Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kunipa fursa ya kuchangia bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na nianze na shukurani kwa kazi kubwa ambayo imefanyika ndani ya kipindi cha miaka mitano hususan katika Sekta za Mawasiliano, Ujenzi na Uchukuzi; nimechukua hizo sekta. Ninaishukuru Serikali kwa kazi kubwa ambayo imefanyika hasa Ziwa Victoria, ujenzi wa bandari na kuimarisha uchukuzi katika Ziwa Victoria lakini na Bahari Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali imekarabati Bandari ya Bukoba na imekarabati Bandari ndogo ya Kemondo ili kurahisisha uchukuzi katika ziwa na hii ni ku-complement kazi kubwa ambayo imefanya na Serikali ya kutujengea meli kubwa. Kama unavyojua meli kwa Kanda ya Ziwa, meli ni siasa na meli ni uchumi. Itasaidia akinamama ambao wanauza ndizi kutoka Bukoba kuzipeleka Mwanza na tutapata masoko na kufanya hivyo tutajenga uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri ambayo imefanyika ya kujenga hizo bandari tunaishukuru Serikali, tunajua meli kubwa sasa itatia nanga Kemondo na Bukoba kama ilivyokuwa miaka ya nyuma tulikuwa tumeikosa hii. Ninaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inaongozwa na Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha hili jambo, ni jambo kubwa amejenga historia na ametuheshimisha kusema kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Bandari ndogo za Kyaukwikwi na Bandari ndogo ya Katebe Magarini, ninashukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, alikuja Magarini alipotembelea Wilaya ya Muleba na alitoa maelekezo. Ninaomba sasa maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri Mkuu alipotembelea Wilaya ya Muleba alielekeza TPA kwenda kujenga gati mpya ya Katebe Magarini. Maelekezo hayo hayajatendewa kazi, lakini ninajua watakuja na ninaomba kuanzia sasa tunapoongea hapa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyoyatoa yakatekelezwe Magarini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hiyo tu na Bandari yetu ya Kyamkwikwi ambayo imechukuliwa na TPA ijengwe ili meli ndogo ambazo zilikuwa zinatoa huduma kabla ya kujenga meli kubwa sasa zikarahisishe usafiri na usafirishaji kupitia hizi Bandari ndogo za Kyamkwikwi na Katebe Magarini kwenda katika Visiwa vyetu vya Ikuza na Mazinga, Bumbile, Kerebe na Goziba ili ziwa lote sasa likapate usafiri wa haraka na usafiri wa bei nafuu; na tuweze kusafirisha mazao ya Ziwa letu la Victoria kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kwa ajili ya kupata masoko ya dagaa na samaki wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali yetu, kwani kwa kipindi kirefu Wilaya ya Muleba hatukuwahi kuwa na hospitali ya wilaya. Ni Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetutengea fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Wilaya ya Muleba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesaini mkataba, na mkandarasi yupo site. Naiomba Wizara ya Fedha ikamlipe advance payment ili mkandarasi yule asitoke site na tupate Hospitali ya Wilaya ya Muleba, watu wetu wa Muleba wakatumie na wenyewe wakafurahie hospitali ya wilaya ambayo tumeikosa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye zao la kahawa. Namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu, alikuja pale Kagera akatoa maelekezo na mwongozo ambao kusema kweli umewanufaisha na kuwafaidisha wakulima wa zao la kahawa Mkoa wa Kagera. Bei imepanda na wakulima wanafurahi na wanaishukuru Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto ndogo tunapoelekea msimu wa kahawa Kagera. Naiomba Serikali yangu sikivu, tunapokuja kwenye msimu wa kuvuna kahawa, tunapata changamoto ya watu wetu wanaovuna kahawa kutoka kwenye mashamba yao, wanakamatwa barabarani kwa kisingizio kwamba ni magendo. Hili jambo lilishatolewa kauli na Serikali. Hivyo basi, naomba katika bajeti hii Waziri wa Kilimo atoe maelekezo mahususi kuhusu masuala ya kahawa, wananchi wetu wanapotoka kuvuna kahawa kwenye mashamba yao wasibughudhiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya ndani kwa ndani nadhani siyo magendo. Biashara ya magendo ni pale ambapo tunavusha kahawa kutoka katika mipaka ya nchi yetu, huko tukashughulike nao; lakini ndani ya wilaya, ndani ya kata zetu, ndani ya tarafa zetu, naomba Bunge lako Tukufu likatoe kauli kabla wananchi hawajaanza kubughudhiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe shukrani tena kwa upande wa miundombinu Mkoa wa Kagera. Tunaishukuru sana Serikali, kwani imetupa fedha nyingi za kujenga miundombinu katika mkoa wetu na hususan Jimbo langu la Muleba Kusini. Barabara nyingi zimejengwa na zinapitika. Hata hivyo, bado nina kilio cha barabara yangu ya kutoka Muhutwe - Kamachumu - Buganguzi - Kishanda - Nshamba – Muleba ambayo ina urefu wa kilomita 56. