Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia Hotuba ya Waziri Mkuu. Nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo kwa kweli, ameionesha kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na mwenzangu kusema kwamba, wakati anaachiwa nchi miradi mikubwa iliyokuwa imeanzishwa kama asingekuwa shupavu, miradi hii, isingeendelea na isingekamilika. Kwa kweli, sisi tunajivunia uwepo wake na utendaji kazi mzuri ambao kwa kweli, Watanzania tulikuwa tunahitaji Rais wa namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo wenzangu wamezungumza, uchumi unakuzwa na miundombinu. Miundombinu ya reli, kwa sasa watu ambao tunasafiri kutoka Dodoma – Dare es Salaam kwa kweli, wameturahisishia sana kwa gharama ndogo na pia, muda mfupi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara pia zimeendelea kufunguka na madaraja yameendelea kujengwa. Ama kweli, lile ambalo limesemwa kwenye Biblia kwamba, watu walivuka baharini kwa Fimbo ya Mussa, ndilo ambalo tunakwenda kuliona Usagara – Busisi kwenda Sengerema ambavyo daraja linaendelea kukamilishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri Mkuu, ndiye Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Amekuwa nasi hapa akitusikiliza, lakini amekuwa kioo kwa Mawaziri wengine. Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa mtendaji mzuri sana wa Serikali kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuyazungumza haya kwa sababu, tarehe 21 ukiondoa mengine, mwezi Desemba alikuwa kwangu Magu. Alipoingia tukaanzia pale Kisesa, Bujora, ambapo kulikuwa na tenki kubwa la maji, likikamilika litasaidia Miji ya Bujora na Kisesa. Mvua ilianza kunyesha, Waziri Mkuu hakusita akaanza kuongea na wananchi mvua inanyesha. Huyu ni Waziri Mkuu wa aina tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu ni Waziri Mkuu wa aina tofauti, tumeona Mawaziri Wakuu, lakini huyu ni wa tofauti. Tunaomba Mwenyezi Mungu aendelee kutusimamia na kumpatia moyo huo huo wa kuwajali wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipotoka pale tulikwenda Shule ya Wasichana ya Kimkoa na tulipotoka pale tulienda Nghaya. Tulipofika Nghaya kwenye daraja ambalo Rais ametupatia shilingi bilioni 9.3, maana yake ni kwamba wale tunaobeba fedha kwenye mabegi ni mabegi 93 yamewekwa pale Nghaya. Mvua ilimwagika, Waziri Mkuu hakusita, akatoka mbele ya turubai akasimama kwa wananchi akaanza kuwahutubia wananchi mvua inanyesha mpaka mwisho wa hotuba yake. Tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri kwa kweli, yeye anamsaidia Mheshimiwa Rais kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakusita, tukaondoka hapo tukaenda kwenye Daraja la Simiyu ambalo Mheshimiwa Rais ametupatia shilingi bilioni 148 na linaendelea kujengwa. Sisi tunaobeba mabegi shilingi milioni 100 ni sawa na mabegi 480; haijawahi kutokea fedha hizo kuletwa Magu, kwa kweli tunakupongeza Mheshimiwa Rais kwa kutupatia fedha nyingi kiasi hicho. Pia, tunampongeza Waziri Mkuu alitembea mvua ikiwa inanyesha, akiwa unawahutubia wananchi maelfu kwa maelfu. Aendelee kuwa na moyo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapompongeza Mheshimiwa Rais na pia, tunaendelea kusema mapungufu ambayo kwa kweli, sasa hivi tunahitaji fedha, kwa ajili ya kumalizia. Mradi wa Maji wa Lugeye ambao upo 65%, Mradi wa Iseni, Nyanghanga, Mradi wa Mwamabanza, Mwarina-Salonghwe ambao upo 85% ni fedha kidogo tu za kumalizia hii miradi wananchi waweze kupata huduma. Tunaamini mipango ya Serikali muda si mrefu itatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapompongeza Mheshimiwa Rais kwa kuleta fedha nyingi za elimu, madarasa mengi yamejengwa. Tunaendelea kukupongeza Waziri Mkuu kwa usimamizi wako madhubuti ambao kwa kweli, umeendelea kujionesha kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niendelee kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita. Tulikuwa na jengo ambalo limeanza mwaka 2012, limekaa kwa muda