Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ushetu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninakushukuru sana. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kibali hiki cha kipekee kusimama kwenye Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kabla sijaendelea, nami naomba niunge mkono hoja ya bajeti ya Waziri Mkuu. Bajeti ni nzuri, lakini pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri iliyoelezea bajeti na mwelekeo thabiti wa Serikali yetu ya Awamu ya Sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, mama yetu, kwa kazi nzuri anayosaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa Jimbo langu la Ushetu, jimbo ambalo lina miradi mingi ya kimkakati. Kwa miaka minne ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ushetu peke yake tumepokea zaidi ya shilingi bilioni 196 ambazo zimekwenda kwenye miradi mikubwa ya kimkakati iliyoshindikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, Jumah Aweso, alifika Jimboni Ushetu na aliwaona akina mama walivyokuwa wanateseka na ndoo za maji, aliona akina mama walivyokuwa wanalia. Shida ya maji katika Jimbo la Ushetu ilikuwa ni kilio kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa maji wa Ziwa Victoria uliokuwa katika Mji wa Kahama kwa zaidi ya miaka 19, lakini umekuja kutibiwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Jumah Aweso, kwa kazi kubwa ambayo umeifanya, zaidi ya shilingi bilioni 44 ambazo zimekuja kwa wananchi wa Ushetu, Mkandarasi yuko site. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kazi anazozifanya za kuwapa wazawa, yaani kampuni za kitanzania ambazo zinafanya kazi vizuri sana. SIHOTECH Engineering Company Limited, ambayo inafanya kazi katika Mradi huu inafanya kazi usiku na mchana katika kuchimba mitaro, kufukia mabomba, mabomba yanatandazwa. Hivyo, ni kazi kubwa inayofanyika kwa wananchi wa Ushetu. Napongeza sana kwa kweli, kazi kubwa imefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kata 11, Vijiji 54 vinakwenda kupata mradi wa maji, ambapo chini ya ardhi ya vijiji hivi, vitongoji na kata zake hazikuwa na mradi. Ushetu ina kata 20, naomba tu awamu inayokuja sasa kata hizi na vijiji vyake vinavyobaki viweze kukumbukwa pia katika kufikishiwa maji katika Mradi huu wa Maji wa Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Kilimo, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, alikuwa kinara wa ushirika. Alizunguka katika nchi hii ya Tanzania kuhamasisha ushirika uweze kuanzishwa. Hata hivyo, baadaye akabadilishiwa jina akawa Baba wa Ushirika. Nami niendelee kumwambia, sasa ushirika umeimarika. Mwaka 2019 alipokuja pale Shinyanga, aliita vyama vya ushirika vyote na warajisi wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitoe shukrani za dhati sana kwake, alikuja kuigawa SHIRECU na akaagiza igawiwe SHIRECU na leo ikaenda kuzaliwa SIMCU (Chama Kikuu cha Ushirika Simiyu) ambapo kimekwenda kuwa chama bora na kupewa fedha na Benki ya Kilimo TADB zaidi ya shilingi 6,800,000,000/= na imenunua pamba safi kwa wakulima na kwa ushindani mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kahama, Cooperative Union, mwaka huu pia nayo iliweza kupewa shilingi bilioni sita (Chama Kikuu cha Ushirika ambacho pia kilitoka SHIRECU), nacho kimefanya kazi kubwa. Vilevile, kimeongezewa fedha nyingine na Benki ya Kilimo, shilingi bilioni mbili ambapo imekwenda kuanzisha oil mill ili kuongeza thamani ya mazao yetu kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, MBCU nayo imepewa shilingi bilioni 11.8. Vilevile, CCU – Chato nayo imepewa shilingi bilioni 8.9. Zaidi ya shilingi bilioni 39.6 zimetoka Benki ya Kilimo (Benki yetu inayohudumia wakulima) na zimepelekwa kuwahudumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukuomba, Benki yetu ya Kilimo imefanya kazi kubwa sana kwenye kuimarisha ushirika. Imevichukua hivi vyama vikiwa na hali mbaya, na leo vyama hivi vimekwenda kuimarika na vimefanya kazi vizuri sana. Niendelee kuomba benki hii iendelee kuongezewa fedha ili iendelee kuwahudumia wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, ndugu yangu Mheshimiwa Hussein Bashe, amefanya kazi kubwa sana kwenye sekta ya kilimo. Leo anakwenda kuanzisha Benki ya Taifa ya Kilimo ambayo inazinduliwa tarehe 28. Ni mkombozi mkubwa sana kwenye sekta ya kilimo na vyama vya ushirika. Niendelee kuomba Mheshimiwa Waziri, tuimarishe mifumo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa ushirika ambao umeanzishwa na unafanya kazi vizuri sana, mfumo wa MUVU, mfumo huu unakwenda kuleta mapinduzi makubwa sana kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa mfumo huu uingie mpaka kwenye vyama vyetu vya ushirika vya pamba ili mkulima anapopeleka pamba yake kwenye AMCOS, akipima tu ni moja kwa moja mpaka kwa mrajisi wa vyama vya ushirika Tanzania ili aweze kuona Mkulima wa Simiyu, Mkulima wa Kishapu, Mkulima wa Ushetu na mkulima wa maeneo mengine nchini ajue kwamba kwenye eneo la ushirika wameuza nini na wamepata kiasi gani? Hata ule wizi mdogo mdogo uliokuwa unasemwa hapo nyuma, tayari tutakuwa tumeshautibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, kwenye eneo la pembejeo na mbolea za ruzuku, amefanya kazi kubwa mno. Leo wakulima wa tumbaku ambao walikuwa hawajawahi kupata ruzuku, tayari hundi ya shilingi bilioni 13 imetolewa kwa wakulima. Ni pongezi nyingi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, masoko ya tumbaku yalikuwa yameshakufa. Masoko ya tumbaku hali ilikuwa mbaya, wanunuzi wote waliondoka. Leo tuna wanunuzi zaidi ya 15 katika nchi yetu ya Tanzania. Madaraja yameongezeka, wastani wa wakulima wa tumbaku hali ilikuwa mbaya sana, lakini leo wastani wa Kitaifa ni dola 2.