kilometa 10.18 ongezeko la zaidi ya kilometa tano kwa miaka hii minne. Barabara za changarawe nilikuwa na kilometa 111, sasa hivi nina kilometa 275. Tumepunguza barabara za udongo kutoka kilometa 391 ni kilometa 222 zilizobaki na kazi inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, box culvert hatukuwa nayo hata moja, sasa hivi nina box culvert tano zimejengwa Biharamulo. Pia line culvert nilikuwa nazo 415 sasa hivi nina 618 na tumefungua barabara mpya kilometa 191 zilizojengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu habari ya umeme 2020 ni vijiji 46 pekee ndiyo vilikuwa na umeme lakini sasa hivi nina vijiji 74 ndiyo vyenye umeme na vitongoji 15, sasa hivi muda siyo mrefu mkandarasi anaingia site. Kwa hiyo kwangu vijiji vyote vimefikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nimeamua niyaseme haya? Ninayasema haya kwa sababu ni lazima tuwapongeze mawaziri wametushika mkono. Wabunge tumeongea humu lakini Mawaziri waliyasikia kutokea ndani ya Bunge wakapeleka hatimaye wakatuletea hizi fedha. Kwa hiyo, kama hatuwezi kuyaona hata haya tukashukuru hatutakuwa tunawatendea haki na kuitendea haki Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa mwenye hii hotuba ni Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tunapoyaona haya yanafanyika Waziri Mkuu amekuwa anafikika, Waziri Mkuu amekuwa ni mtu mwenye ushirikiano kwa Wabunge kama Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Wabunge tume-address kwa Serikali na kuongea nayo kupitia ndani ya Bunge hili, Kiongozi Mkuu wa shughuli hizi akiwa Waziri Mkuu. Kwa hiyo ni lazima tumpongeze na kuona kwamba commitment yake katika kusikiliza hoja za Wabunge imekuwa kubwa hatimaye mambo haya waliyoyasikia katika Bunge wakaenda kuyajadili katika Baraza na kuyapeleka kwa Mheshimiwa Rais hatimaye pesa zikamwagika, zikaja, zikafanya miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipee pia nimpongeze Waziri Mkuu, kwa sababu siyo rahisi nadhani ni Waziri Mkuu wa kwanza ambaye ametumika katika Serikali mbili na Marais wawili full time, akitumika katika Serikali ya Awamu ya Tano kama Waziri Mkuu na ametumika katika Serikali ya Awamu ya Sita kama Waziri Mkuu mpaka sisi tunamalizia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii, uaminifu wake na commitment yake katika kuwasaidia Marais hawa wawili ni kubwa. Kwa hivyo, kipekee kwa niaba ya wananchi wa Biharamulo nichukue nafasi hii kumpongeza na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumhifadhi na kumlinda ili hatimaye commitment hii ambayo umeionyesha Mungu wa Mbinguni akamlipe mara dufu hatimaye tumuone tena wananchi wa Ruangwa wakimuamini na kumpa nafasi nyingine tena ya kuja kushiriki hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nikushukuru kwa nafasi na niseme kwamba naunga mkono hoja, ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)