mrefu, lakini sasa hivi ninafurahi kusema kwamba, Halmashauri yangu ya Magu imehamia mwaka huu kwenye jengo jipya ambalo Mheshimiwa Rais ameendelea kutupatia fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapompongeza Mheshimiwa Rais tunaendelea pia, kupongeza jitihada, hasa kwenye vituo vya afya ambavyo tumepewa na vifaatiba vinavyojitosheleza. Wananchi sasa hivi wanapata matibabtu ya kutosha huko kwenye vituo vya afya kuliko hata kwenda kwenye Hospitali zetu za Wilaya. Tunaomba tuendelee na Serikali iendelee kuweka fedha, hasa kwenye vituo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina Kituo cha Afya pale Nghaya, kimebakiza shilingi milioni 250 kukamilika; ni pale ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu alisimama, mvua inanyesha. Pale Busaranga kituo kile kinapelea shilingi milioni 250 tu kiweze kukamilika kwa hiyo, tunahitaji Serikali inapopata fedha iweze kutupatia. Pia, hata kwenye kituo cha afya ambacho tulikuwa tumekipatia kipaumbele, kama ambavyo Serikali walielekeza kwamba, angalau kila jimbo liweze kuleta orodha ya kituo kimoja kimoja. Kituo cha Lutale nacho tunahitaji fedha, kwa ajili ya kukamilishwa ili kiweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita imefanya mambo mengi na tunaamini kwamba, mahitaji ya Watanzania yapo mengi. Tunapokwenda kwenye umeme, sasa tumekwenda vitongoji 15 ambavyo Serikali imetupatia, ninafurahi kusema kwamba, vitongoji 15 kwenye Jimbo la Magu mkandarasi yupo kazini na anaendelea vizuri. Sasa tunahitaji vitongoji vingine na hapa, tunaomba watuangalie sisi wenye majimbo makubwa. Serikai haiwezi kutufananisha na majimbo mengine madogo na ikatugawia labda vitongoji 50 kila mmoja, wengine tupo double, naomba waangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndipo ambapo ninataka nisisitizie kwamba, sisi tulio na majimbo makubwa watupatie angalau vitongoji vingi kwa sababu, mimi nina vitongoji 508, huwezi kufanisha na mtu mwenye vitongoji 206, kwa kweli waangalie hilo. Wizara ya Nishati iweze kupima ukubwa wa majimbo yetu, halafu iweze kutupatia vitongoji ambavyo vinafanana na majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapompongeza Mheshimiwa Rais, ninataka tu niseme kwamba, tumepiga hatua kubwa. Kama ambavyo wenzangu wamezungumza, Bajeti ya Barabara, TARURA ilikuwa ni shilingi milioni 830, leo nina shilingi bilioni 2.8. Maana yake ni kwamba, nimeongeza fedha ambazo tulikuwa hatuna kuanzia mwaka 2020. Hata hivyo, bado uhitaji wetu wa barabara ni mkubwa mno kwa sababu ya maeneo yenyewe husika, hasa kwenye Mji wa Kisesa na Bujora. Niombe hili kwamba, katika fedha za wafadhili zinazokuja kuboresha miji, Mji wa Kisesa na Bujora unatakiwa uwekwe sasa kwenye mpango wa kuboreshwa na fedha hizi za wadafhili, hasa World Bank, kwa ajili ya kuhudumia barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapompongeza Waziri Mkuu na Mawaziri wanaomsaidia. Kazi hii ya kumsaidia Mheshimiwa Rais ni kubwa. Alipoanza Waziri Mkuu kwamba, mazao matano ya kimkakati pamba, chai na mengine, ninataka nimhakikishie kwamba, ninampongeza sana Waziri wa Kilimo, ameanzisha utaratibu mzuri wa BBT hata wafanyabiashara wa uchambuaji wa pamba wakakubaliana kuwalipa vijana waliotoka vyuo vikuu, kwa ajili ya kusimamia kilimo. Mwaka huu tunayo matumaini makubwa kwamba zao la pamba litakwenda kuongezeka. Ni kazi ya Serikali sasa kuona mwenendo wa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya kazi kubwa sana ya kuhamasisha. Kwa hiyo, hapa Mawaziri wanamsaidia kikamilifu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante. Kengele ya pili.

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu umeisha?

MWENYEKITI: Umeisha. Kengele ya pili.

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi ninaunga mkono hoja, lakini namhakikishia kwamba, Wabunge tutaendelea kumwombea Waziri Mkuu, Mheshimiwa Rais aendelee kumwamini kwa sababu, anamsaidia kikamilifu. (Makofi/Kicheko)