Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Kwanza, nami nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Ardhi anayeendelea kutujaalia afya pamoja na uzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufanya majukumu yake ambayo wananchi wa Tanzania pasipo shaka wanaona gurudumu linakwenda vile ambavyo limekusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi hizi zinaenda sambamba kwa viongozi ambao wanamsaidia Mheshimiwa Rais akiwemo Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango na Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani za mwisho ni kwa Wizara husika ambayo inamsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na hotuba nzuri ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameiwasilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia maeneo mawili. Eneo la kwanza ni la maji na mafanikio yake; na eneo la pili ni miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema hapa, nami Mbunge wa Jimbo la Kibamba ni lazima niwe shuhuda. Huu ni mwaka wangu wa tano ninazungumza humu, lakini miaka mitatu hivi ya mbele ilikuwa ni kila siku ninazungumza juu ya hili hakuna, lile hakuna na hili hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli sasa hivi kila jambo liko kwenye njia. Mambo mengi yamefanyika kwa zaidi ya 90%, mambo yaliyobaki ni madogo madogo. Mfano mzuri, mara nyingi nilikuwa nikisimama hapa nilikuwa nazungumza juu ya maji, lakini nataka niseme, Kamisaa wetu ndugu yangu Jumaa Aweso, Mbunge, amefanya kazi kubwa sana kwenye Wizara yake ya Maji. Katika hili amemsaidia Mheshimiwa Rais vile ambavyo alikusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu Kibamba kuna matenki makubwa matatu. Baada ya kuyakamilisha kama vihifadhia maji, lile la Tegeta ‘A’ lina ujazo wa lita milioni tano, la Mshikamano lina ujazo wa lita milioni sita na lile ambalo mmekamilisha juzi la kule Bangulo ambalo linasaidia wananchi wengi wa Kusini mwa Dar es Salaam na kwangu Kibamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake King’azi ‘A’ na ‘B’ ambao hawakuwa na maji kabisa, maeneo ya Mtaa wa Saranga ambao ni maeneo ya Mashujaa, eneo la Mpakani na eneo la Mtaa wa Ukombozi, maeneo haya yote hayakuwa na maji, lakini nashukuru sana sasa hivi wanaendelea kupeleka usambazaji wa maji na watu wengi wanashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wWanasema Mheshimiwa Mbunge, ule mradi wa ujazo wa lita milioni tisa uliokuwa unausema Bungeni mara nyingi, ambao shilingi bilioni 37.8 za Benki ya Dunia zimetumika. Sasa wananchi wengi wa Kusini mwa Dar es Salaam ambao kwa Jimbo la Kibamba ndiyo walikuwa bado wana shida ya maji, sasa hivi wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kukamilisha mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mara nyingi huwa napenda kutoa elimu katika eneo hili. Mheshimiwa Waziri huwa anajitahidi sana kutupa elimu kwa upana juu ya changamoto ya maji katika historia na sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda wananchi wa Dar es Salaam na Pwani kwa ujumla wakiwepo wa Kibamba wajue, kazi ambayo tumeifanya katika kipindi cha miaka mitatu minne ni kutengeneza matenki makubwa ya kuhifadhia maji ili nyakati nyingi za kiangazi ambazo zinaweza zikaja, tujikute tunayo maji ambayo yanaweza kuwafikia waliopo mbali, lakini ukweli ni kwamba maji bado siyo toshelevu kwa walio wachache. Wengi wamepata, lakini wengine bado wanalia juu ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie ukweli kwamba chanzo cha maji ni Ruvu. Ruvu Juu ndiyo inatulisha katika kipindi chote toka tumepata uhuru. Sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1910, ikaruka tukaenda kuanza upya 1968 na sensa ya mwisho ya sita tumefanya 2022. Dar es Salaam ilikuwa ina watu gani mwaka 1967? Sensa ya mwaka 2022 imekuwa na ongezeko la population