Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Hamida Mohamedi Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Lindi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, nami naendelea kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwanza kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwasilisha hotuba yake nzuri yenye kurasa zaidi ya 100 hapa Bungeni. Ni hotuba ambayo imesheheni mambo mbalimbali ya maendeleo katika nchi yetu. Nampongeza na kumtakia kila la heri katika majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, naendelea kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kila Mheshimiwa Mbunge aliyesimama hapa Bungeni, ameendelea kumpongeza kwa uwajibikaji wake katika Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi ndugu zake, wananchi wa Lindi tunapata faraja sana kwa kutuheshimisha katika uwajibikaji wake katika shughuli zake za Serikali. Tunaendelea kumwombea kila la heri, Mwenyezi Mungu aendelee kumlinda na ampe baraka. Pia, wananchi wa Ruangwa na wananchi wa Lindi wote tuna imani kubwa naye na tumesema hatuna mbadala mwingine zaidi yake. Kila la heri na Mwenyezi Mungu aendelee kumwongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, yale yote ambayo yameelezwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mambo ambayo Mheshimiwa Rais wetu ameendelea kupambana, kuhakikisha kwamba ni lazima alete maendeleo na mapinduzi ya kweli katika nchi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, ni mwanamke pekee Tanzania ambaye hatuna mfano wake. Tuendelee kumtakia heri na kumwombea kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kumwongoza kuhakikisha kwamba anaendelea kutimiza majukumu yake yake ambayo amedhamiria kuyatekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba katika maendeleo makubwa ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameyaelezea katika hotuba yake, nasi tumefaidika nayo, kwa sababu tulikuwa kwenye giza kubwa, lakini leo Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametutoa kwenye giza na ametuweka kwenye mwanga na sasa tunasonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, wiki moja iliyopita Mheshimiwa Tundu Lissu alikuja Lindi Mjini, lakini mapokezi yake yeye mwenyewe ameyaona kwa macho, na amewaambia wananchi wa Lindi kwamba, najua kwamba mna misimamo yenu, nasi tunasema tuna misimamo yetu. Lindi ni ya Samia na tunakwenda na Samia 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mazuri ambayo yametekelezwa kwenye kipindi cha miaka minne cha Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia, yako mazuri ambayo yametekelezwa katika Jimbo letu la Lindi Mjini. Kabla ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia, hatukuwa na Hospitali ya Wilaya ya Lindi; na tangu uhuru upatikane, Lindi Mjini hapakuwa na Hospitali ya Wilaya, lakini leo tunavyozungumza, Lindi Mjini tuna Hospitali ya Wilaya na tumeanza kutoa tiba kwa sababu Mheshimiwa Rais ametupa mapenzi makubwa na kujali afya za Wanalindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, yako mambo mbalimbali yaliyotekelezwa. Hatukuwa na shule za sekondari za kutosha, lakini leo tunapoongea, Jimbo la Lindi Mjini tuna shule tano mpya za sekondari. Tunahakikisha kwamba watoto wetu wote hakuna anayekosa kwenda shuleni kwa kukosa darasa la kusomea. Kwa hiyo, tumepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka minne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, tunazo changamoto mbalimbali. Ukiangalia upande wa Sekta ya Maji, tunayo miradi ambayo haijakamilika. Tunataka wananchi wa Lindi waendelee kufaidika na rasilimali ya maji kwa kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba Mheshimiwa Jumaa Aweso, Waziri wa Maji, amepiga hatua kubwa sana kuhakikisha kwamba amesimamia utekelezaji wa miradi ya maji Lindi, ili wananchi waweze kupata maji safi na salama, lakini bado tuna huduma mbalimbali ambazo tunazihitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa maji wa Mkundi ambao unagharimu shilingi milioni 326. Nikisema Mkundi, Mheshimiwa Jumaa Aweso anajua, ni upande wa pili wa bahari, wananchi wanahitaji mradi huu wa maji uweze kukamilika. Kwa hiyo, tunaomba tukamilishiwe hizi shilingi