Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Maimuna Salum Mtanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili nami nichangie machache kuhusiana na bajeti iliyopo mbele yetu, bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya, pia nawashukuru na niendelee kumwombea sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania afya njema kwa sababu ni mkombozi wetu, analeta ustawi katika maendeleo yetu na sisi tunayaona. Kipekee, namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na timu yake yote kwa hotuba nzuri ambayo ameiwasilisha mbele yetu hapo jana. Hongereni sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri ambayo mnaendelea kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia, nianze na Jimbo la Newala Vijijini kwa kifupi sana. Sisi Wananewala Vijijini tulihamia kule jimboni tukawa hatuna jengo la utawala, hatuna Hospitali ya Halmashauri, hatuna shule nzuri na bora na mambo mengi; lakini kupitia uongozi mzuri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake wote, hapa tunapoongea, tuna jengo la halmashari, tuna Hospitali ya Wilaya na kwamba umeme vijiji vyote sasa tumeshapata. Tulikuwa hatuna hata barabara ya lami pale mjini, sasa tunazo barabara za lami. Tunaishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niongee kidogo kuhusiana na barabara yetu ya Kibiti – Lindi ambayo tarehe sita ya mwezi huu wa Nne ilipata changamoto ya mawasiliano kukatika. Naishukuru sana Serikali, kwa msimamzi wa Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na timu yake, msaidizi wake Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ameshinda kule, amekesha kule na ilipofika tarehe nane mawasiliano yakaanza kufunguka. Hapa tunapoongea, watu sasa wanapita. Tunaishukuru sana Serikali kwa kuona haja ya kunusuru wananchi wa kusini kwa sababu maisha yao yalikuwa hatarini sana kwa kukosa yale mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ya kushauri kuhusiana na ile barabara kwa sababu mwaka 2024 ilijitokeza na sasa imejitokeza tena. Naomba Kiti chako, ili nishauri machache. La kwanza, ambalo nataka kushauri ni kuongeza usimamizi kwa wakandarasi ambao wamepewa kazi katika madaraja yale ambayo yalibomoka mwaka 2024. Tusipoongeza usimamizi wa karibu, inaweza yakatukuta haya yaliyotukuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee katika hili, namshukuru M-NEC wa Mkoa wa Mtwara, ndugu yangu Makapo kupitia Makapo Contraction. Yeye hakusubiri asimamiwe, alikuwa anafanya kazi muda wote, na eneo lake kwa kweli linaonekana. Kwa hiyo, nampongeza sana M-NEC. Nawaomba na wengine ambao wamepata kazi katika madaraja yale, waongeze nguvu, wasisubiri kusimamiwa ndipo wafanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ambao nilitaka niutoe ni kwamba, mwaka 2023 niliiomba Serikali itujengee meli katika Bahari ya Hindi. Niendelee kuuomba mpango ule kwa sababu niliambiwa kwamba meli itajengwa, itawekwa kwenye mpango. Niendelee kuiomba Serikali yangu sikivu iweke kwenye mpango wake ujenzi wa meli katika Bahari ya Hindi, meli ambayo inapotokea changamoto yoyote itasaidia kusafirisha abiria, pia itasafirisha na bidhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Visiwa vya Komoro wanategemea sana nchi ya Tanzania kupata huduma zao. Kwa hiyo, meli ya uhakika ikiwepo itawasaidia wananchi wa Komoro kupata bidhaa kwa urahisi na vilevile wananchi ambao wapo kando kando ya Bahari ya Hindi nao watapata fursa ya kufanya biashara zao ili ziweze kwenda kwa urahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nilitaka kushauri ni kwamba kwa barabara hii imechoka sana, ina viraka vingi. Naishauri Serikali iweke kwenye mpango ili na yenyewe iweze kujengwa barabara yote badala ya vipande vipande au kuziba viraka viraka kama ilivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nilitaka kushauri kuhisiana na barabara ni kuhusu wale wakandarasi ambao wamepewa kazi kuimarisha michepuko ile ambapo wakati wanatengeneza Barabara, watu pamoja na magari ya abiria pamoja na mizigo yanapita kwenye diversions waziimarishe zile diversions ili wananchi waweze kupita kwa uhakika wakati kazi ya ujenzi inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyingine ambayo inahusiana na barabara, naiomba Serikali, Barabara ya Mtama – Kitangali – Newala kilomita 74 upembuzi yakinifu umeshafanyika, Serikali iweke kwenye mpango sasa wa kujenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu Barabara ya Mnivata – Tandahimba, Newala – Masasi. Naomba kipande cha Mnivata – Tandahimba, kile kipande mkandarasi aongeze kasi kidogo ili iendane na muda. Mvua zilivyonyesha magari mengi sana yalikwama, lakini kama ataongeza kasi, basi huu mkwamo ambao umejitokeza kipindi hiki unaweza kuondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine linalohusiana na barabara ni barabara za TARURA. Tunatambua kwamba mwaka 2024 mvua nyingi zilinyesha na barabara nyingi ziliharibika na kuvunjika. Hata katika jimbo langu barabara nyingi sana zimevunjika. Kwa mfano, Mkoma II kwenda Chimemena, haipitiki kabisa; Mulunga kwenda Nandwahi imeharibika haipitiki; na Mtopwa kwenda Chilondolo imeharibika vibaya. Naomba wenzetu wa TAMISEMI watafute namna ambavyo watakuja kukarabati barabara zile ambazo ziliharibiwa na mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye kilimo; nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na timu yake. Kwa kweli kwenye zao la korosho wametuheshimisha sana na wameliheshimisha Taifa kwa sababu uzalishaji kwa msimu wa 2024/2025 umeongezeka sana, na kuongezeka huku siyo kwamba kumekuja kwa bahati mbaya, hapana. Serikali ilileta pembejeo za kutosha ambazo wananchi walizitumia katika mashamba yao, jambo ambalo limeongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nitoe tu mfano kidogo kwa msimu wa mwaka 2023/2024. Tunacho Chama Kikuu cha TANEKU kinachohudumia Newala na Tandahimba, na ongezeko la uzalishaji ni 67.6%, lakini ukienda Bodi ya Korosho yenyewe, kwa ujumla wa Tanzania yote, ongezeko la uzalishaji kwa mwaka 2024/2025 ni 70%. Hili ni ongezeko kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunapoongea leo, tayari mbolea ya Sulphur imeshateremka Mtwara, kinachosubiriwa ni usambazaji ambao utaanza tarehe 15 ya mwezi huu. Kwa hiyo, zile changamoto katika usimamizi wa ugawaji ambazo zilijitokeza kwa msimu uliopita, nishauri wenzetu wanaosimamia usambazaji wa pembejeo zile, basi wasimamie vizuri kwa ukaribu ili zile changamoto zipate tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, hapo kwenye korosho, niwapongeze TANEKU Limited kwa sababu wamejenga kiwanda cha kwanza cha ushirika nchini. Tunawapongeza sana, kwani ni kiwanda ambacho kimeshakamilika, kimeanza kuzalisha ajira kwa wananchi wanaotoka maeneo jirani, kwa maana ya kwamba kimeanza kufanya kazi. Tunaipongeza sana TANEKU, wameanza utaratibu wa kujenga kiwanda kingine pale Tandahimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri tu Serikali, tuendelee kuwaunga mkono, watatuvusha kwa kiasi kikubwa sana. Katika hili, pia naishukuru Serikali kwa kutenga eneo la kongani ya viwanda vitakavyohudumia korosho katika Mkoa wa Mtwara pale Nanyamba. Tunawashukuru sana kwa sababu kongani hii itakuwa mkombozi badala ya kuuza korosho ghafi, basi tutauza korosho, karanga na matunda ambayo yanatokana na korosho tutayapata kwa namna mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naipongeza sana Serikali, na kwa kweli Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi, na anaumiza kichwa kwa ajili yetu. Sisi sote tumuunge mkono, ndiyo zawadi pekee ambayo tunaweza kumlipa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali yake yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanakusini tunaendelea kumshukuru kwa sababu hata mazao ya ufuta na mbaazi na yenyewe bei ilikuwa nzuri kiasi kwamba iliwakwamua wananchi kutoka kwenye ile hali ambayo ilikuwepo na kwenda kwenye hali ambayo unafuu wa maisha ulipatikana kutokana na ziara ambazo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akizifanya katika nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziara hizo ndizo zilipelekea kuwapata wanunuzi wa mazao haya kwa urahisi kiasi kwamba bei ikaongezeka tofauti na ilivyokuwa kule nyuma. Sisi Wanamtwara na Wanaruvuma ambao na wenyewe wanalima korosho pamoja na ufuta, tunamshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuongelea ni suala la maji...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtanda, muda wako umekwisha, ninaomba uhitimishe.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, yalikuwa mengi kwa sababu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametukwamua kwenye maji, shilingi bilioni 84.7 haijawahi kutolewa. Ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye ambaye ameleta kwenye mradi mkubwa wa Makonde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)