Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Abdulhafar Idrissa Juma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelekezo yako.

MWENYEKITI: Basi changia kwa dakika tano.

MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kwa kunipa nafasi. Katika muda wangu huu, naomba niipongeze sana Serikali kwa kuendelea kufanya mambo muhimu na hasa yale ambayo tumeahidi katika Ilani yetu ya mwaka 2020/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yaliyosemwa katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, na yale tuliyoyaandika katika Ilani yamedhihirisha kwamba CCM huwa inapanga maendeleo kwa ajili ya Taifa na yeyote atakayekuwa Serikalini atatenda yale yaliyoelekezwa na CCM kwa maslahi ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tukaona Daraja la Kigogo – Busisi limekwisha, ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere umekwisha na mambo mengine yote yaliyoahidiwa katika Ilani pamoja na mtihani uliotokea kwa Taifa letu, lakini Mheshimiwa Rais, Mama Mheshimiwa Dkt. Samia ameweza kuyatekeleza. Hii ni kwa sababu anatoka katika Chama cha Mapinduzi ambacho kina utaratibu mzuri wa kutenda kwa ajili ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niishauri Serikali jambo moja. Hivi karibuni kumetokea changamoto kidogo kwa vijana wetu wanaosoma elimu, wanaomaliza diploma, walivyoomba kwenda kwenye degree kwa course ya Pharmacy, hakuna muunganiko mzuri sana kwa TCU pamoja na NACTE katika kuwachukua wanafunzi wanaotoka katika ngazi ya diploma kwenda katika ngazi ya degree kwa upande wa Pharmacy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vya mwanafunzi kujiunga na elimu ya diploma ya Pharmacy kwa mujibu wa NACTE vinamtaka afaulu Chemistry, Biology na masomo mengine yoyote lakini wanafunzi hawa walipoenda kuomba kujiunga na degree wakashindwa kwa sababu TCU, imeongeza kigezo cha kuangalia matokea yao ya Kidato cha Nne, siyo kuangalia GPA pekee yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wanafunzi ambao hawakuweza kufaulu mfano katika Somo la Physics, Mathematics pamoja na kufaulu Chemistry na Biology hawakupata nafasi ya kujiunga katika vyuo vikuu ili kuendelea na degree kwa sababu vigezo hivyo haviendani na TCU pamoja na NACTE.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ushauri wangu kwa Serikali? Ikiwa TCU itaboresha vigezo vya kuwapa nafasi vijana kuendelea na elimu ya juu, basi waangalie kwanza vijana waliopo na waangalie vijana ambao hawatoki Kidato cha Sita kwenda kwenye degree, wanatoka katika elimu hii ya kati ambayo inasimamiwa na NACTE.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hii imetokea, hata mimi Jimboni kwangu Mtoni wapo vijana wengi nilikutana nao katika ofisi yangu ya Jimbo. Wao walisoma Diploma ya Pharmacy, walipomaliza Kidato cha Nne, lakini kwa sababu hawakufaulu Somo la Physics na Mathematic na halikuwa katika vigezo vinavyowapa fursa ya kujiunga na Diploma ya Pharmacy lakini kwenda katika degree wamezuiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu kwa sababu kazi yake ni coordination ndani ya Serikali waone navyoweza kui-coordinate NACTE pamoja na TCU watengeneze suluhisho kwa maslahi ya vijana wale wa Jimbo langu la Mtoni na maslahi ya vijana wengi ambao wamekosa fursa hii kwa sababu ya kigezo hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa, kwa sababu kule Zanzibar, moja ya mambo ya manufaiko ya Muungano ni TASAF. Naomba niipongeze Serikali yetu katika miaka mitano hii kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kuimarisha TASAF, lakini nina ombi la ziada pale TASAF itakaporudi na kuongezeka, waone wanavyoweza kuongeza wanachama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jimboni kwetu kule bado maskini, ni wengi waliangaliwa na hawakupata fursa ya kunufaika na TASAF, lakini pia TASAF ina muda maalum wa kupitia wanachama wake na kuwaongeza. Naomba muda huu uwe wazi kwa sababu watu maskini wanajulikana wakiwekwa katika vile vigezo vya kuigizwa katika kunufaika na TASAF basi, isisubiri ile mara moja kwa mwaka waendelee ku-update kulingana na upatikanaji wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa, naishukuru Serikali kwa kuendelea kuwawezesha wanachama wa TASAF kwa kuwapa ruzuku pale kila muda unapostahiki, lakini nawaomba zaidi mradi utakapokuja, basi waongeze ruzuku ile kwa sababu gharama za maisha zimepanda na muda mrefu wanufaika wa TASAF wamekuwa wakipewa gharama ile ile ama ruzuku ile ile moja kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuongeze fedha ili wanufaika wa TASAF waendelee kunufaika na ule msaada wa Serikali iliyo chini ya CCM kwa wananchi wake uendelee kuleta matunda kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa, nimalizie kwa kuwapongeza sana wasimamizi wa TASAF kule Zanzibar, Unguja na Pemba. Naomba nimpongeze TMO wa Pemba kwa maendeleo makubwa na matunda ya TASAF ambayo yameonekana Pemba. Pia, naomba nimpongeze TMO wa Unguja ambaye anasimamia na Jimbo langu, wananchi wameendelea kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Serikali ikifikiria kuendelea kuwatumia vijana kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, basi ni vema ikaendelea kuwafikiria vijana hao na vijana mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)