Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sumve
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na uzima na kutufanya tukutane leo kuzungumza maendeleo ya nchi yetu na kupitisha bajeti kwa ajili ya ofisi muhimu kabisa ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba nitumie fursa hii kwa ruhusa yako kabla sijasahau, maana nimeona mambo yapo vizuri, niunge mkono bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ndipo niendelee kushauri na kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo amewasilisha, lakini kwa mambo ambayo yamewasilishwa kwenye hotuba yake ya bajeti ya ofisi yake. Mheshimiwa Waziri Mkuu hongera sana na umetutendea vyema Watanzania na umelitendea vyema Bunge hili la Kumi na Mbili.
Mheshimiwa Mweyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu anao wasaidizi ofisini kwake wakiongozwa na Waheshimiwa Mawaziri; Mheshimiwa Lukuvi, Mheshimiwa Ridhiwani; Waheshimiwa Manaibu; mdogo wangu Mheshimiwa Katambi na Mheshimiwa Ummy, wanamsaidia vizuri; nao hongera zao ziwafikie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niseme maneno machache ambayo ninaamini hata Mwenyezi Mungu yanayo baraka yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, tumemshukuru kwa uhai lakini Mwenyezi Mungu mimi ninamshukuru sana kwa nchi hii inayoitwa Tanzania. Mwenyezi Mungu ametujalia Taifa imara, lenye utulivu, lenye amani na lenye mshikamano. Nchi yetu bado ipo imara na tumekuwa mfano mzuri kwa dunia na nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Tanzania ipo hivi kwa sababu Watanzania wenyewe waliamua iwe hivi. Watanzania kwa utashi wao na kwa uelewa wao wamendelea kwa muda mrefu kukiamini na kukipa kura nyingi na ushindi Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama cha Mapinduzi kimekuwa ni msingi wa uimara wa nchi yetu. Nawe na Watanzania wote ni mashahidi, Chama Cha Mapinduzi kimepita katika mapito mbalimbali kikiwa imara na mshikamano na kuweka mbele Utaifa. Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikibadilisha viongozi wake. Leo tunaye Mheshimiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ambaye ni wa sita chama kikiwa imara bila mgawanyiko na bila vurugu yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi, kuna baadhi ya vyama vikitaka tu kubadilisha viongozi, mwisho wa siku hawamalizi vizuri. Kwa hiyo, Watanzania sio wajinga kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi. Mimi nawashukuru sana, wamekuwa wakitumia upeo wao, uwezo wao na baraka za Kimungu kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi. Naamini bado wanaendelea kukiamini, na mwaka huu watakipa ushindi wa kishindo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama hiki Cha Mapinduzi tangu mwaka 2020, leo ni 2025 tumekuwa na Ilani yetu, tumeitekeleza kwa kiwango kikubwa, na hii ni bajeti ya mwisho kwenye Ilani ya 2025. Nasimama mbele ya Bunge lako kama shuhuda. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye bajeti yake tunaijadili leo ndiye aliyekuja Sumve mwaka 2020 akaniombea kura kwa wananchi wa Sumve.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu mwenyewe ni shahidi, wakati anakuja Sumve wananchi walisema wana shida ya maji, walisema wana shida ya umeme, walisema wana upungufu wa vyumba vya madarasa, upungufu wa zahanati na vituo vya afya. Tunavyozungumza leo, wakati mimi naomba kura kwa watu wa Sumve, Serikali hii ya Awamu ya Sita iliyorithi kwenye Serikali ya Awamu ya Tano, wakati inaingia watu wa Sumve walikuwa wana vituo vya afya viwili, lakini leo tunavyozungumza, vimejengwa vituo vya afya vipya vitatu. Ina maana sasa vipo vitano. Katika muda wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wa miaka minne amejenga vinne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo tunavyozungumza, vijiji vya Sumve vipo 60, vijiji vilivyokuwa na umeme vilikuwa ni 18, leo tunavyozungumza vijiji vyote vina umeme. Hili ni ongezeko la vijiji 42. Kazi ya heshima kubwa sana imefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumza leo, barabara za Jimbo la Sumve zinapitika vizuri. Sumve haikuwa na maji ya Ziwa Victoria, lakini tunavyozungumza leo, zaidi ya shilingi bilioni 67 zimepelekwa Sumve ili kuleta maji ya Ziwa Victoria na kazi inaendelea. Kwa hiyo, tunajivuna. Tunasimama hapa kusema kwamba tumefanya kazi kubwa ya heshima, tunampongeza Mheshimiwa Rais. Kwa niaba ya watu wa Sumve, tunamwahidi kwamba kura zitajaa, zitakuwa za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri kidogo. Kwenye Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuna jambo ambalo nafikiri tunatakiwa tuongeze kasi. Suala la ajira limekuwa bado na changamoto kwa vijana wetu. Vijana wanamaliza vyuo vikuu wanatafuta kazi, na Serikali kwa kweli imejitahidi kutoa nafasi za ajira kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto ya vijana wanaoomba kazi kuwa na imani ya mfumo wa ajira Serikalini. Kwa hiyo, naomba kuishauri kwenye Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali kwamba tunayo kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa mfumo wa kuajiri vijana Serikalini unaaminika na umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani sote ni mashahidi, zinapotokea nafasi za ajira Serikalini simu zetu Waheshimiwa Wabunge zinajaa message, kila mtu anataka tumsaidie kupata kazi. Hii ina maana kwamba wale wanaoomba kazi wanaamini kwamba kazi hizi zinapatikana kwa kusaidiwa na siyo kwa kuwa na sifa. Hawa watu hawawezi kufanya mambo haya kwa bahati mbaya, nadhani lipo jambo la kuangalia kwenye mfumo wa ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi zetu zinazosimamia ajira, tuangalie namna bora ya kuhakikisha Watanzania wanaamini ule mfumo, na ule mfumo uwe rafiki ili kila mmoja aweze kuuamini. Ninadhani wote mmeona, juzi TRA wametangaza nafasi, kila mmoja hana imani. Kwa hiyo, hii ni changamoto, lakini ninaamini Serikali ya CCM ni sikivu na sisi Waheshimiwa Wabunge wa CCM tutaendelea kuishauri vizuri Serikali yetu ili kuhakikisha kwamba changamoto zinazowazunguka Watanzania zinatatuliwa na tunaendelea kuaminika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo siri kwamba CCM bado inaaminika, CCM bado ni kimbilio la Watanzania, CCM bado ndicho chama chenye nguvu na kinachoweza kuwasaidia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naomba niishie hapo. Kwa kuwa nilishaunga mkono hoja, sasa nitoe nafasi kwa watu wengine. Ahsante sana. (Makofi)