Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye hotuba hii muhimu kwenye bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nianze kwa kusema, nilikuwa nimejipanga kuchangia siku ya jana na Mheshimiwa Naibu Spika aliposema twende tukatafakari bajeti hii, akawa amenivuruga kidogo hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyofika nyumbani baada ya kusoma kwa kina hotuba hii yenye kurasa 103 ambazo Mheshimiwa Waziri Mkuu ametumia saa mbili kuisoma nilielewa kwa nini Mheshimiwa Naibu Spika alisema turudi nyumbani tukatafakari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwa makini hotuba hii, na kwa uzoefu mdogo nilionao wa kukaa ndani ya Bunge hili kwa miaka 10, nimejifunza jambo moja kubwa sana. Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na kwamba tunamsifia ndani ya Bunge hili, kuna kazi kubwa sana ambayo ni mtihani mkubwa, labda pengine wengi wetu tusingeweza kufaulu kama tungepewa ambao mama huyu alifaulu kuufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mataifa mengi yanapokuwa yamemaliza uchaguzi, au yanapobadilisha utawala, moja kati ya changamoto kubwa ambayo yanapata Mataifa hayo ni namna ya kuendeleza miradi au mipango ya mtangulizi aliyetoka madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na ukarejea hotuba mbalimbali kwa miaka mitano, sita, kumi iliyopita, unaona namna ambavyo Mheshimiwa Rais ameonesha siyo tu dhamira ya dhati, lakini ameonesha commitment ya hali ya juu kuhakikisha kwamba mipango ya watangulizi wake inakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuonesha commitment hiyo kabla, sijaanza kutaja mipango hiyo. Mama huyu ametupa dira kwa kusema kwamba na isitokee tena ndani ya nchi utawala ukibadilika mipango inabadilika. Akaamua kutengeneza Wizara maalumu, Wizara ya Mipango, akatengeneza Tume Maalumu ya Mipango akamweka Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo na mjomba wangu pale Mheshimiwa Nyongo, wasimamie Wizara ile kuhakikisha mipango ya nchi hii inayopangwa kwa miaka 25, miaka 50 itatekelezwa pamoja na kubadilika nyakati mbalimbali za mamlaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu na upande wa nishati, lile Bwawa la Stiegler’s, mipango yake ilianza kufanyika tangu miaka ya 1960. Watangulizi wake walihangaika kutekeleza wakahangaika na kuhangaika, lakini hivi tunavyozungumza leo mitambo yote imeshawashwa chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, turbine zote zimewaka, vijiji vyote 10,000 na kitu vimewashiwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya hayatokei hivi hivi, ni lazima uwe na kiongozi ambaye anasimamia shughuli hizi zitekelezwe, sio mwingine, ni Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, mambo haya hayatokei kama muujiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Wizara ya Kilimo, kama, ulikuwa humu Bungeni tunaongelea bajeti ya shilingi bilioni 200, leo tunaongelea 1.3 trillion. Kaka yangu Mheshimiwa Bashe, anasimamia, Mheshimiwa Waziri Mkuu anakimbizana nao kila siku, anaangalia namna ambavyo miradi inatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, leo sisi Tanzania tunajivunia tumeagiza ndege kwa maana ya (Aeroplane) ya kuua ndege wale waharibifu, ya kupulizia dawa. Haya mambo hayatokei hivi hivi, ni lazima uwe na viongozi makini kusimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa ukurasa wa sitini na ngapi? Anasema kwenye Wizara ya Maji, ndani ya mwaka mmoja visima vya maji 925 wastani kila jimbo moja la uchaguzi limepata visima vitano. Hivi mimi ni nani leo nishindwe kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ni nani kama nitakuwa sina uchungu na nchi hii? Akina mama wametuliwa ndoo kichwani. Nami Salome nilikuwa pale Shinyanga, tunatembea kilomita 13 kufuata maji ya kunywa na ya kutumia. Leo angalau kila Jimbo limechimbiwa kisima ndani ya mwaka mmoja, tena siyo kimoja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, anafanya kazi kubwa, anasimamia Serikali, anatusimamia na kazi inaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwetu Shinyanga Ibadakuli, ule uwanja wa ndege ilikuwa ni nightmare, ilikuwa ni ndoto. Kamati ya Bunge imeenda kukagua juzi uwanja, unakaribia kukamilika, ndege zitatua pale. Serikali inafanya kazi. Leo unatenganishaje demokrasia tuliyonayo na maendeleo makubwa na Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali iliyopo madarakani? Nitakuwa ni mtu ambaye sina shukurani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anaibuka mtu mmoja tu leo, unajua, naomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge wenzangu; hii nchi tumeanza uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1992 na mwaka 1995 tulikuwa na Wabunge wa Upinzani 51, mwaka 2000 tulikuwa na Wabunge wa Upinzani 26, wakati huo Mheshimiwa Mbowe ndio aligombea Urais; mwaka 2005, tulikuwa na Wabunge wa Upinzani 41, mwaka 2010 tulikuwa na Wabunge wa Upinzani 89, mwaka 2015 tulikuwa na Wabunge wa Upinzani 116 na 2020 tupo Wabunge 28 wa Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mtu aliyesema hashiriki uchaguzi mpaka tufanye mabadiliko ya sheria. Kwenye chaguzi zote, hakuna mtu aliyethubutu kusema hivyo, hakuna mtu aliyesema tuingie barabarani tufanye uasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna mtu mmoja aliyekuwa na tamaa ya Urais, ameukosa kwa sababu anajua Mheshimiwa Dkt. Samia amefanya kazi, anataka kumwaga mboga, anataka kumwaga ugali, na maji ya kunawa. Hatuwezi kukubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kukubali. Ukweli ni kwamba, kwa namna ambavyo mazingira ya uchaguzi yamewekwa, kwa namna ambavyo wameruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara, kwa namna ambavyo wametumia vibaya nafasi yao ya kufanya haki ya demokrasia, wamegundua kwamba wakishiriki uchaguzi huu, hawapenyi, ndiyo maana wameweka mpira kwapani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka yote awamu zote sita ambazo tumeshiriki uchaguzi kwenye hii nchi, CCM ni ile ile, Katiba ya nchi ni ile ile. Tume ya Uchaguzi imeboreshwa mwaka jana 2024, wanaweka mpira kwapani, hii haikubaliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, unaweza kusema yote kwenye hii nchi, lakini mimi Salome Makamba ni Msukuma wa Shinyanga, sina pa kwenda. Passport ya kusafiria kwenda nje nchi, nimepewa na Bunge. Sina pa kwenda, mama yangu, na familia yangu haina pa kwenda. Hatuwezi kuhamasisha uasi kwenye nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kung’ang’ania kitu kisichowezekana, kung’ang’ania kwamba hatuwezi kufanya uchaguzi, imebaki miezi mitatu twende kwenye uchaguzi; unang’ang’ania hatuwezi, na mtu ni Mwanasheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunajua humu ndani kwamba utaratibu wa utungaji wa sheria, na utaratibu wa kurejea sheria una namna yake ambayo unahitaji muda. Ni lazima tu-table mara ya kwanza, ni lazima tu-table mara ya pili, ni lazima watu watoe maoni, na ni lazima wananchi watoe maoni. Huo mchakato unahitajika. Mtu, ametia mpira kwapani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na wale wanaojiita sijui G55, sijui nani? Mimi naenda kugombea, na nitarudi humu Bungeni. Nimwambie Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimeona wameongeza bajeti. Baba ongeza mpunga, leta ballot paper, leta maboksi, sisi tupo tayari kwa uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mtu mmoja awe ndio anaamua kwamba hii nchi leo iwe Jumapili, kesho iwe Jumatatu, anaongea yeye, mwanaume yeye, kibaunsa yeye. Hatuwezi kukubali. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie kitu kimoja, mimi Mheshimiwa Salome na wananchi wa Shinyanga hasa akina mama tunasema hivi, yote yametekelezwa. Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia mitano tena, Mama Samia mitano tena, tumeyasubiri maboksi ya kura kwa muda mrefu, kwa ajili ya kuhakikisha tunapiga kura. Tunamvika huyu Mama nguo, tunamfuta machozi kwa kazi kubwa aliyoifanya, na kutukanwa kwa ajili yetu sisi wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walisema yote, mara ameuza bandari, mara sijui mama amefanya hivi. Sasa hivi wameishia kusema Mama akifungua pochi mambo yanatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo Kamati ya TAMISEMI, kwa mara ya kwanza kwenye nchi hii, nimeshuhudia kwa macho yangu jengo la mama na mtoto. Mimi nina Watoto. Jengo la mama na mtoto, yaani ukishindwa kujifungua kawaida, chumba kinachofuata unaweza ukafanyiwa operation; chumba kinachofuata kama mtoto wako ni njiti, unaweza kumweka kwenye chumba cha watoto njiti; chumba kinachofuata kama umefanyiwa operation, unaweza kupumzishwa pale. Haya mambo tuliyaona lini haya? Hatuwezi kukubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Ulinzi na Usalama lipo. Kaka yangu Mheshimiwa Bashungwa, Waziri wa Mambo ya Ndani upo, tekelezeni wajibu wenu. Hii nchi ni ya demokrasia. Kuzuia uchaguzi ni uhaini na hatuwezi kukubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie tu ukweli, huyu jamaa anataka kutupiga changa la macho. Chama chochote cha siasa lengo lake namba moja, ni kushika dola. Hilo ni lengo lake namba moja. Sisi hatufanyi kazi ya uharakati hapa. Najua siasa ni kushika dola. Haiwezekani hata siku moja, wamekaa nje huko, leo watu waendelee kukaa nje huko, hatuna kambi rasmi ya upinzani, hatuwezi kurudi Bungeni kama Waheshimiwa Wabunge, halafu unasema sisi ni wanasiasa. Hapana, ni lazima tushike dola. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wenzangu waliopo nje ninaungana nao. Ni lazima turudi humu ndani kama tulivyokuwa zamani. Lazima tukae humu ndani kama tulivyokuwa zamani. Serikali ishauriwe, ipokee ushauri; nasi tushauriwe, tupokee ushauri, tulijenge Taifa moja kwa umoja. Hiyo ndiyo kazi ya chama cha siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, uwakilishi wa wananchi, huwezi kuwakilisha huko kwenye majukwaa, na ndiyo maana unaona huko wanapofanya haina tija. Ni lazima tukae kwenye mabaraza ya vijiji, ni lazima tukae kwenye Baraza la Madiwani, ni lazima tukae Bungeni ili tuweze kuishauri Serikali kwa mfumo unaoeleweka. Huwezi kuishauri Serikali nje ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, rai yangu, tunataka uchaguzi, na tupo tayari kushiriki uchaguzi. Hatupo tayari kuungana na mtu ambaye anataka kupindua nchi hii na kuleta uhaini. (Makofi)

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, wapi? Mheshimiwa Ole-Sendeka.

TAARIFA

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri sana wa Mheshimiwa Mbunge, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kusema, uhuru bila demokrasia ni udikteta; lakini demokrasia bila ya nidhamu ni fujo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachoendelea hivi sasa ni sheria kuzingatiwa kwenye kuweka mipango ya kuwapa Watanzania fursa ya kutumia haki yao ya kuchagua. Ni dhahiri kabisa kwamba Mheshimiwa Mbunge alichokizungumza hapa, ameonyesha kabisa kama Yesu Kristo alivyosema, atakayenionea haya mbele za watu, nami nitamwonea haya mbele za baba yangu. Hakujali itikadi, hakujali jambo lolote, amemsifia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na rekodi iliyotukuka, aliyoionyesha. Dunia inajua, Tanzania inajua na wapinzani wanajua. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Salome Makamba unapokea taarifa?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hiyo taarifa naipokea. Kazi namba moja ya chama cha siasa ni kushika dola. Huwezi kushika dola kwa kwenda kwenye vyombo vya Habari, wala huwezi kushika dola kwa kwenda kwenye mikutano kuwaambia watu wafanye uasi na uhaini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unashika dola kwa kushiriki chaguzi huru na za haki. Unashika dola kwa kuhamasisha watu waende kupiga kura. Unashika dola kwa kuwa na ushawishi kwa vyombo vinavyotoa maamuzi ndani ya nchi hii, na kwa kufanya hivyo ndiyo njia sahihi ya kueleza yale ambayo unatamani yafanyike ndani ya nchi yako. Tofauti na hapo ni kinyume na Katiba, ni uasi na ni uhaini kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)