Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manonga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Binafsi napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima na afya njema kuweza kuhudhuria katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, napenda kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya katika kipindi chake cha uongozi. Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amepata uongozi katika kipindi ambacho Taifa letu tulikuwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, lakini Mwenyezi Mungu alimpenda, baada ya kumpenda akatupa tunu nyingine, tukampata Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, Taifa hili ni Taifa la Mungu kwa maana katika kipindi kigumu ambacho tumekipitia, kama Taifa, tumeweza kuvuka salama. Mwenyezi Mungu kwa hekima kubwa alizomjalia Rais wetu, ameweza kutekeleza yale yote ambayo yalikuwa ndani ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa katika kipindi cha miaka mitano 2020/2025. Kwa kweli, tunampongeza na kumwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema, aweze kuhudumu tena kwa kipindi kingine cha miaka mitano, 2025/2030. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, napenda kutumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa kipindi chote ambacho ameweza kuhudumu, sasa anaenda kukamilisha miaka 10 katika nafasi ya Uwaziri Mkuu, nampongeza sana. Utendaji aliokuwa akiufanya alipokuwa Waziri Mkuu kipindi cha Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ameendelea kuwa hivyo hivyo ama zaidi katika kipindi cha Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu hongera sana, kazi yako ni njema. Tumeona umekuwa msaada mkubwa kwa Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan sehemu zote katika Taifa hili, lakini pia, umekuwa mstari wa mbele katika kuisimamia Serikali na Mawaziri wote ndani ya Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa akifanya ziara maeneo mbalimbali. Hata hivi karibuni alikuja Jimboni kwetu Manonga, ndani ya Wilaya yetu ya Igunga na ameingia kipindi ambacho ni muda mrefu kumekuwa hakuna mvua, zimesimama, lakini siku aliyoingia yeye, mvua kubwa sana ilinyesha ndani ya Wilaya yetu ya Igunga. Mwenyezi Mungu, na yeye pia ni shahidi kwamba ilikuwa ni neema. Wananchi walifurika kumsubiria Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mvua kubwa, wananchi wa Simbo walijaa, walivumilia, walinyeshewa na mvua. Ama kwa hakika Mwenyezi Mungu amekubariki na tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu, Mheshimiwa Rais akipata tena awamu ya 2025/2030, ikimpendeza, tunakuombea akurudishe kwenye nafasi hiyo ya Waziri Mkuu kwani unatosha na unaweza kuifanya hii kazi vizuri. Umekuwa ni kiongozi unayeleta matumaini kwa Watanzania, Mungu aendelee kukubariki na kukupa afya njema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho naweza nikasema katika huu mpango ambao ameuwasilisha Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kweli kuna mambo makubwa ambayo watu huwa wanadhani kwamba, Rais anapokuwa madarakani, kwa mfano tunapomaliza bajeti mwezi wa Sita, watu wanadhani fedha huwa zinabaki kwenye akaunti za benki, zipo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawajui kwamba, fedha tunazikusanya, tunazitafuta. Mfano katika kipindi hiki cha Bunge la Bajeti, tunapanga mipango ya maendeleo ya miaka mingine mitano au kwa kutegemeza kwa bajeti ya mwaka mmoja mmoja. Katika utafutaji wa fedha, huwa tunazitafuta kutokana na makusanyo, kwa mfano, tulikuwa na bajeti ya shilingi trilioni 50 ambayo tunaenda kuikamilisha mwezi huu wa Sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa na hii bajeti, tunakuwa na fedha ambazo nyingine tunazikusanya kutokana na mapato yetu ya ndani. Tumejiwekea kukusanya shilingi trilioni 39 point something, lakini tunakuwa na deficit ya bajeti ambayo fedha hizi nyingine tunakopa kutoka katika Mataifa mengine mbalimbali, kutoka kwenye mashirika makubwa ya kifedha na pia, nyingine zinatoka kwa wahisani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba, hatuna fedha ambazo zinakuwepo tu, maana yake, kuna fedha tunazitafuta kupitia kukusanya kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanasema tunadaiwa shilingi trilioni 97. Ni kweli, tunadaiwa shilingi trilioni 97, lakini tumedaiwa kuanzia lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni fedha ambazo ni za mwendelezo kuanzia Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni madeni ya Awamu ya Pili ya Mwalimu Ally Hassan Mwinyi, madeni ya mwendelezo ya Mheshimiwa Mkapa, madeni ya mwendelezo ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ni madeni ya mwendelezo ya Dkt. John Pombe Magufuli na hivyo hivyo ni madeni ya mwendelezo katika Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ni madeni ambayo tumeanzia chini mpaka leo kufikia deni la shilingi trilioni 97.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili deni ukilinganisha na Mataifa mengine, mfano katika Taifa la Kenya jirani zetu, ambao wao uchumi wao ni mkubwa, tunakwenda, tunawakimbiza, tunawafuata, wao wana deni la zaidi ya shilingi trilioni 200. Sisi ni shilingi trilioni 97, kumbe bado sisi ni Taifa himilivu na tuna uwezo wa kukopa. Serikali kopeni tutekeleze miradi ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi tunazokopa, hatukopi kwa ajili ya kuja kulipana mishahara. Fedha hizi tunazokopa zinaenda kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Tumeona wakati ujenzi wa reli ya SGR unaanza, Dkt. Magufuli alitafuta fedha, ni fedha hizo hizo za mikopo tumeanza kujenga kutoka Dar es Salaam tukaja mpaka Morogoro na nyingine zikajengwa kutoka Morogoro kuja Dodoma. