Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Joseph Michael Mkundi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kunijaalia uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina kila sababu ya kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana anayoifanya na kuwatendea wananchi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ukerewe kama sehemu ya Taifa hili, tangu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameingia madarakani limefaidika kwa miradi mingi sana ya maendeleo. Karibu kila sekta wananchi wa Ukerewe wamenufaika na uongozi wake; Sekta za Afya, Elimu, Nishati, Miundombinu na nyinginezo. Kwa hiyo, ninampongeza sana na kumshukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake; hotuba nzuri ambayo pia inaakisi utendaji wake mzuri. Sina mashaka na yale yaliyoko kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema, mambo mengi sana yamefanyika kwenye maeneo yetu. Ukerewe ikiwa sehemu ya Taifa hili kama nilivyosema, imenufaika kwenye maeneo mengi. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninampongeza kwa namna ambavyo Serikali imetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani yetu ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 – 2025, Ibara ya 9(f) inaelezea dhamira ya Serikali kutengeneza ajira 8,000,000. Kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu mpaka sasa ajira milioni 8.08 zimetengenezwa. Kwa hiyo, ninapongeza sana kwa utekelezaji wa Ilani yetu ya Uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mpango wa Maendeleo wa Mwaka wa Fedha 2025/2026, moja ya misingi ambayo itatupelekea kwenye mafanikio ya kuongeza ya ajira hizi ni ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za uwekezaji na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Ni kwamba sekta binafsi ina mchango mkubwa sana kwenye utengenezaji wa ajira hizi, ndiyo maana utaona katika ajira milioni 8.08 zilizotengenezwa mpaka sasa ni milioni 1.04 tu ambazo ni sekta iliyo rasmi na karibu milioni 7.04 ni sekta isiyo rasmi. Hii inaonesha namna mchango wa sekta binafsi ulivyo muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta binafsi inaweza ikaingia kwenye uchumi, kutengeneza hizi ajira kama miundombinu na mazingira wezeshi yatakuwepo, lakini kama kutakuwa na kikwazo itakuwa ni changamoto kubwa. Kwa maana hiyo, ule uchumi jumuishi au kwa Kikerewe tunavyoita inclusive economy itakuwa ngumu kidogo. Sasa kwenye eneo hili niombe ili wananchi wa Ukerewe waweze kuwepo na wajumuike kwenye huu uchumi jumuishi kuna baadhi ya maendeleo ninaomba Serikali iyafanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, miradi iliyokuwa imeanzishwa na haijakamilika basi iweze kukamilishwa; baadhi ya miradi ya maji, Serikali ifanye kila linalowezekana ili iweze kukamilika. Vilevile, miradi ya barabara ni muhimu sana, kwa mfano, Barabara ya kutoka Bunda kuja Nansio ambayo mkandarasi aliingia site pale akavuruga barabara ile ili aanze kuitengeneza lakini kwa sababu ya kutolipwa pesa yake ameondoka site inaathiri sana uchumi wa wananchi wa Ukerewe. Kwa hiyo, niombe kwa msisitizo mkubwa, Wizara ya Ujenzi, Mheshimiwa Waziri Mkuu, tusaidie barabara hii iweze kukamilishwa ili wananchi waweze kushiriki kwenye uchumi jumuishi, lakini na kutengeneza ajira kupitia sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatamani kushauri kwenye maeneo mengine mawili, kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kupandisha utalii wetu kupitia The Royal Tour Film pamoja na Amazing Tanzania ambayo imepelekea idadi ya watalii kuongezeka kutoka milioni 1.048 mpaka kufikia idadi ya watalii milioni 1.1 karibu tisa, ni jambo jema sana. Bahati njema sana tuna fursa kubwa