kiasi gani? Lakini chanzo bado kilikuwa ni Ruvu Juu. Kwa hiyo, ni lazima tujue watu wanaendelea kuongezeka, lakini chanzo ni kile kile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan peke yake kwa kufikiria jambo hili, ndiyo ameenda kuanzisha mradi wa Bwawa la Kidunda. Nataka niwaambie, Bwawa la Kidunda mpaka mwezi Machi, 2025 lilikuwa limefika 28%. Hili likikamilika, linaenda kujaza ujazo wa lita bilioni 190. Mheshimiwa Waziri anajua hili, lakini fedha zinazohitajika kutumika pale ni shilingi bilioni 335. Fedha hizi siyo nyingi kwa Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumeambiwa amekamilisha bwawa au mradi wa maji kule Rufiji wa zaidi ya shilingi trilioni sita nukta kadhaa, atashindwa shilingi bilioni 335 kukamilisha Bwawa la Kidunda ili maji yawe ni sustainable kwa Mikoa ya Pwani, Morogoro na Dar es Salaam? Kwa hiyo, tunamtakia Mheshimiwa Rais kila la heri katika mradi huu. Mradi huu utatusaidia sasa maji yatapatikana Dar es Salaam kwa muda wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo juu ya eneo la miundombinu. Jimbo la Kibamba wakati tunaingia, hali ilikuwa ni mbaya sana, lakini sasa hivi barabara nyingi zimepata wakandarasi na wananchi wanajua hilo na barabara nyingi zimejengwa kwa zege na lami zinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mwepesi, tunao mradi wa DMDP chini ya TARURA, ambao mpaka sasa tayari wakandarasi wameshasaini mikataba na Mheshimiwa Waziri Mchengerwa. Kwa mfano, barabara ya Makabe – Msumi yenye kilomita 11.2 na daraja lake sasa hivi tayari Mchina yuko site anaendelea. Wananchi wana furaha kwenye jambo hili na wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni barabara ya Mkorea Road – Goba yenye kilomita 7.7. N,ataka niwaambie kuna Daraja la Mama Katunzi tulilijenga mwaka 2022 na sasa hivi barabara nzima inaenda kujengwa na mkandarasi amepatikana. Mwisho, ni kule ambako tunajenga VETA ya Wilaya ya Kibamba – Kibwegere, barabara ya Shija Road, kwa heshima ya Mzee wetu Shija William Shija, tuliipa hiyo barabara jina lake, na sasa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amekubali kujenga lami kilomita 4.2 na mkandarasi amepatikana. Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie, hizo ni barabara za TARURA ambazo ziko chini ya mradi wa DMDP, lakini TANROAD na yenyewe imeendelea kuwepo ndani ya Jimbo la Kibamba kwa barabara chache cha haraka. Barabara ya njia panda ya shule inayoenda Mpiji mpaka sasa ipo kilomita ya saba ya lami na mkandarasi yuko site anaendelea. Haya mambo huko nyuma hayakuwepo. Pia, kuna barabara ya Matosa kuelekea Temboni, kilomita sita. Kilomita tatu tayari mkandarasi yupo na anaendelea na ujenzi wa barabara hiyo. Nashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo barabara ya pale Kimara inayoenda Bonyokwa, mara nyingi nimeisema hapa. Tupo Waheshimiwa Wabunge wote watatu, sasa hivi mkandarasi ameshalipwa na yupo site, anaendelea kujenga lami ya kilomita zote saba. Mimi kama Mbunge wa Kibamba, lazima niziseme shukrani. Huu mwaka siyo wa kulalamika, ni mwaka wa kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ya Awamu ya Sita kwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mheshimiwa Mbunge anasema huku mambo ambayo wamefanyiwa au ambayo wamefanikiwa. Huyu ni nani? Ni zaidi ya Rais mwenye macho makubwa yenye kuona kila pembe ya nchi hii, tunaona na tunapata maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niseme wazi Mheshimiwa Rais anatudai sisi Jimbo la Kibamba na Wilaya ya Ubungo, tuna haki ya kutoa kura za kutosha kwa Mheshimiwa Rais. Pia, kwa kuendelea na utetezi wa Wabunge wote, kaka yangu Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo, Jimbo la Ubungo na Kibamba, ni mimi Issa Jumanne Mtemvu, kwa kishindo sana asubuhi tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)