Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kunipatia uzima na afya njema. Nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya maendeleo iliyofanyika ndani ya nchi hii. Kila mtu anaendelea kushuhudia sehemu zote pande nne za nchi hii na dunia pia inashuhudia.
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge tunaomba utulivu kidogo. Mheshimiwa Ungele endelea.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashuhudia miradi hiyo mingi kama vile SGR na mingine. Sasa hivi usafiri kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam ni rahisi tu. Hata wenye changamoto ya miili, ni shida kwenye mabasi, lakini tunakwenda na SGR. Hiyo ndiyo kazi za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Lindi, tuna miradi mingi ya maendeleo, amefanya miradi mingi sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na inaendelea kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Sekta ya Afya. Katika wakati wote nilivyoendelea kutoa huduma za afya, sijapata kushuhudia kuona huduma za ICU zikiwepo kwenye ngazi ya Wilaya pamoja na wagonjwa wa dharura ndani ya wilaya, lakini kwa mikoa ya Lindi na kwingineko, hospitali za wilaya kumejengwa huduma hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye elimu kuna madarasa na kila kitu. Sasa hivi inajengwa shule kubwa ya wavulana ya sekondari pale Kiwalala kwenye Wilaya ya Lindi Vijijini kwa ajili ya mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi inayoenda kugharimu shilingi bilioni 4.1. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha hizo. Jambo hili hatujapata kulishuhudia, ndiyo sasa tunayaona mambo haya katika kipindi chake cha Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, sisi Wanalindi na Mtwara tumeshuhudia bei nzuri ya mazao ya biashara kama vile korosho, ufuta na mbaazi, na kila mmoja anashuhudia. Hapa ninapozungumza, kila mmoja anayesikiliza huko Lindi na Mtwara wanashuhudia na wanakubali jinsi alivyofanya mambo makubwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hakuna leo atakayekuja akatudanganya danganya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapita huko, lakini hakuna lolote. Wengine wanakwenda kushangaa tu kwamba kumbe huyu ndiyo bwana huyu! Lakini siyo kwamba wanasikiliza yale wanayoyasema. Hakika mambo mazuri yanaendelea kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa kwa jinsi alivyowasilisha hotuba yake jana kwa umahiri na umakini mkubwa sana. Masaa mawili tangu mwanzo mpaka mwisho, tone ya sauti ni ile ile na kutamka ni vilevile yaani mpaka mwisho, kiasi kwamba kila sehemu alikuwa anaendelea kusisitiza, kila point mpaka amemaliza nukta yake ya mwisho. Kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi anavyomsaidia Mheshimiwa Rais kwa namna kubwa sana. Nguvu zake na akili zake zote anamsaidia Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kujenga nchi hii. Hii inajidhihirisha vile Mheshimiwa Waziri Mkuu anavyopita kwenye mikoa, kwenye wilaya, na kwenye halmashauri zetu. Waheshimiwa Wabunge hapa tangu asubuhi walipoanza kuchangia imedhihirisha kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu zote zile zinazoonekana kuna shida, kuna changamoto au kuna kadhia fulani, akishaenda Mheshimiwa Waziri Mkuu pale kama ulivyosikia, hajali mvua, hajali jua kali, atasimama hapo juani, atasimama hapo kwenye mvua lakini yupo na wananchi. Hakika hatujapata kushuhudia mtu kama huyu. Tunaomba tuendelee kumwombea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa, humu ndani Wabunge wenzangu tutaendelea kumwombea Mheshimiwa Waziri Mkuu aendelee kuimarika na pia tunamwombea Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aendelee kumwamini kijana wake huyu, kwani ni msaada mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wizara ambayo ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, kuna kijana wake ambaye ni Waziri ambaye ni Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete akisaidiwa na Mheshimiwa Patrobass Katambi. Vijana hawa ni wanasheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nipo kwenye Kamati ile ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ambayo tunasimamia Wizara hiyo. Vijana hawa pamoja na Katibu Mkuu, Maganga na Watendaji wao wote ni watu mahiri, na ni watu wapo imara wanaosimamia kazi yao ambayo wamekabidhiwa. Tunawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hiyo hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, kuna taasisi hizi za hifadhi ya jamii; NSSF, PSSSF, WCF, OSHA na CMA. Taasisi hizi wamekuja hawa watendaji na ubunifu mkubwa kweli. Sasa hivi huduma zao wanaendesha kidijiti. Pia, kwenye uwekezaji, wanafanya uwekezaji mwingi kwenye mambo ya ujenzi. Tunawapongeza kwa sababu ni uwekezaji wenye tija, unaoenda kuhakikisha kwamba mwisho wa siku mafao ya wastaafu wetu yatatolewa katika uhalali wake na kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye changamoto tulizonazo, kuna changamoto ya barabara hii ya Kibiti - Lindi. Barabara hii ni ya muda mrefu sana, tunakubaliana humu ndani na kama kuna wasiofahamu, basi wanaweza wakaendelea kurejea Hansard ya Bunge zilizopita kwa miaka iliyopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, b,arabara hii pia ipo pembezoni mwa Bahari. Tangu inaanza Dar es Salaam mpaka inapofika Mtwara ni pembezoni mwa Bahari wa Hindi. Ni kilomita chache tu kutoka bahari ya Hindi, ndiyo barabara hii ilikopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini sasa kinachoendelea? Kwa kuwa barabara hii ipo pembezoni mwa bahari ya Hindi, kwa hiyo ardhi yake ipo na unyevunyevu. Mito yote inayotoka huko milimani kwenye hifadhi ya Selous, kwenye milima ya Matumbi, kwenye Wilaya hizo za Ruangwa, Nachingwea, kote huko inazoa inapeleka baharini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, barabara hiyo ni laini sana kiasi kwamba mvua kidogo tu ikinyesha basi barabara ile inaweza ikabomoka, na ndicho kilichotokea mwaka jana 2024 kwenye ile mvua kubwa na kile kimbunga cha Hidaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishuhudia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyafanya mambo makubwa, akatoa fedha za dharura na kazi ile ikafanyika mwaka jana, 2024. Hata hivyo, ilifanyika kwa muda tu ili isaidie wale watu kwa muda. Mwaka huu pia imejirudia tena, mvua kubwa imenyesha na barabara imebomoka tena na madaraja yamezolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, sisi Wanalindi hatuna mashaka, hatuna wasiwasi na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na hatuna mashaka na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa ambaye anasimamia shughuli za Serikali ndani ya Bunge hili. Kwa kuwa anamsaidia sana Mheshimiwa Rais, kazi hii Dkt. Samia Suluhu Hassan anakwenda kuimaliza. Sisi Wanalindi tuna imani sana na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaenda kuijenga hii barabara upya tena kuanzia Kibiti mpaka Lindi, mpaka Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna imani sana na ndiyo maana sisi Lindi tunasema, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mitano tena. Tunaamini kabisa hata kama ikiwa namna gani, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hatashindwa. Hatashindwa ile barabara ya kutoka Kibiti - Lindi - Mtwara, kuijenga upya kwa sababu ameyafanya mambo makubwa ndani ya nchi hii na anaendelea kuyafanya mambo makubwa ya maendeleo ndani ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Naomba kwa asilimia zote bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu ipite kwa asilimia zote, ahsante sana. (Makofi)