Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hii bajeti ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takribani zaidi ya miaka tisa sasa nimekuwa nikilalamika sana kwa zao la chai, zao la parachichi na mara nyingi sana hata Waziri Mkuu alipotembelea katika Mkoa wetu wa Mbeya mimi nilikuwa sikosi na nikilalamika na nikitoa malalamiko mbalimbali juu ya wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema namshukuru Mungu baada ya malalamiko haya ya muda mrefu mwezi huu Mheshimiwa Bashe kama Waziri mwenye dhamana ya Kilimo ameweza kutoa nafasi na kutoa elimu na kutoa tamko kwa ajili ya kuwasiliza wakulima hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa mara ya kwanza ninaipongeza na ninampongeza waziri kwa maana yeye anafanya kwa niaba ya Waziri Mkuu kwamba ameweza kujibu kilio cha wakulima wa parachichi. Mwaka huu ulikuwa mwaka mbaya sana kwenye mazao, parachichi ziliuzwa vibaya lakini Mheshimiwa Waziri ameamua kuja na suruhisho na ninapenda niwaambie Wabunge waelewe ni nini alisema kwenye siku ya wadau wa parachichi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe pia kama Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo ulikuwepo. Baada ya kuona kilio kikubwa sana na uharibifu wa zao hili likiendelea Mheshimiwa Waziri ametoa maelekezo mahsusi na ninaamini Waziri Mkuu atakapopitishiwa bajeti hii ataenda kutekeleza yale ambayo waziri wa dhamana ameyasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ameweka kitu kinaitwa (COPRA) amewekea nguvu kwa watu wa (COPRA) waweze kusimamia tasnia hii ya parachichi kwa kumuweka dada Hellen kuwa ndiyo msimamizi pale na tunaamini tunamwamini dada huyu wa sababu wanawake wakiwa na jambo lao huwa wanafanya vizuri kwa hiyo tunaamini Ndugu Hellen atasimamia (COPRA) na atafanya maagizo ambayo Mheshimiwa Waziri amempa na sisi tutamsaidia kuhakikisha anatimiza wajibu huo kwa wakulima wa parachichi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ameona kuna umuhimu Mheshimiwa Waziri Bashe kununua magari zaidi ya 18 ya kuchimba visima kupeleka kwenye mashamba ya parachichi hii, ni kwa mikoa 6 inayolima parachichi. Hili ni jambo kubwa sana na la muhimu kwa wakulima kwa sababu tumesema parachichi ni zao la kijani ni dhahabu ya kijani inaleta uchumi na inaongeza Pato la Taifa, basi wazo hili la Mheshimiwa Bashe kutoa fedha na anasema ifikapo Aprili 30 magari haya yatakuwa tayari mimi nipongeze kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna fahamu kabisa kwamba mbolea na viatilifu kwa ajili ya parachichi sasa hivi Mheshimiwa amesema vitatoka kama ruzuku na fedha yake ipo tunaamini inakwenda kutekelezeka na wakulima sasa wataenda kufanya. Wajibu wa mkulima sasa uliobaki ni kusimamia mazao hayo kwa uangalifu kwa sababu suala siyo kupanda tu mche na kuacha ni lazima usimamiwe na kufika kwenye viwango vya kimataifa ili tunapodai soko basi soko letu lipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa Mheshimiwa Bashe amezungumzia suala la kuongeza Maafisa Ugani. Ni ukweli usiyopingika kwamba Maafisa Ugani hawatoshi lakini mwisho wa siku kwa sababu zao hili limekuwa la kimkakati basi amefikiria kuna namna ya kuongeza na kuhakikisha vijana hawa wanakuwepo kuwasaidia wakulima wetu, mimi kwa hilo ninapongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo suala la soko tumekuwa na soko la Ulaya kwa muda mrefu lakini tumepata taarifa kutoka wizarani kwamba sasa India na China wanakwenda kununua parachichi za wakulima. Kwa hiyo, suala la kuwa na mazao yanaozea mashambani pale kwetu sisi kama wakulima na tunaowasimamia wakulima imetupa furaha ya kujua msimu unaokuja hatutatupa maparachichi yetu na kuuza kwenye viroba, sasa basi soko liko tayari na ndugu zetu watasimamia ambao wamepewa dhamana kuhakikisha mwaka ujao basi hatutakuwa na kilio tena cha kuozesha parachichi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza pia Wizara, Mheshimiwa Waziri Mkuu nimesoma katika bajeti yako umeelezea kwamba kuna magari zaidi ya 40 