Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ninapenda kuanza kuchangia mchango wangu katika eneo la Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC). TFNC ilianzishwa kama shirika la umma la kutoa huduma, kwa Sheria ya Bunge Na. 28 mwaka 1973.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uundwaji wa taasisi hii ilikuwa ni utekelezaji wa maono ya Baba wa Taifa, kwa maana ya kuhakikisha kwamba tunalinda Taifa letu vizazi kwa vizazi katika eneo la lishe pamoja na chakula. Eneo la lishe pia, ninapenda kumpongeza na kumtambua Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Lishe tangu akiwa Makamu wa Rais. Hivyo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendeleza utekelezaji wa maono ya Baba wa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusikitika, Disemba, 2023, Waziri wa Ofisi ya Rais, Mipango na Utekelezaji aliitangaza TFNC kama moja ya mashirika ambayo yanafutwa kwa sababu hayazalishi ilihali Shirika hili la TFNC lilianzishwa kwa sheria na kutambuliwa kwamba ni shirika la kutoa huduma. Hivyo, suala la uzalishaji wa mapato na fedha halimo kabisa katika msingi wa uanzishwaji wa Shirika hili la TFNC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi hiki cha hivi sasa tangu tangazo hili litoke, kumekuwa na sintofahamu kubwa kuhusiana na namna ambavyo masuala ya lishe yatakavyoratibiwa katika Taifa letu. Hatueleweki kama Tanzania. Wakati bado tuna uhitaji mkubwa na tuna changamoto nyingi za masuala ya lishe (utapiamlo) na aina zote nyingine, sisi tunaamua kwenda kufuta shirika kama la TFNC. Wakati umefika sasa tufikirie upya uamuzi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili, ninaomba nishauri mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, hivi karibuni Serikali iliamua kutokuendelea na uamuzi wake wa kufuta Shirika la Elimu Kibaha. Kwa msingi huo huo, kama Serikali iliweza kutambua kwamba kutaka kulifuta Shirika la Elimu Kibaha ilikuwa ni makosa na itakuwa na madhara makubwa, basi kwa msingi huo huo ninaiomba sana Serikali ipitie upya na ifute ule uamuzi wa kufuta shirika hili la Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, kwa sababu bado lina umuhimu mkubwa na tuna uhitaji nalo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili katika eneo hili, Serikali ifanye marekebisho kwenye Sheria ya Chakula na Lishe Sura ya 199, ili Taasisi ya Chakula na Lishe iwe chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambaye sasa hivi ndiye anayeratibu masuala ya lishe, kwa sababu masuala ya lishe ni masuala mtambuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zimeshaonyesha kuchangia kudhibiti na kupambana na masuala ya utapiamlo kwa upande wa Wizara ya Afya, inachangia 20% tu, 80% inachangiwa na sekta nyingine. Hivyo, ni muhimu sana Taasisi ya Chakula na Lishe kuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye pia ndiye anayeratibu Mpango Jumuishi wa Lishe (NMNAP). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia hapa kwa unyenyekevu mkubwa nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Mkuu ahadi aliyotoa tarehe 3 Oktoba, 2024, kwenye mkutano Mwanza kuhusiana na suala hili la kurejesha TFNC na ahadi hii Mheshimiwa Waziri Mkuu aliitoa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee wetu Mheshimiwa Mizengo Pinda. Kwa hiyo, ninaamini kupitia hotuba hii ya bajeti tutapata kusikia kauli ya Serikali kuhusiana na nini Serikali inakwenda kufanya katika kuiokoa na kuirejesha Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), kwa sababu bado tuna uhitaji nayo mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu la pili ni usalama wa chakula (food safety). Hali ya sasa ya vyakula vinavyouzwa sokoni, na hivi ni vyakula vinavyotoka ndani na nje ya nchi, hairidhishi, kwa maana ya upande wa usalama wa chakula, eneo la food safety. Mwaka 2019, kwa maono na mapenzi mema kabisa Serikali iliamua kufua TFDA na kuhamishia jukumu la udhibiti wa usalama wa chakula (food safety) kwenda TBS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuseme kwa uwazi kabisa, TBS imeshindwa kuratibu na kudhibiti masuala ya usalama wa chakula. Hatuwezi