Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ili nichangie katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya njema na kutuwezesha kufika siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nitumie nafasi hii kumshukuru sana, sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hekima, kwa umakini, kwa ujasiri na uwezo mkubwa ambao ameuonesha katika kuiongoza nchi yetu. Nampongeza sana, sana, sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza kwa sababu amekuwa na uwezo mkubwa sana wa kutafuta rasilimali, kutafuta fedha; amekuwa na uwezo mkubwa sana wa kupeleka miradi karibu kila jimbo, kila kata na kila kijiji. Amepeleka miradi mingi sana yenye manufaa kwa nchi yetu. Kwa hiyo, tunampa hongera kwa kazi nzuri ambayo ameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na taasisi zake zote zilizoko chini ya ofisi yake kwa kazi nzuri ambayo taasisi hizo na Mheshimiwa Waziri Mkuu umefanya, kwanza katika kusimamia Serikali yetu, lakini la pili katika kuratibu majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali, na tatu kwa hotuba nzuri iliyosheheni taarifa, takwimu, maarifa mengi na mambo mengi ambayo yapo katika hotuba yako. Tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Timu yako kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa sababu imetekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa zaidi ya 100%. Kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025 tulibainisha baadhi ya mambo ambayo yalionekana ni changanmoto katika maendeleo ya Taifa letu. Moja ya changamoto zilizobainishwa ni pamoja na umaskini wa baadhi ya Watanzania, ambapo tuliona karibu 26% ya Watanzania, ambao ni robo, bado walikuwa katika umaskini mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tulibainisha changamoto ya ajira katika nchi yetu, tukabainisha uwezo mdogo katika kuongeza thamani ya mazao yetu katika maeneo mbalimbali; na tukabainisha uzalishaji duni na zana duni za uzalishaji na mambo mengine ambayo yapo katika ujenzi wa uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi ninapenda nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita. Katika suala la ajira, kutokana na kuona hizi changamoto, tuliweka lengo kwenye ilani, tukasema kwamba tunataka tuhakikishe katika kipindi hiki tutengeneze ajira zisizopungua milioni nane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, takwimu zilionesha kuwa ajira zilizotengenezwa ni zaidi ya milioni nane kwenye upande huo. Kwa hiyo, hii ni kazi nzuri imefanyika, ndiyo maana ilani imetekelezwa kwa zaidi ya 100%, zaidi ya ajira milioni nane zimetekelezwa. Kutekelezwa kwa ajira hizo na miradi mbalimbali, maana yake umaskini wa Watanzania unazidi kupungua, kwa sababu uwekezaji mkubwa ndiyo unaosaidia katika kutanzua tatizo hili la umaskini katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sanjari na hilo, Serikali ya Awamu ya Sita iliweka mkazo katika kuimarisha maslahi ya watumishi wa umma, na tumeona jitihada mbalimbali ambazo zimechukuliwa na Serikali katika kuhakikisha inaboresha maslahi ya watumishi wa umma. Kwa kweli kazi nzuri imefanyika, tumeona madaraja ya baadhi ya watumishi yanapanda, nyongeza zinajitokeza na mambo mengine mazuri ambapo fedha hizi zikipatikana ndiyo zinaenda kuwekezwa katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeona pia Ofisi ya Waziri Mkuu ikishughulikia masuala ya maslahi ya wafanyakazi katika sekta binafsi. Sekta binafsi, sekta mbalimbali zilionekana kwamba zina maslahi duni. Hata hivyo, Serikali imeshughulikia na inaendelea kushughulikia, lakini bado kuna changamoto kwamba, wafanyakazi wengi wanaofanya katika sekta binafsi bado masilahi yao ni duni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tunaamini Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kwamba inaboresha hayo maeneo na sekta binafsi inaimarika ili iweze kuwa ndiyo muhimili wa ujenzi wa Taifa letu na itoe ajira mbalimbali kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kutekeleza majukumu yote haya na katika kutanzua tatizo la ajira, ni wazi kabisa hii changamoto bado ni kubwa. Pamoja na kazi nzuri ambayo imefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, bado ukienda mitaani kuna vijana wengi bado wanahangaika kutafuta ajira. Pia, hii inatupatia nafasi kwamba, sasa kuna haja ya kukaa chini na kuitafakari na kuona namna ya kuongeza mikakati zaidi ili kusudi tuweze kutatua tatizo la ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi utaona vijana wengi sana wanahangaika. Ikitangazwa ajira, wanaoomba ni wengi kupitiliza. Wanaohangaika huko mitaani ni wengi. Sasa, maana yake ni lazima tuongeze mkakati wa kuimarisha sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya umma peke yake haitaweza kutatua hili tatizo la ajira. Hata hivyo, tumeona Serikali ya Awamu ya Sita imetoa ajira nyingi sana kwenye Mashirika, Wakala, lakini tumeona pia imeajiri watu wengi sana. Walimu wameajiriwa, watu wa afya wameajiriwa, lakini bado kuna sekta nyingine zinatakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu. Baada ya kuliona hili tatizo, wameanzisha utaratibu wa kuhakikisha vijana wanaohitimu katika vyuo vikuu na vyuo vingine, waende katika Vyuo vya VETA ili waweze kupata maarifa ya kuweza kujiajiri. Hii hatua ni nzuri sana katika kuleta maendeleo. Kwa hili, tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, tumuunge mkono kwa kuwahamasisha vijana wetu waende kwenye vyuo vya VETA wakapate maarifa ili waweze kuchangia katika ujenzi wa Taifa letu. Hii ni hatua madhubuti ya kukabiliana na changamoto ya ajira hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeona katika Jimbo letu la Vwawa na katika Wilaya yetu ya Mbozi, tulikuwa na changamoto nyingi. Ni mkoa wa mwisho kuanzishwa katika utaratibu wa uanzishwaji wa mikoa. Tumeanzisha Mkoa wa Songwe, lakini tulikuwa hatuna vyuo vyovyote vinavyoweza kuwasaidia kuwapa maarifa, elimu na ujuzi vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Serikali ya Awamu ya Sita imeanza ujenzi wa vyuo katika Mkoa wa Songwe. Chuo cha VETA kinajengwa, Chuo cha Walemavu kinajengwa, kwa kweli tunawapongeza sana. Pale Wilaya ya Mbozi kwenye eneo la Sasanda, kulikuwa na kambi ya vijana ambayo ina ekari zaidi ya 700.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile kambi bado tunaweza tukaweka mkakati na ikatumika katika kuwaandaa vijana ili kuweza kushiriki katika uchumi wa nchi hii. Ekari 700 ni nyingi, zinaweza zikazalisha, zikaongeza na tunaweza tukajenga hata vyuo vingine pale, na vikaweza kuwaajiri hata vijana wengi ambao wanakosa maarifa na ujuzi wa kuyaendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaishukuru sana Serikali kwa ujenzi wa hivi vyuo. Hata hivyo, Chuo cha Afya najua kiko mbioni na wametutangazia kwamba kinakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo, tumeona miradi ya barabara mbalimbali zimejengwa. Tunaona barabara ya kutoka Njiapanda ya Iyula kwenda mpaka Idiwili kilometa 21 wanajenga wanawake wa Tanzania. Barabara imechaguliwa, na wanawake wa Tanzania ndiyo wanaokwenda kujenga ili kuwajengea uwezo kiuchumi. Ni hatua nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi zinapojengwa ndiyo zinafungua uchumi. Zinafanya kila mahali sasa paweze kufikika na mazao ya wananchi yaweze kwenda sokoni. Hapo ndipo uchumi unakuwa na ajira mbalimbali zinatengenezwa kwa wale wote wanaokwenda kufanya kazi. Kwa hiyo, hili ni jambo zuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona vituo vya afya vimefunguliwa na vimejengwa katika maeneo mengi. Pia, naipongeza Serikali imejenga vituo vya afya vizuri kwetu. Zaidi ya vituo vinne vimejengwa katika kipindi hiki. Sasa hivi tunapambana katika kuhakikisha tunapata watumishi wa kutosha, vifaa vya maabara na vifaatiba ili vituo vile viweze kutoa huduma zile ambazo tulikuwa tunazikusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kazi nzuri, na zote hizi ni ajira kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la ajira hapa nchini na kupunguza umasikini kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumeona miradi ya maji mingi ambayo imetekelezwa katika maeneo mbalimbali. Tumeona mradi wa maji wa kutoka Ilomba unakuja mpaka Vwawa, Mradi wa maji kutoka kule Momba unakwenda mpaka Tunduma, unakuja mpaka Vwawa hadi Mlowo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tumeona soko la mazao, stendi ya Mkoa na Maghala ya NFRA yanajengwa. Zote hizi ni jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kutanzua umasikini, kukabiliana na ajira, kujenga uchumi mpana na kutatua matatizo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kazi nzuri hii tunaunga mkono hoja na tutaendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita ili tuweze kupata ushindi mkubwa na ninahakikisha kabisa kwamba, mwaka 2025 ushindi ni mkubwa, Mungu atubariki na naunga mkono. Ahsanteni sana. (Makofi)