Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi na nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema aliyenijalia uzima kusimama tena kwenye Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nawashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Nkasi Kaskazini kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wananipatia, na imani kubwa waliyoijenga kwangu kuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya nchi yetu na Mkoa wetu wa Rukwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini. Imani hiyo nimeilinda na nitaendelea kuilinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ziara aliyoifanya kwenye Mkoa wetu na Jimbo langu. Ziara zote ambazo amekuwa anazifanya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni ziara zenye tija, zenye maagizo na unaona faida ya ziara anazokuwa anazifanya. Kwa hiyo, upande wa kumsaidia Mheshimiwa Rais, naye kama Mtendaji Mkuu wa Serikali, kiukweli viatu hivyo vimemtosha, amevitendea haki, na ameitendea haki nafasi hiyo. Pamoja na mema mengi ambayo yalifanyika kwenye ziara yake, nina mambo machache ya kushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda kwenye kushauri, jana Mheshimiwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Tundu Antipas Mugwai Lissu, amekamatwa Ruvuma. Tungependa Serikali, kwa kuwa yule ni Kiongozi Mkuu wa Chama Kikuu cha Upinzani, taarifa za kukamatwa kwake na sababu ziwekwe hadharani Watanzania wazijue, na haki itendeke kama Mtanzania mwingine.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa mdogo wangu Mheshimiwa Khenani, Mbunge wa Nkasi. Kwa kweli ingekuwa mimi katika nafasi yake, nisingesimama kumsemea kiongozi asiye na heshima kama yule. Nisingethubutu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiongozi huyo anayemwita yeye ni kiongozi, mimi nimemshangaa. Yaani badala ya kuongea na wananchi mambo ya msingi, ameenda kupeleka matusi na kuwadharau wananchi wa Nyasa kwa kuwasemea matusi ya viongozi wao. Akome, akome, akome kabisa!
MWENYEKITI: Mheshimiwa Aida Khenani umepokea taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Manyanya?
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba tu mama yangu, nimelelewa, nimefundishwa, yule ni mama yangu na amekuwa Mkuu wangu wa Mkoa wa Rukwa. Ni wajibu wangu kama Mbunge, na nimesimama kuiambia Serikali, haki itatendeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini historia ya nchi yetu itaendelea kujengwa kwa amani na utulivu. Kama kuna kosa limefanyika, liwekwe hadharani na sababu za kukamatwa. Naomba niendelee.
MWENYEKITI: Endelea na mchango wako.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mengi yaliyofanyika na Serikali, nina ushauri kwenye mambo kadhaa. Jambo la kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu, mwaka 2024 na mwaka 2023 tumezungumza juu ya usafiri wa Ziwa Tanganyika. Tumelisema kwa kina, kwenye vitabu tunasoma kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Tanganyika uwekezaji ambao Serikali imeweka kwenye bandari hakukuwa na sababu leo tuzungumzie ukosefu wa usafiri wa uhakika wa Ziwa Tanganyika. Tunawezaje kuwekeza Bandari ya Kabwe, Bandari ya Kasanga, Bandari ya Kipili, Bandari ya Kalema halafu usafiri haupo kwenye Ziwa Tanganyika? Tulitaka ku-achieve nini kwenye hizo fedha tulizowekeza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. MV Liemba ni meli ambayo imeharibika muda mrefu sana, MV Mwongozo, sababu zake ukiziona, hakukuwa na sababu ya kukaa zaidi ya miaka nane. Leo tulitegemea wananchi wa Mkoa wa Rukwa kwenye hotuba yake ambayo inatoa mwelekeo wa nchi tujue, sisi Wanarukwa ambao tunaamini uchumi wetu unatokana na mazao tunayolima ikiwemo mpunga na mahindi, na watu wa Kongo wanategemea mazao kutoka Tanzania, tunasafirisha kwa njia gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwenye hili eneo kumekuwa na changamoto kubwa. Kila siku tunapoteza ndugu zetu kwa usafiri usiokuwa rasmi. Tunawezaje kupeleka meli mpya, iwe ni mbili au tatu kwenye ziwa moja, wakati Ziwa Tanganyika ambalo tungewekeza kwa kina ingesaidia uchumi wa mkoa na uchumi wa Taifa? Leo kutueleza habari tu ya ukarabati, na kuchukua muda wote huu Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninaamini Wanarukwa hatujatendewa haki. Tumechoka kulia juu ya wananchi wetu kupoteza maisha kwa sababu ya