milioni 326 ili tukamalize mradi wa maji ili wananchi waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunao mradi wa Angaza ambao unahudumia pale katikati ya mji, tunahitaji shilingi milioni 172 ili tumalizie. Mkandarasi amesimama anashindwa kukamilisha mradi huu. Kwa hiyo, tunajua kwamba Serikali imewekeza nguvu kubwa ya kuleta fedha nyingi ili kutekeleza miradi ya maji, lakini bado nguvu hii kubwa haionekani kwa sababu wananchi wengi hawajaunganishiwa maji nyumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Jumaa Aweso akamilishe ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kutupatia shilingi milioni 500 kwa sababu alizungumza mbele ya wananchi ili tusogeze miundombinu ya maji na wananchi waweze kuvuta maji majumbani mwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wetu wa Lindi unategemea uboreshaji mkubwa wa Barabara. Tunajua kwamba Lindi tuliathirika sana na mvua za mwaka uliopita. Kimbunga Hidaya kilituathiri kwa kiasi kikubwa sana na tumechelewa kurekebisha miundombinu kwa kukosa fedha kwa wakati. Ninaiomba sana Serikali kuhakikisha kwamba wanatuletea fedha kwa haraka ili tuweze kuboresha barabara zetu na tuweze kuendelea kufanya kazi, na pia wafanyabiashara na wakulima waweze kuendelea kutumia barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba barabara ya Kibiti – Lindi imepata changamoto. Wiki hii kumetokea mafuriko makubwa, lakini ukiangalia uharibifu uliotokea ni mkubwa sana. Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Ulega, ameendelea kuwepo katika eneo kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kupata huduma ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi aangalie Daraja la Mbwemkuru, daraja lile linaliwa kwa kasi kubwa kwenye kingo za barabara kunakoshikilia daraja. Mto ule umeendelea kupanuka na maji yanakula barabara kwa kasi kubwa sana. Sasa tusipokwenda kuchukua hatua kwa haraka, maana yake daraja lile linakwenda kuvunjika, litazama na juhudi zote zinazofanywa na Serikali hazitasaidia kwa sababu daraja lile ni kubwa na likikatika maana yake mawasiliano yanakatika kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi ahakikishe kwamba anakwenda kusimamia kwa haraka kutafuta dawa ya haraka na kuweza kunusuru daraja lile lisiweze kuporomoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunaishi kwenye ukanda wa bahari na tunajua kwamba katika bahari yetu kumetokea uharibifu mkubwa wa mazingira, ardhi yetu inaendelea kuliwa kwa kasi kubwa sana, lakini nimeizungumza hoja hii karibu mara tatu hapa Bungeni. Mheshimiwa Waziri Mkuu alishatoa maagizo kumwagiza Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira kuja kutazama ili kuona ni kwa namna gani wanaweza kutusaidia kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali ihakikishe wanakuja Lindi kuangalia ili kuwanusuru Wanalindi na bahari ile isiendelee kula nchi kavu ili kuhakikisha kwamba mji wetu unanusurika. Tusipochukua hatua kwa haraka, maana yake changamoto kubwa itakuja kutokea mbele ya safari. Tuna kilomita 570 zinazohitaji kufanyiwa ukarabati kwa haraka ili kunusuru mazingira ya bahari yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo yote mazuri yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, bado katika Mji wetu wa Lindi ukiangalia jiografia ya Mji wa Lindi ni miteremko na vilima, lakini udongo wake ni wa mfinyanzi. Kwa hiyo, katika upande wa TARURA, tunashukuru kwamba Serikali inatupatia fedha kila mwaka shilingi bilioni 3.6, lakini kutokana na mazingira na changamoto kubwa iliyopo, tunahitaji kuongezewa fedha hizi tuweze kuboresha barabara zetu ili ziwe kwenye ubora unaostahili ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Lindi wanaendelea kutumia barabara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambazo tunaletewa, tunashindwa kutengeneza hata kilomita mbili za lami, ni fedha kidogo, lakini ukiangalia mtandao wa barabara ni kilomita 564. Barabara ambazo zina lami hazizidi hata kilomita 200. Kwa hiyo, bado tuna changamoto kubwa ya kuhakikisha kwamba tunaendelea kuwekeza ili kuboresha barabara zetu.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakushukuru na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)