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi wamemalizia masoko pale kwa wenzetu wa Musoma. Madaraja ya tumbaku wastani wao ilikuwa ni dola 2.5, hali ilikuwa ngumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana uongozi wa vyama vikuu vya ushirika hapa nchini pamoja na warajisi wasaidizi wa vyama vya ushirika hapa nchini kwa kazi ambayo wanasimamia wakulima na kusimamia ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niendelee kuomba wachape kazi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, yuko pamoja nao. Waendelee tu kuimarisha vyama vyetu vya ushirika kwa sababu karibu 60% ya nchi yetu ni wakulima. Ili waendelee kuwaunganisha wakulima wetu waendelee kujua kwamba, dira ya ushirika wakati mwingine ndiyo maeneo ambayo watakuja kupata faida kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, kwa upande wa barabara nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametupatia Ushetu zaidi ya shilingi bilioni 18. Tulikuwa na madaraja yaliyoshindikana toka uhuru. Leo tuna daraja letu la Mwabomba, mwaka 2024 wananchi wetu zaidi ya sita walikwenda na maji. Leo daraja lina shilingi bilioni 4.7 na linajengwa kiwango kizuri kwa zaidi ya mita 60.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tuna Daraja la Ubagwe ambalo nalo pia lilishindikana na lenyewe lina zaidi ya shilingi bilioni tano, tuna Daraja la Kasenga – Ulowa lina zaidi ya shilingi bilioni tano, Daraja la Ng’wande na lenyewe limepewa zaidi ya shilingi bilioni tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi sana kwa Wizara ya Ujenzi. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri aliyekuwepo, Ndugu yangu Mheshimiwa Bashungwa, alifika Ushetu na alijionea mwenyewe alipokuwa Waziri. Alishuhudia wananchi walipofurahi mapokezi yake baada ya mateso makubwa ya miaka nenda rudi kwa madaraja yale yaliyokuwa yameshindikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Wizara ya Ujenzi, tuna barabara yetu iliyowatesa wananchi miaka nenda rudi. Barabara inayotoka pale Nyandekwa – Kahama inakuja Uyogo ambayo ina kilometa 54. Naomba mwaka huu 2025/2026 wa bajeti angalau itengewe hata kilometa kadhaa ianze kujengwa taratibu kwa kuwa wananchi hawa wa Ushetu, hii barabara ndiyo kiungo chao kikubwa cha biashara na magari yao yanapita katika barabara hiyo, yanaleta mizigo katika Manispaa ya Kahama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kupongeza sana upande wa umeme. Tuna mradi mkubwa wa solar system, ambao una zaidi ya shilingi bilioni 11.7. Nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dotto Biteko, hali ni nzuri na mradi wa mabilioni ya fedha umekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, vijiji vyangu 112 tayari vina umeme na vitongoji tayari vimeanza kupelekewa umeme. Vile 15 tayari vimekamilika. Mheshimiwa Naibu Waziri, upande wa mafuta kwa kweli hongereni sana. Mafuta yanazidi kushuka bei, hali ya maisha ya Watanzania wanazidi kufurahia. Pongezi kubwa sana kwa usimamizi huu, endeleeni kusimamia na kuwasaidia Watanzania, endeleeni kumsaidia Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kazi mnayoifanya Waheshimiwa Mawaziri ni kubwa sana. Sisi kama Wabunge tunaendelea kuwapongeza sana, kwani kazi ni kubwa mno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mfano kama Jimbo langu la Ushetu, ni jimbo ambalo liko vijijini na ni la wakulima. Kwa hiyo, mafuta yanapopanda bei, wananchi wetu wanapata shida sana. Hata hivyo, kwa kipindi hiki mafuta yanazidi kushuka bei na wananchi wetu wanazidi kufurahia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza sana Serikali kwa upande wa shule. Leo hii najengewa shule ya shilingi bilioni 1.6 ambayo ni shule ya vipaji maalumu. Pia, ni Mheshimiwa Rais huyu huyu ambaye amenipelekea Hospitali kubwa ya kisasa ya shilingi bilioni 3.5. Jengo langu la utawala zuri kabisa la shilingi bilioni tano limepelekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, hii 10% ambayo mmekuja kuiruhusu, sisi tunaruhusu. Mmeongeza kutoka vijana hawa ambao walikuwa wanaishia 35, leo mmekubali miaka 18 mpaka 45.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kundi hili la wanaume limesahaulika. Kama akina mama hawa tunawapa mikopo wote bila kujali umri, hili kundi nalo Wabunge tunapopita kule majimboni tunalalamikiwa sana. Tuwape tu na hawa wote waweze nao kupata mikopo kwa sababu ni kundi kubwa, lakini ni kundi ambalo ni tegemeo katika familia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kundi hili ndilo unakuta linahangaika na ada, linagangaika kutibu familia, kundi hili ndilo kila kitu na shida ikipatikana nyumbani kundi hili linateseka. Naomba kwenye bajeti, kundi hili nalo liwekwe na liingie kwenye mikopo hii ya 10%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Halmashauri ya Ushetu, kwa mwaka huu peke yake, kwa vijana imetoa vikundi 85 zaidi ya shilingi 1,036,000,000 wamepewa hawa vijana wetu na akina mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, lakini pia niendelee kuunga mkono hoja. (Makofi)