biashara wanazozifanya kwa usafiri wanaotumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani kwenye hitimisho lake mtoa hoja, atueleze Wanarukwa, Kigoma na Katavi hatima ya usafiri wa uhakika wa Ziwa Tanganyika, Ni lini tutapata meli mpya? Meli hizo za ukarabati tu, ni lini zitakamilika ili tuweze kuinua uchumi wetu wa Mkoa wa Rukwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la uanzishwaji wa mamlaka za kiutawala. Hili jambo limekuwa kama favor hivi, lakini lipo kwa mujibu wa sheria, na nimelisema leo wakati nauliza swali. Nimesema hivi, Tume kutoka TAMISEMI 2013 ilifika Nkasi, wakaangalia vile vigezo vyao vyote 13, wakasema tumekidhi vigezo. Ni nini kinatokea leo mpaka nazungumza mara kadhaa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Namanyere upande wa TANESCO, badala ya kulipa shilingi 27,000/= wameingizwa kwenye kulipa shilingi 320,000/=. Kwa nini? TANESCO wanatumia Sheria ya Mipango Miji. Kwa hiyo, huku wanahukumiwa wakati mmeshindwa kutimiza wajibu wenu. Kwa nini tunawatia kwenye maisha magumu bila sababu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema, kama tunasema bado tunaendeleza yale maeneo tuliyoanzisha huko nyuma, tufute kwanza hizi mamlaka mpaka tutakapojiandaa, wasiendelee kuhukumiwa kwenye hili jambo. Ukiwaangalia maisha yao ni ya kawaida, lakini TANESCO wanatumia Sheria ya Mipango Miji; na hili eneo siyo kwa Namanyere tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, nilishapeleka mpaka kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu document ikiwa imekamilika. Tume walizoziandaa, zimekwenda kule, kama hatujaamua leo kutoa halmashauri ya Mji wa Namanyere tukafute ile Mamlaka ya Mji Mdogo, waendelee kuishi kama zamani ili tuache kuimba huu wimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza haya, pamoja na kwamba lipo kisheria, nakubaliana kwamba kuna maeneo ambayo lazima waendeleze hayo majukumu mengine ya kimaendeleo. Sasa kama ndivyo, kipaumbele chetu kama Taifa ni nini? Hebu wewe fikiri, Mkoa wa Rukwa toka mwaka 1984, kaangalieni Halmashauri ziko ngapi? Mbona wengine wana Halmashauri nyingi, halafu Rukwa ni chache! Mikoa mingine mnaionaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kuanzisha hizi mamlaka ni kupeleka huduma kwa Watanzania. Sasa kama kuna shida imejitokeza hivi karibuni, kwanza ile sheria yenyewe tuibadilishe ili tujue kwamba sasa hivi kuongeza maeneo ya kiutawala ni favor au mtu aamue tu kwamba inakaaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, natambua jitihada za Serikali upande wa kilimo, na eneo hili limefanya vizuri sana kwa kuongeza bajeti, lakini hata utendaji wake. Leo wakulima wameongeza tija sasa ya kilimo chao baada ya kuweka ruzuku kwenye mbolea. Nataka kushauri jambo moja hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2024 wakati Mheshimiwa Rais amekuja kwenye Jimbo langu, akasimamia kama kiongozi wa nchi na kusikiliza kilio cha wananchi. Nikamweleza juu ya changamoto ya bei, aliongeza bei pale, sasa hatuwezi kuwa tunasubiri mpaka aje kiongozi ndiyo tuzungumze changamoto ya bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu anajua kila mwaka lazima twende kwake kumwambia kuna changamoto ya bei ya mahindi. Sasa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anafanya kazi nzuri, mbolea imekwenda, watu wamezalisha. Tunachotaka, ni uhakika wa masoko ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaenda kwenye msimu wa mavuno, mvua zinaendelea, kwa hiyo, mazao yataharibikia shambani. Ni wajibu wa Serikali kuona ni kwa namna gani inakwenda kumkomboa mkulima kama ilivyodhamiria kwa kuweka ruzuku kwenye mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo naweza kulishauri ni kwamba, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, kwa sababu anamsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali kwenye eneo hili, hiki ni kipindi ambacho wakulima wengi wanatamani kutoka kuwa wakulima wadogo kwenda kuwa wakulima wa kati au wakulima wakubwa. Serikali iangalie namna ya kuwakopesha hizi mbolea waje walipe kulingana na kilimo ambacho wanakipata, wasikose haki ya kupata mbolea kwa sababu hawana fedha. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Muda wako umeisha.
MHE. AIDA J. KHENAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa muda ulionipatia. Ahsante. (Makofi)