Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo wa kusimama humu kwenye Bunge lako Tukufu na kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninapenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake aliyoitoa. Kwa kweli, ni nzuri sana, ambayo inaonesha utendaji na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kusimamia hili pamoja na Mawaziri ambao wapo chini ya sekta yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya moyo wangu namshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa muda wa miaka minne hii, kwa kweli ameonesha kazi ya umahiri. Ni mwanamke shupavu, ni Rais wetu ambaye tunampenda sana, anatuonesha mambo mengi aliyoyafanya kwenye Awamu ya Sita. Kweli tunamshukuru na tunampogeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa mkazi wa Morogoro, siachi kuongelea reli ya kati ambayo imejengwa kwa kiwango kikubwa cha kimataifa. Wananchi wa Morogoro na Tanzania tunamshukuru sana kwa sababu, reli hii ya mwendokasi tayari imejengwa kuanzia Dare es Salaam kuja mpaka Morogoro, tunakwenda bila ya matatizo kuja mpaka Dodoma, tunafurahia sana usafiri. Wabunge na wananchi wengi tunatumia usafiri huu wa reli ya kati ambayo ni mwendokasi, ni nzuri sana. Ukikaa humo unatulia na unaweza hata kusinzia, kwa kweli unafika kwa wakati, kwa muda mfupi, ukilinganisha na usafiri wa basi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, reli hii imeleta ajira kwa vija wetu tunawaona wasichana kwa wavulana, tunashukuru sana. Reli hii ni ya kimataifa ambayo kwa kweli ni ya kiutalii, ni nzuri sana. Jambo muhimu sana kwa reli hii ninaomba sana wananchi, wasafiri pamoja na wafanyakazi waendelee kuitunza. Sehemu hizi ambazo zimebaki za Makutopora – Tabora – Mwanza – Kigoma ziweze kwenda kwa wakati, ili tuweze kuserereka bila ya kuchelewa. Rais kweli tunaye na tunasema kuwa tunatamba naye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ninaweza kuongelea ni Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere. Tunamshukuru sana Rais wetu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Biteko na Naibu wake. Kwa kweli, tunafurahi sana kuona umeme tayari umewaka, bwawa limekamilika. Hili bwawa halipo popote, tunasema kuwa, sana sana lipo Mkoa wa Morogoro kwa hiyo, tunashukuru sana pamoja na Mikoa ya Lindi, Pwani na Tanzania nzima.


Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme megawati 2,115 ambazo zimeongezwa kwenye gridi na kufikia megawati 4,000 sio chache. Kwa hiyo, tunashukuru, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kusimamia, kumalizia na kulikamilisha hili Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo wazo la kulijenga lilianza enzi za Baba wa Taifa. Kwa hiyo, tunampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la muhimu ni tuweze kusambaza huu umeme uweze kwenda kwenye vitongoji na vijiji kadiri Serikali ilivyopanga, ili kusudi wananchi wote wafurahie umeme huu. Kwa kweli, tunashukuru kwa umeme huu ambao tumepewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kuongelea ni maji. Ninamshukuru sana Mheshimiwa ametenga fedha tumepata maji na miradi ya maji inaendelea. Tunashukuru sana wananchi wengi wanapata maji. Wananchi 76.6% ni ambao wanapata maji vijijini na mijini ni 90%. Kwa kweli, tunashukuru kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ambao bado hawajapata maji, ninaamini Mheshimiwa Waziri, Aweso, pamoja na Naibu wake hawalali, wanafanya kazi kweli. Kwa hiyo, tunaomba maji yaweze kuwafikia watu wote kwa wakati, lakini tunashukuru kwa hiki tulichopata, unaendelea vizuri, maji tunayo. Kwa mkoa wangu wa Morogoro tuna maji, lakini kwa ile miradi ambayo bado haijakamilika tunaomba ikamilike kwa wakati, ili watu wote waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninaloongelea ni kuhusu barabara, kwa kweli tunajivunia mtandao wa barabara wa lami. Sasa hivi ninaweza nikatoka Dar es Salaam nikaenda mwisho wa nchi yetu. Mwisho wa nchi siyo kwingine ni Mkoa wa Kagera, Ruvuma na hata Tanga, kwa gari bila ya kuwa na tatizo. Hata saloon inakwenda kwa sababu mtandao wa lami umeenea. Kwa hiyo, tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa barabara hizi za TARURA ambazo bado ninaamini fedha zitategwa kwenye bajeti hii tunashukuru sana kuwa, tumepata mtandao mzuri na zenyewe zitajengwa. Ninaamini hata barabara nyingine ambazo bado hazijakamilika, kama asubuhi tuliuliza swali la Barabara ya Ifakara kwenda mpaka Namtumbo, tumejibiwa majibu mazuri; fedha zinatengwa kwa hiyo, hii barabara itajengwa. Mheshimiwa Rais tunamshukuru kwa mambo mengi anayofanya, kwa kweli Watanzania tunajivunia kuwa na yeye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bwawa la Kidunda limekuwa la muda mrefu, lakini ninashukuru limewekewa jiwe la msingi. Mheshimiwa Waziri Mkuu tulikuwa pamoja kule Morogoro, aliweka jiwe la msingi. Kwa hiyo, tunamshukuru na tunajivunia sana kuwa na yeye. Tunajivunia sana Rais wetu, mambo mazuri yanakwenda na Bwawa la Kidunda litakamilika watu wa Dar es Salaam na Pwani watapata maji ya kutosha hata Morogoro, vijiji vinavyozunguka Bwawa la Kidunda vitaweza kupata maji ya kutosha na umeme. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hili kwa sababu, katupatia Mama Samia kuwa Rais wetu. Ahsante Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni vituo vya afya. Ukweli, nani ambaye haoni kuwa Mheshimiwa Rais amejenga vituo vya afya vingi, kila jimbo na mkoa tuna vituo vya afya. Tunajivunia sana kuwa na vituo vya afya, sasa hivi madaktari wataletwa na pale ambapo hawatoshi watawekwa, ikiwa ni pamoja na dawa zitakuwepo. Kwa kweli, tunashukuru, mambo ni mazuri, ila maboma ambayo bado hayajakamilika tunaomba yakamilike kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninashukuru, nina furaha sana pale ninapoongea kuwa, Mama Samia amefanya mambo mazuri. Kweli tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia Rais wetu. Ahsanteni sana na Mwenyezi Mungu ambariki. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)