Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ambayo iko chini ya Waziri Mkuu pamoja na Wizara nyingine ambazo ziko chini yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kutulinda na kutujalia afya njema hatimaye tumefika mwaka wa tano wa uhai wa Bunge hili toka tulivyochaguliwa mwaka 2020 na tunaamini kwa msaada wa Mungu tutarejea kwa sababu ni mpango wake na mapenzi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Tunamwona jinsi anavyohangaika kwenda wilayani na mikoani kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Namshukuru sana Waziri kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu kwa kazi kubwa anayoifanya pamoja na wasaidizi wake wote na watendaji wote. Kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wajumbe wa Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI, tumekuwa tukifanya ziara mbalimbali mikoani na kwenye wilaya kufuatilia, kusimamia na kuangalia ni kwa kiasi gani fedha ambazo Bunge hili lilizipitisha, zinafanya kazi. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana, yeye pamoja na Wizara yote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa kipindi cha miaka mitano ambayo nimekuwa hapa Bungeni, namshukuru Mwenyezi Mungu nimeweza kuhudumu kwenye Kamati ya UKIMWI, na sasa hivi Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa fedha za ndani, kulikuwa na changamoto kubwa sana ya utoaji wa fedha hasa kwenye masuala mazima ya fedha za maendeleo, lakini kwa miaka hii minne nikiangalia mtiririko wa utoaji wa fedha, kumekuwa na mabadiliko makubwa sana. Hadi kufikia Februari 2025, Tume ya Kudhibiti UKIMWI imepokea zaidi ya 73% ya fedha ambazo Bunge lako Tukufu lilizipitisha. Hayo ni matumizi ya kawaida, lakini kwenye matumizi ya miradi ya maendeleo, imepokea zaidi ya asilimia saba. Haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu ya nini? Ni kwa sababu Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan ina dhamira safi ya kuhakikisha kwamba mapambano dhidi ya virusi vya UKIMWI yanapiganwa kisawasawa. Kwa mara ya kwanza, ukiangalia ulinganisho wa bajeti kwa mwaka 2024/2025 na 2025/2026 utaona kabisa kwenye fedha za ndani za maendeleo fedha zilikuwa kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukipiga kelele tukisema kwamba tuna Mfuko wa Kudhamini Mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI (ATF) ulikuwa ukipata fedha kidogo, ni shilingi milioni 500, bajeti inayomalizika ikatengwa shilingi bilioni 1.8; lakini kwa mwaka huu wa fedha Serikali imetenga shilingi bilioni 5.28 zaidi ya 180%. Haijawahi kutokea. Hii yote ni dhamira safi ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI yanapiganwa kiukamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tuliweza kuona nchi mbalimbali na hasa nchi ambazo zilikuwa zinatufadhili sisi kama Watanzania kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ya kupambana na Virusi vya UKIMWI pamoja na miradi mingine. Wananchi walipata hofu, walipata simanzi, kila mtu alikuwa na mashaka; itakuwaje? Kwa sababu misaada mingi inatoka nje, lakini kwa bajeti hii ambayo Serikali imeileta, na kwa maelezo ambayo Serikali imekuwa ikiyatoa, na kwa kuonesha kabisa dhamira ya kusimama, sisi kama Watanzania kuweza kuboresha mfuko wetu wa udhamini kutoka shilingi bilioni 1.8 mpaka shilingi bilioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wajumbe wa Kamati tunaona kwamba ni jitihada kubwa ambayo imeshafanyika. Japo, tunaona kwamba bado kuna uhitaji wa kuendelea kutafuta vyanzo vingine vya fedha za ndani kwa kushirikisha wadau wa ndani ili sasa mfuko wetu uwe endelevu na uweze kustahimili kuweza kupambana na Virusi vya UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yamefanyika, pamoja na afua ambazo zimefanyika na pamoja na mipango mizuri ambayo Serikali inayo, tunaona katika utafiti uliyofanyika mwaka 2022/2023 bado kuna changamoto ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. Watanzania tusibweteke, UKIMWI bado upo, na kila mwaka Watanzania 60,000 wanapata maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, na katika hao 60,000 wanaopata maambukizi ya Virusi vya UKIMWI 34.4% ni vijana wadogo, na ni ambao ni nguvu kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatuambia nini? Hii inatukumbusha kwamba bado tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha kwamba vijana wetu wanaendelea kupata elimu, lakini suala zima la kuhamasisha upimaji wa VVU unafanywa kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika huo utafiti kwenye suala zima la upimaji, bado tuna 82.7% tu, ina maana kuna wananchi wengine wengi ambao bado hawaelewi afya zao mpaka sasa. Pamoja na afua zote zinazofanyika, bado kuna wananchi hawajajua status zao, ni 82.7%; lakini katika wale 82.7% ambao wameshajua kwamba wana maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, tunaishukuru sana Serikali yetu kwa kuhakikisha kwamba 97% wamepatiwa dawa za kuweza kufubaza Virusi vya UKIMWI; na katika wale ambao wameshagundulika, 94% tayari wameshafubaza Virusi vya UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwetu sisi hiyo ni hatua kubwa sana ambayo kama sekta tumeweza kuipiga. Kwa hiyo, kinachotakiwa sasa ni kuendelea kuhamasisha wananchi kuendelea kupima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, akina baba wengi hawapimi. Usijidanganye kwamba mke wako akipima, akaonekana yuko salama na wewe upo salama kwa sababu, kila mtu ana modality yake ya kupata maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. Inawezekana mke wako yuko salama kwa sababu kinga yake iko imara, lakini wewe baba ukawa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa kinara wa kuhamasisha upimaji wa Virusi vya UKIMWI. Kwa hiyo, Watanzania tujitokeze, tuendelee kupambana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza hapa mambo makubwa ambayo yamefanywa na Serikali ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan. Mwenye macho haambiwi tazama. Ukienda sekta ya afya hakuna kijiji ambacho hakijafikiwa, ukienda sekta ya maji, elimu na miundombinu; mwaka uliopita kulikuwa na Mvua za El-Nino, kila Mbunge hapa alikuwa analalamika, kila mwananchi alikuwa analalamika kwamba jamani, miundombinu imekuwa mibovu, lakini kutokana na juhudi za Serikali ya Mama Samia, miundombinu mingi iliweza kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata jana tumeshuhudia kule kusini barabara imekatika, lakini ndani ya masaa machache, barabara ile iliweza kupitika. Kwa hiyo, hizi ni juhudi kubwa ambazo zinafanywa na Serikali ya Mama Samia. Kwa hiyo, sisi kama Watanzania, sisi kama wananchi, sisi kama wanawake wa Tanzania, tutakuwa bega kwa bega kuhakikisha kwamba Mama Samia Suluhu Hassan na Serikali yote, Oktoba, 2025 inashinda kwa kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri, wamekuwa wasikivu, wachapakazi, hawalali; leo tunawaona Mashariki, kesho Magharibi, keshokutwa Kusini na Kaskazini, wanafanya kazi, wanatekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto waliozaliwa Shinyanga mwaka 2000 walikuwa wameusahau Uwanja wa Ndege Ibadakuli, lakini sasa hivi tunavyoongea, uwanja ule umeshakamilika zaidi ya 100%. Ni masuala machache ambayo yamebaki kwa ajili ya kukamilisha ili wale watoto wa mwaka 2000 waone kwamba kumbe Shinyanga kulikuwa na uwanja wa ndege mzuri ambao ndege kubwa zinaweza zikatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yamefanyika. Halmashauri ya Manispaa ya Kahama ni mji ambao unakua sana, miundombinu haikuwa mizuri kabisa, barabara zilikuwa hazipitiki, ukienda Kata ya Majengo, ukienda Mungula, ukienda Malunga kulikuwa na barabara ambazo siyo rafiki na zilikuwa kero kwa wananchi, lakini sasa hivi ninavyoongea wakandarasi wako site wanatengeneza barabara kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Shinyanga Manispaa wakandarasi wameshasaini mikataba, wanatengeneza miradi yote ya TACTIC ambayo imeidhinishwa. Tufanye nini sasa? Tuseme nini sasa? Ni lazima sisi kama Watanzania tuunge mkono juhudi za Mama Samia Suluhu Hassan, tumtie moyo na tumwambie kwamba akanyage mafuta, tena akanyage mafuta kwenye mteremko kabisa, asiachie. Wale wanaozira, wanaokataa, lakini sisi tunajua mwezi wa Kumi tuna Uchaguzi utafanyika, na Chama cha Mapinduzi kinakwenda kushinda kwa kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, Mungu ibariki Tanzania. (Makofi)