Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hotuba hii ya Bajeti. Ninaungana na mchangiaji aliyemaliza Mheshimiwa Chiwelesa kuwapongeza sana timu ya Simba kwa ushindi wa jana chini ya mgeni rasmi, Mheshimiwa Jumaa Aweso, hakika Jumaa Aweso ameona namna gani timu ya Simba inafanyakazi nzuri na kama methali yake ambavyo amekuwa akisema ‘anayejua hali ya mgonjwa ni yule aliyelala nae kwa sababu anajua mihemo yake’ kwa hiyo Mheshimiwa Aweso amesikia mihemo ya Simba na tunaiombea Simba kwa ajili ya nusu fainali ambayo iko mbele yao.(Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anazozifanya na kwa namna anavyopambana kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata maendeleo, katika kazi nzima ya kutafuta fedha katika majimbo yetu na katika nchi yetu kama ambavyo Mheshimiwa Ezra, amesema hapa, miradi mikubwa ambayo sasa imekamilika na mingine imeanza kazi ikiwemo SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo tunaenda kupata megawatts 2,115 itakayosababisha kuwa na megawatts 4,031 katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni maendeleo makubwa na ni pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan. Angalia daraja la Busisi na lenyewe ni kama limekamilika muda siyo mrefu litaanza kutumika. Hii miradi ilikuwa ni mikubwa na mingine ilikuwa inatumia fedha zetu za ndani, ninampongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii na mimi nataka niwaambie watanzania Mama Samia tunae na tunatamba nae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais lakini pia nimpongeze sana mwenye hotuba, Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu mimi nikupongeze sana kwa kazi unayomsaidia Mheshimiwa Rais, Wabunge hatuna mashaka na wewe tunajua utendaji wako wa kazi mkubwa na tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kukuamini wewe na kuendelea kuchapa kazi kwa ajili ya watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona anavyotembelea Halmashauri zetu, pale unapokuja wewe tunaona mabadiliko makubwa sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu, ulikuja pale kwangu sikumbuki nafikiri 2022 au 2023, tukaanza kujisifia heeeee! Kumbe unatusubiri tu, dakika mbili mbele Mheshimiwa Waziri Mkuu unauliza kwa nini milioni kadhaa hazikupelekwa kwenye akaunti? Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli umeendelea kuzisaidia sana Halmashauri zetu, umeendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa majukumu ambayo umeendelea kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba tu wananchi wa Ruangwa kwamba waendelee kukuamini, ni mchapakazi na mimi niwaambie bado tuna wewe na tunatamba na wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu. Pamoja na hayo Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na pongezi hizo tunatambua mambo makubwa uliyoyaeleza kwenye hotuba yako, tunatambua sekta mbalimbali ulizoeleza kwenye hotuba yako, tunaona maendeleo makubwa sana kwenye nchini yetu, tunaona namna gani nchi yetu imeendelea kupiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kadri tunavyoendelea tutakuwa pazuri zaidi, tukiona sasa hata uchumi wetu wa nchi unazidi kuimarika, ninamkupongeze wewe kwa namna unavyoendelea kumshauri Rais, niwapongeze Mawaziri kwa namna mnavyoendelea kumshauri Waziri Mkuu katika utekelezaji wa majukumu yake hakika nchi yetu sasa iko vizuri na maendeleo ni kemkem, ‘ma-ti’ na ‘ma-bi’ yameendelea kuwepo kwenye majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Busega kama Busega tumenufaika na fedha nyingi. Tukisema tuanze kutaja hapa Mheshimiwa nitahitaji nusu saa katika mchango wangu ili niyataje yale ambayo yamefanyika kwenye Jimbo letu la Busega. Tumeona tulikuwa na Hospitali ya Wilaya na sasa tulipokea zaidi ya bilioni nne na Hospitali ya Wilaya sasa inafanyakazi, haya ni mapinduzi makubwa na wanabusega wanasema Mheshimiwa Rais wanae na wanatamba nae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo pia barabara zimefunguka kwa kiwango kikubwa sana, bajeti yetu ya 2020 ilikuwa milioni 714 