kuendelea kuendesha suala la usalama wa chakula kibiashara. Suala la usalama wa chakula ni suala ambalo linahusu uhai na afya za Watanzania. Hatuwezi kuendelea kuweka maisha ya Watanzania rehani kwa sababu tu ya kuangalia maslahi ya kibiashara. Kwa hiyo, wakati umefika sasa, kwa unyenyekevu mkubwa chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu tupate kauli ya Serikali. Maana katika Bunge hili tangu mwaka 2021 tumekuwa tukiomba Serikali irejeshe masuala ya udhibiti na usimamizi wa usalama wa chakula (food safety) Wizara ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata ahadi mbalimbali hapa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imeshajadili, Serikali imeona lina tija, suala hili liko kwenye uamuzi wa mwisho. Ninaomba sana tupate kauli ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Je, ni lini sasa suala la udhibiti wa usalama wa chakula (food safety) litarejea Wizara ya Afya ili tuache kuendelea kuweka maisha ya Watanzania rehani kwa sababu tu ya maslahi ya kibiashara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ni pana kwa sababu, katika makubaliano ya Kikanda na Kimataifa ili uweze kuuza vyakula vyako nje ya nchi, suala la usalama wa chakula ni muhimu. Sasa hivi Tanzania kuna maeneo ambayo tunapata changamoto kuuza mazao yetu nje ya nchi kutokana na kwamba tunashindwa kukidhi vigezo vya usalama wa chakula, kwa maana ya chemical residue pamoja na masuala mengine yanayoendana na hayo. Kwa hiyo, suala hili la usalama wa chakula si suala la kuendelea kulichukulia kwa wepesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niiambie Serikali jambo moja, kama haifahamu. Sasa hivi ukienda pale TBS wale wataalam wetu wa food safety sasa hivi hata vyeo vyao vya food safety havipo tena. Sasa hivi wote wanatambuliwa kama Quality Assurance Officers. Wataalamu wetu wa food safety sasa hivi wanafanya kazi ya kupima ubora wa nondo. Haikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haikubaliki katika Taifa ambalo tumeona ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza. Tumeona ongezeko kubwa la magonjwa ya cancer; tumeona namna gani ambavyo Mfuko wetu wa Bima ya Taifa ambavyo umeelemewa, ambapo zaidi ya 70% ya magonjwa yanayotibiwa pale ni magonjwa yasiyoambukiza. Magonjwa haya ni magonjwa ambayo yanaepukika. Yanaepukika kwa kuhakikisha tuna mfumo ulio thabiti wa kulinda suala la usalama wa chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo, suala la usalama wa chakula haliwezi kuendelea kuwa chini ya TBS. Tumesema sana ndani ya Bunge hili, nalo tumepata ahadi nyingi sana ndani ya Bunge hili. Sasa, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa unyenyekevu na kwa uchungu mkubwa wa maisha ya Watanzania, tufike mwisho kwenye jambo hili. Tusiendelee kurudisha nyuma jitihada za Serikali. Serikali inafanya uwekezaji mkubwa sana kwenye maeneo mengi, halafu tunatumia fedha nyingi sana kutubu magonjwa ambayo yanaepukika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanya jitihada kubwa sana kuweka wawekezaji kwenye maeneo mengi yenye tija, halafu tunarudisha na kufifisha jitihada hizo kwa kupunguza ubora wa nguvu kazi yetu. Jambo hili halikubaliki na sasa wakati umefika lifike tamati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kwa kuzingatia masuala ya chakula, lishe na usalama wa chakula ni masuala ambayo yanashabihiana. Ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa sana niishauri Serikali ifikirie namna ya kuunda chombo kipya chenye hadhi na mamlaka zaidi ya kuratibu, ya kuongoza, ya kusimamia, ya kudhibiti na kushauri katika eneo hili la chakula, lishe na usalama wa chakula (food safety), kupitia Sheria ya Executive Agencies Act, CAP. 245. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninashukuru sana. Ninaamini chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu Kassim Majaliwa na namna ambavyo yeye mwenyewe ni Kinara wa Lishe, ni Kinara wa Usalama wa Chakula, tutapata ufumbuzi na kauli thabiti ya Serikali ni lini TFNC inarejeshwa na ni lini masuala ya usalama wa chakula (food safety) yataondolewa TBS na kurejeshwa Wizara ya Afya. Ahsante. (Makofi)