Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitangulize shukrani kwako. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kupata fursa ya leo kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi ambayo anaifanya kwa ujumla kwenye nchi yetu pamoja na jimbo langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu na wasaidizi wake wote kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kutuunganisha na kutusaidia kupitia kwenye majimbo yetu. Mungu ambariki sana na ampe maisha marefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ambao tunatoka ukanda huu wa kusini, lazima tuishukuru Serikali. Tunaishukuru Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, kwa vigezo. Kwanza, kwenye jimbo langu wakati naingia 2020 kulikuwa kuna shida kubwa sana ya maji. Hata hivyo, Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliweza kutupatia zaidi ya shilingi bilioni 3.4 za kujenga chujio pale na tukaweza kusafisha maji katika Mji wa Mtwara yakiwa salama na safi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mtwara Mjini, ni jimbo ambalo lilikuwa na uhaba wa shule za sekondari takribani zaidi ya kata tisa. Hapa ninapozungumza, katika kata tisa, tumepatiwa shule za sekondari za mfano tatu, na shule ya moja msingi. Kwa hiyo, tunatoa shukrani kubwa kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza uchumi wa nchi, lazima tuwe na viwanda ndani ya nchi. Tunapozungumza Kanda ya Kusini, Mtwara na Lindi tuna malighafi ya aina nyingi sana. Hata hivyo, kwa suala hili naiomba Serikali, sasa kwenye mipango watusaidie kutuletea viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunaomba sana viwanda? Tumezungumza kuhusu ajira za vijana wetu na vijana wetu wengi wanamaliza vyuo mwaka hadi mwaka, nao wanategemea ajira. Tukiwa tuna viwanda vya kutosha, nadhani suala la ajira litakuwa ni ndoto kwetu kulizungumzia kila mara tunaposimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza tena Rais, mwaka 2024 tulipatwa na mafuriko; barabara yetu ya Mtwara – Kibiti - Lindi ilipata hitilafu kubwa sana ya kuvunjika kwa madaraja. Mheshimiwa Rais alitupatia fedha shilingi bilioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja yale. Pia, tuna imani kabisa, mpaka kufika kufika mwezi wa Tisa au wa Kumi madaraja yale yatakuwa yamekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, barabara hii imejengwa kwa muda mrefu sana, na kujenga kilometa moja barabara ya lami, standard inawezekana tukajenga kwa shilingi bilioni 1.4 na kuendelea. Ikiwezekana Serikali itutafutie fedha zaidi ya shilingi bilioni 800, tunaweza tukatengeneza barabara ya lami kutoka Dar es Salaam mpaka Lindi na Mtwara, ikawa shida yetu ile ya barabara imekwisha, kwa sababu shida ya kwanza ya madaraja Mheshimiwa Rais ameshatoa fedha, itakuwa hatuingii tena kwenye madaraja. Kwa hiyo, tutajenga barabara ambayo itakidhi mahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tunazungumzia shida za maji na mara nyingi Serikali imekuwa inatueleza kwamba sasa twende kwenye maji ambayo yanastahili ambayo ni maji ya kutoka kwenye mito mikubwa. Tunao Mto Ruvuma ambao unaweza ukatuletea maji katika Mkoa wa Mtwara na Lindi bila shida na maji yakawa mengi zaidi. Tuiombe Serikali, muda umefika sasa wa chanzo hiki cha maji ya kutosha tuweze kupatiwa fedha ili tupate maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishukuru Serikali kuhusu masuala ya umeme. Mtwara ilikuwa ni sehemu ina shida ya umeme takribani kwa siku umeme ulikuwa unakatika zaidi ya mara 30, lakini sasa hivi shida ya umeme imeisha. Tunamshukuru sana Rais na Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais, kwani tayari tuna bandari pale ambayo ina uwezo mkubwa. Tumetumia zaidi ya shilingi bilioni 156 kuitengeneza Bandari ile, lakini ilikuwa haifanyi kazi hasa kupitisha mazao ambayo tunalima kwenye Mkoa wa Mtwara kama vile korosho, mbaazi na ufuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekaa zaidi ya miaka mitatu bandari ile haipitiki na wala haifanyi shughuli za kimazao. Tunamshukuru tena Mheshimiwa Rais, tulipomlilia juu ya kuitumia bandari yetu, alisimama nasi na akasema Bandari ya Mtwara itafanya kazi; na kweli Bandari ya Mtwara sasa inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunasema bandari yetu tulikuwa tunaipigania ifanye kazi? Sasa hivi vijana wengi wa Mkoa wetu wa Mtwara au majimbo yaliyo karibu na bandari wanafanya shughuli zao za halali pale bandarini na wanapata fedha na wanajiendeleza. Pia, hata uchumi wa kibiashara katika jimbo langu sasa hivi umekuwa mzuri sana kutokana na bandari hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali. Tunao mpango na hii ninaishukuru sana Serikali kwamba tayari imeamua sasa kama kutujengea hili Daraja la Mto Ruvuma pale Kilambo. Daraja