yananunuliwa, pikipiki 555. Basi tuombe, mimi ninaamini nchi nzima inaenda kupata keki hii lakini mwisho wa siku tusisahau baadhi ya Majimbo ambayo kwa kweli tumepata, lakini tunafikiri yaongezewe kwa sababu tunafahamu Mkoa wa Mbeya ni katika zile big five ambayo inalisha Taifa hili, basi katika mgawanyo tuhakikishe watu wa Mbeya hususan Jimbo la Rungwe wanapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmesema mnajenga nyumba, tujengewe basi hata sisi kajumba kamoja msitusahau kwa Maafisa Ugani. Tunafahamu kabisa zao la parachichi lilianzia Rungwe japokuwa ndugu zetu wa Njombe wamefanya kwa uzuri zaidi basi msitusahau sisi mkahakikisha katika mgawanyo huu ikiwemo visima tunapata katika Jimbo letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu akisimamia mazao kwenye korosho amefanya vizuri, kwenye ufuta amefanya vizuri, kwenye chai nimelalamika wakati ule mwaka 2016 chai ya Rungwe ilikuwa shilingi 132 kwa kilo, leo imefika kwenye mia tatu na basi Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba bei ya chai uhalali wake unafahamu angalau iwe 700 kwa kilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu mkulima anatumia gharama kubwa sana na dola imepanda, kwa hiyo ni lazima tuweke bei iwe juu ili wakulima wetu wafanikiwe. Ninafahamu mmeanzisha soko la chai, hiyo ni juhudi kubwa ambayo mmefanya lakini bado tunahitaji jitihada za zaidi kwa wale wawekezaji ambao wamewekeza Mheshimiwa Waziri Mkuu tuweze kuhakikisha wanawasaidia watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunae mwekezaji ambaye ameacha kuvuna chai “Mo”. Tunatambua kabisa kwamba wawekezaji wanahitaji kupewa mazingira mazuri, lakini wawekezaji hawa hawawezi kuacha kununua chai bila kuwa na taarifa kwa wakulima. Tunafahamu zaidi ya wafanyakazi 300 hawana ajira sasa, nakumbuka tarehe 30 mwezi wa tano mwaka jana Mheshimiwa Bashe alimwambia mwekezaji tunaomba uvute muda ili tuweze kujipanga kama wananchi, kama Taifa tuone tunawasaidiaje watu hawa, lakini mwekezaji alifunga pamoja na kwamba anaweza akawa na haki, tunaomba Sheria za Wawekezaji ziangaliwe upya tuwe tuna win win situations, mwekezaji hawezi kuacha ghafla, chai imekuwa mashamba makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alipita kiongozi wa CCM katika Wilaya yetu wananchi walilalamika, leo hii mashamba ya chai yametupwa hayana nafasi, basi yale mashamba kama ni hivyo mtupatie tuwagawie vijana waweze kulima, vijana waweze kujenga, maana maeneo yale sasa yamekuwa mapori hayasaidii lolote. Pamoja na hayo hawa wananchi ambao wameachishwa kazi, wapate haki yao ikiwa ni pamoja na NSSF ninaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu uaichukue hili na kulifanyia kazi. (Makofi)

Tunafahamu kabisa kwamba, mazao mengine ya ndizi ni ya msingi kabisa. Kuna nchi kama Jamaica wananunua silaha kwa ndizi. Sisi tunaamini ndizi ni zao zuri, kama likisimamiwa vizuri. Viwanda vidogovidogo vijengwe kwenye maeneo yetu, wawekezaji waje waangalie, kuwekeza na kuongeza thamani ya mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndizi ni zao ambalo linatoka kwa wingi sana katika Jimbo la Rungwe na katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Tunaomba Serikali, kwa Bajeti inayokuja, basi muhakikishe viwanda vingi vinaletwa na kuweza kuongeza thamani katika mazao ambayo tunayasimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ardhi; ninatambua kabisa ardhi ina migogoro ya muda mrefu na jitihada mbalimbali zimefanyika. Kuna wawekezaji ambao wanachukua maeneo makubwa, hawayafanyii kazi na wanaondoa wananchi bila utaratibu. Tunaomba muweze kuyasimamia ili wananchi hawa wapate haki katika nchi yao ambayo wamezaliwa, maana hawana sehemu nyingine ya kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, kwa mara ya kwanza ninaunga mkono bajeti hii kwa sababu, ninajua kuna mbolea ya parachichi inakuja, ninafahamu kuna visima vya parachichi vitachimbwa. Basi, kwa maana hiyo sina sababu ya kuipinga, ninaiunga mkono hoja ya bajeti hii. Ahsante sana. (Makofi)