Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Segerea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa ninachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya. Pia, ninampongeza kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa kuweza kukutana na wananchi wangu wa Kata ya Kipawa, kufanya nao vikao na hatimaye hao wananchi wakalipwa. Kwa hiyo, ninachukua nafasi hii kumpongeza kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Kipawa. Tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa aliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kutuona na kuweza kuanza kutulipa kwa kilio ambacho tulikuwa nacho kwa takribani miaka tisa; kwa kuweza kuwaona sasa wananchi wa Kipunguni. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuwaona wananchi wa Kipunguni ambao wamekaa kwa muda wa miaka 27 wakidai madai yao ya fidia ili waweze kupewa fidia kutokana na viwanja vyao ambavyo vilichukuliwa na Airport. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza vile vile Mheshimiwa Waziri Profesa Mbarawa. Kwa namna ya pekee ninampongeza sana sana Naibu Waziri Mheshimiwa David Kihenzile kwa kazi kubwa aliyoifanya, kwa kuja Kipunguni na kuongea na wale wananchi. Pia, ninampongeza Mkurugenzi wa Viwanja vya Airport, ambaye ni Ndugu Mambokaleo kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa wananchi wangu wa Kipunguni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, sasa ninaomba nitoe hotuba yangu. Kwanza nianzie kwa watu wa Kipunguni, kwamba wamelipwa, lakini waliolipwa si wote; wamelipwa nusu. Nimepata habari sasa hivi kwamba wale waliobaki wataanza kulipwa mwezi huu. Kwa hiyo, ninaendelea kushukuru na ninaendelea kuwaasa wananchi wa Kata ya Kipawa waendelee kuwa na uvumilivu, kwamba tulielewana malipo yatakuwa ni ya awamu. Wamelipwa awamu ya kwanza, lakini pia awamu ya pili inaenda kulipwa mwezi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, ninaomba niipongeze sana Serikali kwa Mradi wa DMDP. Kama mnavyojua, kwa kweli Mkoa wetu wa Dar es Salaam kila siku tumekuwa tunauongelea kutokana na mvua ambazo zinanyesha, lakini pia miundombinu ambayo haiko vizuri katika Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwa sasa Mradi wa DMDP umesainiwa. Tunachokiomba tu Serikali ni kwamba, hao watu ambao wamesaini au hawa wakandarasi ambao wameshasaini Miradi ya DMDP, sasa waanze kwa haraka. Kwa sababu huu mradi tumeusubiri kwa muda mrefu, lakini hatimaye umesainiwa. Ninampongeza sana Waziri wa TAMISEMI kwa kuweza kulikamilisha jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na issue ya Bonde la Mto Msimbazi. Pamoja na miundombinu ambayo tunaisema Mkoa wa Dar es Salaam, lakini pia katika majimbo yetu, takribani majimbo yote tuna Bonde la Mto Msimbazi, bonde ambalo limepita katika Jimbo la Segerea, limepita katika Jimbo la Ukonga, liko Ilala, liko Kinondoni na pia liko Kawe. Bonde hili la Mto Msimbazi ni muda mrefu sana tumekuwa tukiambiwa kwamba litaanza kujengwa. Kama unavyojua, juzi juzi hapa mvua imenyesha Dar es Salaam na watu bado wameendelea kupata mafuriko. Wananchi wengine wanajua kabisa kwamba bonde hili lilikuwa kwenye mkakati wa kuendelea kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka katika majibu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu atakavyokuja kuhitimisha, atuambie sasa Bonde hili la Mto Msimbazi limefikia wapi? Kwa sababu ndilo bonde ambalo linaendelea kutupa shida katika Mkoa wa Dar es Salaam. Kama nilivyosema, shida si katika jimbo moja, ni shida katika majimbo yote. Unaweza labda ukasema kwa sababu majimbo mengine yako mbali hayajaweza kufikiwa, lakini pia kuna mikondo ile ambayo imefika kwenye majimbo hayo. Kwa hiyo, ni mkoa mzima ambao unaathiriwa na Mto Msimbazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililotaka kuongea ni kuhusiana na issue ya miundombinu ya elimu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Katika Mkoa wa Dar es Salaam hususan jimbo langu kwa kweli madarasa mengi yameongezwa, shule nyingi za sekondari zimejengwa. Katika shule tisa ambazo zimejengwa katika hii miaka minne ya Mheshimiwa Rais, kwenye jimbo langu peke yake zimejengwa shule nne za ghorofa na shule moja ina madarasa 40. Kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba, katika jimbo langu kuna shule ambazo zitachukua watoto ambao walikuwa wanakwenda kusoma sehemu tofauti; kwa hiyo, watabaki pale pale katika Jimbo langu la Segerea, Wilaya ya Ilala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kupongeza sana, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais, pia ninampongeza Waziri wa TAMISEMI kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Ninapenda kuwaambia Wabunge wenzangu hapa kwamba, shule ambazo tumejenga katika Jimbo langu la Segerea ni shule ambazo ni za mfano kwa sababu kuna shule za ghorofa nne, lakini pia kuna shule tano ambazo ni shule za msambao. Kutokana na Jimbo langu la Segerea kuwa na sehemu ndogo ya ya kujenga tumeamua sasa tujenge madarasa au shule za ghorofa ili tusitumie nafasi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ninapenda pia kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa TAMISEMI kutokana na kazi kubwa ambayo ameifanya kwenye Sekta ya Afya. Katika Jimbo langu la Segerea kabla ya Mama Samia kuingia hatukuwa na kituo cha afya. Kwa sasa hivi tuna Kituo cha Afya Kata ya Kinyerezi, tuna Kituo cha Afya Kata ya Kiwalani na tuna Kituo cha Afya Kata ya Segerea. Bado tunaendelea kutafuta maeneo mengine ili kuweza kujenga vituo vya afya. Kwa hiyo, ninachukua nafasi hii kumpongeza sana sana sana Mheshimiwa kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ili kuwaletea huduma za karibu wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ninataka niongelee suala la 10% kwa vijana, akinamama, pamoja na walemavu. Tunashukuru kwamba kipindi kilichopita watu waliweza kufaidika sana kutokana na hii 10% mpaka iliposimamishwa. Sasa hivi imeanza kutolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii kuwaomba wananchi, kwa sababu kuna wananchi wengine bado hawajajua na hawajui kwamba hii 10% inatoka. Kwa hiyo, waende watengeneze vikundi ambavyo vinaweza kuwasaidia kwenda halmashauri na kufuata masharti. Pia, ni muhimu sana kuweza kurudisha hizi pesa ili na watu wengine waweze kukopa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)