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati anaingia hakukuwa na fedha za kujenga treni, kwanza kumalizia, lakini pia kuanzisha route nyingine, kwa maana ya kutoka Mwanza – Isaka, Isaka – Tabora, Tabora – Makutopora na pia, Tabora – Kigoma. Fedha hazikuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutafuta fedha kwa ajili ya kuwekeza, na leo tumeona treni ya umeme kutoka Mwanza – Isaka imeshafikia hatua ya 62%. Pongezi nyingi sana, kazi ni nzuri na tunaendelea kuiunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunasema, kwa sababu tunaruhusiwa kuendelea kukopa, tukope tukamilishe hii miradi na fedha tunazokusanya tunaenda, tunalipa madeni kidogo kidogo mpaka hata miaka 20, miaka 30, Taifa letu ni himilivu na linaweza kulipa haya madeni. Mtu ambaye hawezi kulipa madeni hawezi kukopesheka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kazi zote nzuri. Tumeona mradi mkubwa wa Bwawa la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere la megawatt 2,115 limekamika. Hongera sana Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri iliyofanyika. Hili taifa lilikuwa na uhaba wa umeme, tuna upungufu, tulikuwa tunazalisha umeme kwa megawatt 1,700, lakini bado tulikuwa na upotevu, tulikuwa tunaweza kupeleka kwenye mfumo wa grid ya umeme 1,400.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyozungumza, tumezalisha umeme zaidi ya megawatt 4,000. Kwa kweli, ni hatua kubwa, tunaipongeza sana Serikali na tunajua kwamba, kazi zote hizi ni kuhakikisha tunamkwamua Mtanzania, kumwondoa katika kiza, kumpeleka katika maendeleo. Tumeona katika maeneo yetu leo nchi nzima hakuna kijiji ambacho hakina umeme. Hii kazi ni nzuri, hongereni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema kwa nini mnapongeza nyie Wabunge wa CCM? Sasa kama kazi inafanyika, kwa nini tusipongeze?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anapofanya kazi vizuri, ni lazima apongezwe. Tuna vitongoji 66,000 nchi nzima, leo vitongoji vilivyopelekewa umeme ni 33,000, tumebakiza vitongoji 33,000. Hii ndiyo kazi ambayo sisi Wabunge wa CCM tunaishauri Serikali itafute fedha, iwekeze ili wananchi wetu waweze kupata umeme katika maeneo yote. Serikali kopeni fedha zije zipeleke umeme katika vitongoji vyote ili nchi nzima iweze kuenea umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko tunaona mabadiliko makubwa sana kwenye vijiji vyetu. Vijiji ambavyo vilikuwa havina umeme, vikipata umeme tunaanza kuona maendeleo. Pale kwenye eneo lile la Kijiji, watu walikuwa wanalala saa mbili, leo wanalala mpaka saa saba usiku.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa Taarifa mzungumzaji. Pamoja na mchango mzuri, pale kwenye Jimbo la Kibiti kuna vitongoji na kuna vijiji vipo visiwani kabisa. Tangu uhuru walikuwa hawategemei na hatukutegemea kupata umeme. Leo ninavyozungumza, shilingi bilioni 3.8 imekwenda, na umeme kule uko pukapuka.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Gulamali, unaipokea Taarifa.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa. Imenikumbusha hata jimboni kwangu nilipewa na Serikali hii ya Dkt. Samia Suluhu Hassan shilingi bilioni 15 kupeleka umeme kwenye vijiji vyangu vyote jimbo zima na sasa umeme unawake. Kwa nini nisipongeze?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge wa Chama cha Mapinduzi, napongeza na kuwatia moyo kwamba, chapeni kazi, Watanzania wamewaelewa, watu wa Manonga wamewaelewa. Hata jimboni kwangu tunasema, Mama Samia mitano na hata mimi mwenyewe, Gulamali, mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukwambia, ndani ya jimbo letu tulikuwa na shida kubwa sana ya maji. Hii Serikali imetupa fedha za kupeleka maji kwenye vijiji vyetu, kati ya kata 19, kata 16 tunakwenda kutumia maji ya Ziwa Viktoria. Kwa nini nisipongeze hii kazi nzuri ya Chama cha Mapinduzi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaambia Watanzania na Wana-Manonga wanajua kwamba, tunakwenda kwenye uchaguzi mwaka huu 2025, watapata kura za kujaa nyingi. Hata haya maneno wanasema kwamba, No Reform No sijui nini, hakuna kitu kama hicho ndani ya Jimbo letu la Manonga; hakuna kitu kama hicho ndani ya Wilaya yetu ya Igunga. Mwaka huu uchaguzi utafanyika na utakuwa wa amani na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu na watu wako wote kwenye ofisi yako na Mawaziri wanaokusaidia tunawatia moyo, chapeni kazi, tembeeni kifua mbele, mjiamini, Watanzania wanawaunga mkono, msisikilize hizi kelele. Tunasema, kelele za chura hazimzuii ng’ombe kunywa maji. Kwa hiyo, ninyi chapeni kazi, sisi tupo, jeshi lenu lipo, na wananchi wanawaamini kwamba kazi inaonekana.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Gulamali ahsante sana. Muda wako umeisha.
MHE. SEIF K. A. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nilikuwa na mengi, lakini kwa sababu muda siyo rafiki, naipongeza na kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)