ya kuongeza idadi ya watalii. Kwa mfano sasa tunaelekea kwenye michezo ya AFCON ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji mwaka 2027, lakini kinachonitia mashaka na ambacho ningependa kushauri, sioni kama tunaweka nguvu kubwa sana kwenye matangazo ili kuweka awareness ya kidunia, watu wajue kwamba mwaka mmoja au miaka miwili ijayo kuna tukio kubwa litakuwepo Tanzania na watu wajiandae kuja kushiriki, kuhudhuria kwenye michezo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, badala yake kwa sababu tunaandaa na nchi nyingine tukishirikiana, wenzetu wataanza kuwa bora kwenye matangazo na kwa hiyo watalii wataingia kwenye nchi zile sisi tutakuwa wanufaika watatu au wa pili kupitia fursa ya michezo hii ya AFCON. Kwa hiyo, ninashauri kuanzia sasa Serikali ione umuhimu wa kuweka nguvu kubwa kwenye kutangaza michezo hii ili dunia ijue kwamba mwaka mmoja ujao au miaka miwili ijayo katika nchi ya Tanzania kuna tukio fulani litakuwepo itangaze vivutio vyetu vya utalii iweze kuwa sehemu ambayo fursa hii ya utalii tukaitumia vizuri kupitia michezo hii ya AFCON.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la tatu ambalo ningependa kushauri kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, niipongeze Serikali imeonesha kukua kwa diplomasia ya uchumi. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kama mwanadiplomasia namba moja. Changamoto iliyopo na ambayo ninaiona ni kweli kwamba kama Taifa tumefanya kazi kubwa sana kupandisha diplomasia ya kiuchumi, tumeshiriki mikutano mingi sana ya nje, viongozi wetu wakuu wameshiriki sana mikutano mingi ya nje na shughuli mbalimbali za kiuchumi za kimataifa tumeshiriki; na sisi kama Taifa hapa nchini tumeandaa mikutano na shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo watu wengi wamekuja wakahudhuria lakini kuna shida moja ambayo tunaiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa la elimu kwa wananchi wetu. Wananchi wetu hawana elimu ya kutosha kuweza kujua hii diplomasia ya uchumi ni nini na fursa zinazojitokeza ni namna gani wananchi wa Taifa hili waweze kutumia zile fursa ili waweze kufaidika na fursa zilizopo kupitia diplomasia ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu ya mambo ya nje inafanya kazi kubwa sana kuunganisha na kutafuta fursa mbalimbali kwenye mataifa mbalimbali nje ya nchi, lakini namna gani sasa sisi kama jamii tuna grab zile fursa ili tuweze kuzitumia. Kwa hiyo, ningeshauri moja ili kuongeza awareness lazima tuwe na programs maalum kwa ajili ya kuelimisha kupitia idara, Wizara na maeneo mbalimbali. Kwenye ofisi zetu wanakuja watu wa nje kwa mfano wanakuja kuleta fursa, lakini wanapoingia kwenye ofisi kwa mfano za halmashauri zetu au kwenye idara mbalimbali inachukua muda mrefu kuhudumiwa jambo ambalo linachelewesha matumizi ya fursa zile ambazo Wizara ya Mambo ya Nje au taasisi nyingine yoyote imezifanyia kazi kuzileta nchini. Kwa hiyo, ni muhimu sana tukawekeza kwenye ku-create awareness kwa wananchi wetu ili wajue hii diplomasia ya uchumi ni nini na namna gani sasa tunaweza tukaitumia kwa ajili ya kutengeneza ajira, lakini na kuimarisha uchumi wetu kama Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwenye eneo hilo hilo, kwenye diplomasia ya uchumi ninahisi kunakosekana chombo maalum kwa ajili ya kuratibu ili fursa hizi zinapotengenezwa na Wizara ya Mambo ya Nje basi namna gani Wizara nyingine au idara nyingine zinashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ili kufanya fursa hizi ziweze kuonekana na kuweza kutumika. Kwa hiyo, Serikali ifanyie kazi mambo haya ili tuweze kutengeneza uchumi kupitia diplomasia hii ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa nafasi. (Makofi)