Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii na nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa chama changu (Chama Cha Mapinduzi), kwa jinsi anavyoipeperusha bendera yetu vizuri na kufanya takwa la kikatiba ambalo mwaka huu linategemewa kufanyika. Ninaamini chama changu kitaenda kushinda kwa kura nyingi sana kutokana na kazi nyingi zinazofanywa na watu wanaomsaidia Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa jinsi alivyowasilisha hotuba yake yenye kurasa nyingi zaidi ya kurasa 110 ambazo kwa hakika zimesheheni mambo ya msingi na yenye tija kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ofisi ya Waziri Mkuu inazo taasisi nyingi na za muhimu ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo mwaka huu inaenda kusimamia Uchaguzi Mkuu, ambalo ni takwa la kikatiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, Tume hii Huru ambayo imebadilika kutoka Tume ya Uchaguzi sasa na kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaye Msajili pia wa Vyama vya Siasa, lakini na taasisi nyingi ambazo zipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambazo kwa hakika ufanisi wake unaifanya Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufanya kazi ambazo zimetukuka sana katika kipindi hiki cha miaka minne. Ninaomba nichukue nafasi hii kupongeza kazi ambazo zimefanyika katika sekta zote hususan Sekta ya Elimu, Sekta ya Afya, Sekta ya Maji, Sekta ya Nishati na Sekta ya Mawasiliano katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi ambalo siyo muda mrefu sasa litaenda kuitwa Jimbo la Itigi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki cha miaka minne Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na mimi Mbunge wake na Madiwani wetu katika Halmashauri yetu ya Itigi tumeletewa pesa nyingi sana na Serikali na kujenga shule nyingi ya msingi na sekondari. Sasa, mfano mdogo, kuna kijiji kilikuwa na shule moja sasa kina shule nne, kingine kina shule tano, kingine hadi shule saba, kutoka shule moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni namna ambayo Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia inavyofanya kazi kwa weledi mkubwa sana hasa katika kuhakikisha watoto wa wakulima na wafugaji ambao walikuwa scattered wamekaa kufuata mazingira bora ya kilimo katika eneo langu sasa wamepelekewa shule. Kwa hiyo, watoto wale ambao kaka zao na dada zao walikosa fursa ya elimu leo wanaenda kusoma pasipo na shida japo kutakuwa na changamoto kadha wa kadha pengine walimu hawatatosha lakini tumeanza na majengo, maana yake kitakachofuata ni hayo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ukurasa wa 58 imezungumzia sana juu ya suala zima la elimu katika nchi hii lakini suala la afya katika ukurasa wa 62; lakini suala la maji katika ukurasa wa 61, kwa hakika ninataka niseme pia Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu huyu anaitendea haki nafasi yake na anatutendea haki sisi Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa naye humu katika Bunge hili na yeye kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali katika nyumba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazuri haya ninatamani kuishauri Serikali yangu baadhi ya maeneo ambayo yanapaswa kwenda kufanyiwa kazi. Mkoa wa Singida hadi tunavyozungumza hivi haujaunganishwa na Mikoa ya Mbeya na Simiyu kwa njia ya Barabara. Mkandarasi yupo site lakini bado anasuasua, kama zipo changamoto ambazo wanaziona hawajaenda naye sawa ninaomba Serikali ikae naye mezani amalizie kipande hiki ambacho anaendelea nacho ili wananchi wa jimbo hili na wananchi wa Mkoa wa Mbeya na wa Mkoa wa Singida, lakini kuunganishwa na Mkoa wa Simiyu kupitia Daraja la Sibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mtu akitoka nchi Jirani ya Kenya akipita Mkoa wa Mara akaja Simiyu kama anakwenda Mbeya hatakiwi kupita Morogoro, hatakiwi kupita Dodoma, anatakiwa apitie Itigi kama barabara ni ya lami anakutana na Mkoa wa Mbeya, anaingia boarder nyingine ya Zambia. Kwa hiyo, Mkoa wetu wa Singida umepakana na mikoa miwili, Mkoa wa Mbeya ambao ni mkoa wa mpakani, Mkoa wa Simiyu unaenda kupakana na Mkoa wa Mara ambao nao ni mpakani. Kwa hiyo, maana yake fursa ya kufungua Mkoa wa Singida kwa barabara unatengeneza uchumi wa nchi hii, unamsaidia mwananchi wa Tanzania na wa nchi jirani ambaye anakusudia kufanya biashara na nchi nyingine jirani kutoka ukanda mmoja kwenda ukanda mwingine. Vilevile ni corridor muhimu sana ya katikati kiuchumi tukiacha hii ya kupita Babati, Dodoma, Iringa lakini corridor nyingine ni ile pale mtu anatoka Moshi anakuja Arusha, Manyara, Singida tayari ameshafika Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu wa zaidi ya kilometa 150 mtu anayepita anayetoka Moshi kwenda Mbeya kupitia Babati, kupitia Dodoma na Iringa na yule atakayepitia Babati, Singida na kwenda Mbeya atapunguza zaidi ya kilometa 150 kama barabara hii itakuwa ya lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mengine hayo lakini kwenye Sekta ya Nishati, pia ninaomba niipongeze sana Serikali yangu, kwa kazi nzuri na kubwa zilizofanyika katika sekta hii. Vijiji vyangu vyote vimewashiwa umeme na sasa tunakwenda vitongojini. Ninaomba sasa nihimize Serikali mkandarasi wa Mkoa wa Singida hajapatikana, basi katika kipindi hiki kifupi tukiwa humu ndani tumwone mkandarasi wa Mkoa wa Singida naye amepatikana ili na sisi tu-enjoy fursa hii ambayo wenzetu wa mikoa mingine hapa wamekuwa wakitamba kwamba vitongoji vyao vinapelekewa umeme, sisi Mkoa wa Singida bado jambo hilo halijafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mawasiliano ya mitandao ya simu, mawasiliano ya redio, niipongeze sana Serikali kwa jitihada za kuweka na kutenga pesa nyingi, leo baadhi ya maeneo ya jimbo langu ambayo yalikuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano yanaenda kupatiwa huduma hii adhimu na mahsusi. Kama nilivyosema jimbo langu lipo sehemu kubwa linaelekea Mbeya maeneo ya Kintanula leo mkandarasi yupo site anajenga mnara kwa hakika ni jambo ambalo limesubiriwa kwa muda mrefu sana na nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa hilo, lakini bado usikivu wa Redio ya TBC haupo vizuri katika eneo zima la Halmashauri ya Itigi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walizindua mnara pale Manyoni tukitegemea kwamba Itigi napo utasikia, leo hausikiki kabisa. Ninaomba jitihada za makusudi za Serikali tunapoelekea katika uchaguzi, wananchi wetu wanapenda kusikiliza redio zao zaidi kuliko TV, maana yake kule vijijini nguvu ya wananchi kununua TV ni ndogo wanaweza kununua karedio kale kadogo na wakasikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)