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali, imejenga kilomita zaidi ya 49, zimebaki kilomita saba. Naiomba Serikali, kwa kuwa ilishatoa commitment ya kumaliza hiyo Barabara, tukamalizie hicho kipande cha kilomita saba ili wananchi wa Muleba wakafurahie kutumia barabara ya lami ambayo ni ya Muhutwe - Kishanda, Muhutwe – Kamachumu - Buganguzi - Kishanda - Nshamba – Muleba, kilomita saba tu zimebaki. Najua kwetu wanasema, ukishakula mbuzi usishindwe kula mkia wake. Naomba tukamalizie na mkia uliobaki ili barabara hii ikapitike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali yangu, tumepata kwani fedha nyingi na ya heshima, tunajenga daraja la Kamishango katika Mto Ngono. Hili daraja ambalo lilikuwa limeshindikana kwa miaka mingi, ni kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita tumepewa fedha za kutosha na mkandarasi yupo site. Wananchi wa Muleba wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inaongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutuonea hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wanasema kura za Mama tunapokwenda kwenye Uchaguzi Mkuu zipo salama na hazina shaka yoyote. Pale, kazi iliyofanyika kila mmoja anaiona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwenye kilimo na uvuvi. Mkoa wa Kagera hususan Wilaya ya Muleba, tunapakana na Ziwa Victoria. Uchumi wetu umefungamanishwa na Ziwa Victoria, lakini tunayo matatizo makubwa sana ya uvuvi haramu ambao unatishia ustawi wa mazalia ya samaki kwenye Ziwa Victoria. Nashukuru wakati Serikali inaongelea kupumzisha ziwa, na ninashukuru nimeongea na Waziri wa Mifugo na Uvuvi leo, Ziwa Victoria halimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tunaomba Serikali yetu sikivu tulishakuja na pendekezo hapa kuunda mamlaka ya uvuvi ambayo itasaidia kulinda mazingira ya Ziwa letu Victoria, kulinda mazalia ya Samaki, lakini kikubwa zaidi kupambana na uvuvi haramu. Hali ilivyo kwa sasa, hatuwezi tukalinda mazingira ya Ziwa Victoria tukapamba na uvuvi haramu kama hatuna chombo mahususi cha kupambana na hayo madhara ya uvuvi haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara husika tunapokwenda kumalizia hii bajeti, ituambie hiyo mamlaka tunaiunda lini? Kwa sababu tumeliongelea hili jambo miaka zaidi ya mitatu. Hili jambo lina faida kubwa sana kwa uchumi wa nchi yetu hasa kwa mazao ya samaki na dagaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Victoria pale tunayo changamoto kubwa, na nimemwelezea Mheshimiwa Waziri, kwenye Ziwa Victoria tulikuja na taa za solar ambazo wavuvi wengi wanalalamikia kwa sababu zina athari kwa mazalia ya Samaki, lakini zina athari hata kwa wananchi ambao wapo nje ya ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali hii ikafanye utafiti, iangalie ni madhara gani yanasababisha hizi taa za solar na ikachukue hatua haraka sana iwezekanavyo ili kunusuru mazalia ya samaki na kunusuru afya za watu wetu hasa wanaoishi ukingoni mwa Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hiyo hiyo ukiangalia umiliki wetu wa Ziwa Victoria, tunamiliki zaidi ya 51%, wenzetu Uganda 43%, nadhani, wenzetu Kenya asilimia sita; lakini ukiangalia faida tunayoipata, na hii nilishawahi kuichangia hapa Bungeni. Wenye asilimia ndogo wana viwanda vingi vya samaki kuliko sisi wenye asilimia kubwa. Hili jambo halikutokea tu kwa sababu ya miujiza au ya nini, inatokana na mfumo wetu wa tozo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naliomba Bunge letu Tukufu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wakaangalie tozo tunazotoza. Tunang’ang’ania vitu vidogo vya tozo tozo, lakini watu wanakimbia eneo letu kuwekeza viwanda, wanakwenda kuwekeza nchi jirani na tunapoteza ajira, tunapoteza kodi, tunapoteza mali kabisa, kwa sababu ya vitozo vidogo vidogo. Unang’ang’ania shilingi 20,000 unapoteza shilingi 1,000,000. Hii haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara, Serikali ikafanye tathmini (due diligence) wakaangalie kwa nini, viwanda vinakimbilia nchi za jirani? Ukiwa ziwani mle hakuna traffic, wala hakuna nini. Biashara zinafanyika humo ziwani kwa sababu sisi tozo zetu zipo juu, na nchi jirani zipo chini, wanakimbilia kule wanauza hata samaki kule. Badala ya kujenga viwanda hapa, sisi tutabaki tu na maji tunayaangalia, wenzetu wanatengeneza fedha huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi, na kwa kuwa hili jambo kwa kiwango fulani lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tukaliangalie, tukarekebishe tozo ili tuvutie viwanda wakawekeze kwetu, tukaajiri vijana wetu, na pia tukapate kodi kutokana na viwanda vitakavyojengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naishukuru Serikali yangu kwa minara mingi ya mawasiliano kwenye jimbo langu, sasa kuna usikivu wa simu. Nawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)