na sasa tunavyozungumza kila mwaka kuanzia 2021 mpaka sasa tumekuwa tukipata bilioni mbili na milioni mia saba hii ni hatua kubwa na Busega sasa imefunguka na haya yote ni mapenzi makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan, tunae na tunatamba nae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo tumepata shule za msingi mpya za kisasa shule mbili na shule za sekondari mpya mbili. Haya ni mafanikio makubwa kwa wananchi wa Busega, nina imani kwamba kazi kubwa iliyofanywa na Serikali wananchi wa Busega watazidi kuiunga Serikali yao ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama Samia na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo tumepata Vituo vya Afya vya kutosha ambavyo Jimbo letu la Busega wameendelea kunufaika, tunaishukuru Serikali imeendelea kutuletea wahudumu wa afya wakiwemo madaktari lakini pia tuendelee kuiomba, kuendelea kuimarisha eneo la watumishi ili sasa vituo vya afya ambavyo tayari vimejengwa na Serikali yetu pendwa sana ya Awamu ya Sita viendelee kutoa huduma iliyo na tija kwa wananchi wa Jimbo la Busega na wananchi wa Tanzania nzima. Hii ni kufatana na upatikanaji wa wahudumu katika vituo vyetu ambavyo vimejengwa, wakiwemo madaktari, wakiwemo manesi na watu wengine ambao wanahitajika kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Kata moja ya kimkakati, Kata yetu ya Kabita pale Nyamikoma. Tulishaleta pendekezo letu kama wananchi wa Busega kwa ajili ya kituo cha afya, ni imani yangu sasa bajeti itakapokuja ya TAMISEMI, eneo hili sasa ni eneo muhimu ili Wananchi wa Kata ya Kabata wapatao zaidi ya 36,000 wapate huduma ya kituo cha afya ili wao sasa na kata zingine za jirani kama Kalemela waweze kufikiwa na huduma ya karibu ya kituo cha afya katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulipata mafuriko pale Lamadi na mafuriko haya yalisababishwa na magugu maji ambayo yamevamia Ziwa pamoja na Mto Lamadi ambao ulisababisha Ziwa Victoria kujaa kwa maeneo yale na maji sasa kurudi kwa wananchi ambao wananchi wetu walipata hadha kidogo. Sasa tulishaandika andiko letu kwa ajili ya milioni 118 ya kutoa magugu maji kwenye mto pale, Mto Lamadi. Tunaomba sasa Wizara husika itakapokuja ije ione namna gani inawasadia wanabusega kwa sababu maafa haya hayabishi hodi siku nyingine tuondokane na hadha hii tupate hizo fedha kwa ajili ya kujenga mitaro lakini kwa ajili pia kutoa magugu maji kwenye eneo hili la Lamadi na wananchi wa Lamadi waweze kuishi salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja hayo Mheshimiwa Waziri Mkuu pale Busega tumeanza ujenzi wa VETA, tunaishukuru sana Serikali yetu ya Awamu ya Sita kwa ajili ya Ujenzi wa VETA lakini kwa kweli sasa una muda mrefu umesimama takribani miezi sita. Tunaomba sasa wizara yetu, Wizara ya Elimu iangalie namna gani VETA hii inakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kuitumia na value for money iendelee kuonekana kwa wananchi wetu kwa sababu VETA hizi zilijengwa kwa ajili ya vijana na zilijengwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yetu sasa zitakapokamilika zitaleta tija kwa vijana ambao watakuwa wamesoma katika maeneo yale na katika wigo mzima wa kupata ajira, wananchi wetu watapata ajira na itaweza kuwasaidia kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukushukuru sana kwa kuendelea kutupa nafasi hii ili tuweze kuchangia na kuona mustakabali mzima wa bajeti ilivyo salama ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mimi sasa niungane na Waziri Mkuu kuunga mkono hoja hii na tumpitishie fedha alizoomba ili waweze kutekeleza majukumu yao, niwapongeze sana Mawaziri mnaomsaidia Mheshimiwa Lukuvi, Ridhiwani na Manaibu Waziri mnaosaidia hii Wizara ya Waziri Mkuu, tunaimani kubwa pamoja nanyi na mimi niungane nanyi kupitisha bajeti yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nirudie tena Mheshimiwa Rais tunae na tunatamba nae wananchi wa Ruangwa Mheshimiwa Waziri Mkuu tunae na tunatamba nae na tunampongeza kwa kazi, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)