hili na wenzangu tulipiga kelele sana takribani miaka mitatu mfululizo tukiiomba Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaishukuru sana Serikali kwamba tayari imeshaingiza kwenye mpango. Kwa hiyo, ujenzi wa daraja lile utaleta manufaa makubwa na uchumi mkubwa kwa Mkoa wa Mtwara. Mara nyingi nimekuwa nawaeleza hapa Waheshimiwa Mawaziri na muda ule walikuwa hawanielewi kwa nini nazungumzia daraja lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mikoa nane ya Mozambique ambayo ni mikubwa na ina matajiri. Katika mikoa ile minane, kutoka kwenye mkoa wa mwisho Pemba kuelekea Beira - Nampula ambako wanatumia ile Bandari ya Nampula wanatumia zaidi ya kilometa 1,800 au 1,900 lakini kutoka kwenye mkoa wa mwisho tunaouzungumzia kuja Mtwara watatumia kilometa 800. Kwa hiyo, watatumia Bandari ya Mtwara yenye kilometa 800 kutoka kwao wanapoishi na hivyo bandari yetu itafanya kazi na tutapata mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kiuchumi ninalozungumzia la korosho. Niendelee kumpongeza Mheshimiwa Bashe, Waziri wa Kilimo. Kwa kweli sisi watu wa Mtwara tunampa sifa zake zote. Korosho Mtwara ilikuwa haina thamani kwa sababu kulikuwa kuna wahuni wanachezea zao la korosho. Mheshimiwa Bashe alisimama akaingilia zao la korosho na kuondoa kitu kinachoitwa box ambacho wahuni waliweka mle. Sisi tunawaita wahuni kwa sababu walikuwa wanawaibia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka kwenye shilingi 1,800/= mpaka shilingi 1,700/= kwa kilo; mwaka huu uliopita tumeuza korosho kwa shilingi 4,300/= na kuendelea. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza kuhusu suala la kilimo, tayari Sulphur iko kwenye ma-godown. Yaani hatuzungumzii shida ya Sulphur kwenye zao la korosho, tunamshukuru sana Rais, tunamshukuru Mheshimiwa Bashe kwamba kazi hii tunaiomba iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo nataka niishauri Serikali. Hizi halmashauri ziko tofauti. Ziko halmashauri zina uwezo wa kukusanya mapato zaidi ya shilingi bilioni moja, bilioni mbili au bilioni tatu, lakini ziko halmashauri zinakusanya zaidi ya shilingi bilioni 60 kwa mwaka. Sasa nini ninachotaka kukizungumza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko migao ya Serikali ambayo inatoka kupitia kwenye fedha za Serikali. Hebu tuangalie kwamba ziko halmashauri ambazo kwa kweli ziko nyuma kimaendeleo na halmashauri hizi tufike mahali sasa Serikali izi-boost baada ya kuachana na wale wenzetu ambao sasa hivi wamekuwa ni matajiri na wana fedha nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ningekuwa na uwezo kwenye halmashauri yangu kupata shilingi bilioni 60 za makusanyo kwa mwaka, ningekuwa niko mbali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaishauri Serikali kwamba iangalie kwenye huu mfumo na hasa nataka kuzungumzia fedha za tozo za barabara. Tukikubaliana na Serikali tukasema kwamba kuna halmashauri zaidi ya 10 kwenye uwezo wa fedha wanaweza kujitegemea, basi hizi tozo za fedha za barabara za TARURA inawezekana baadhi ya halmashauri zikapiga hatua sana kwenda kutengeneza barabara kwenye eneo husika ili tuondokane na ile adha inayotukuta kila mwaka kutengeneza barabara za moramu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unatumia zaidi ya shilingi milioni 200 kukwangua barabara kilometa 70 au kilometa 80 na mvua zikishanyesha, barabara ile imeharibika. Kwa hiyo, kila mwaka mtatumia shilingi milioni 100 au 200 kwenda kuburuza zile barabara. Kwa nini tusifike mahali tukasema tuna kilometa hapa zaidi ya 15, kilometa hizi bajeti yake iende tukaweke lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani baada ya miaka 10 itakuwa hatuwezi kupita tena kwenye barabara hizo kwenye maintenance, tutakuwa fedha zile tunafanyia jambo lingine lakini….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante, muda wako umeisha sasa Mheshimiwa Mtenga.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja.

MWENYEKITI: Hitimisha.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo la ajira. Hivi karibuni vijana wetu walikuwa wanahitajika kwenye usaili Jeshi la Zimamoto. Kitu ambacho kimetokea na ni kitu ambacho ni hatari sana, wanakwenda wale vijana pamoja ni sheria, sikatai ni sheria, wanapimwa ufupi au urefu. Wakishapimwa pale wanaambiwa wewe bwana una mita tatu haustahili kabisa kuwa kwenye Jeshi la Zimamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, twendeni tutafute lugha nyingine nzuri kwa sababu hao wafupi wameumbwa na Mwenyezi Mungu na kama wameumbwa na Mwenyezi Mungu ni vijana wetu, tumewasomesha, na wana elimu. Watafanya kazi wapi? Kwa hiyo, nawaomba sana, hili nalo tuliangalie, ni bomu ambalo linatujia. Sisi wenyewe hatujui kama hili ni bomu tunalitengeneza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)