Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hii hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, naunga mkono hoja kwa sababu hii ndiyo hoja inayohusu maslahi ya Wabunge na maslahi ya watumishi wa Bunge. Kwa hiyo, hii ni hoja yetu sisi kama Wabunge, na ninaiunga mkono moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa humu, tumeona sifa za watu wengi. Mimi niwapongeza Mawaziri wote walio chini ya Waziri Mkuu na Mawaziri wengine tunafanya nao kazi. Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, tunafanya naye kazi, Mheshimiwa Dorothy tunafanya naye kazi, lakini nampongeze sana Mheshimiwa Lukuvi. Amekaa Bungeni humu kwa muda mrefu, amekuwa mzee wa Bunge, ametushawishi mambo mengi sana ametushauri, tunamwombea kwa Mungu aendelee kuwepo, aendelee kutushauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Waziri Mkuu, watu wengi mnakaa humu ndani, lakini sijawahi kuona, unakaa na mwanadamu mstaarabu kama Waziri Mkuu wa sasa hivi tuliyenaye. Ni mstaarabu mno yaani. Ni mchapakazi na mstaarabu, anasikiliza kila mtu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nikawa nasikiliza maneno maneno; unajua bwana, Waziri Mkuu sasa amemaliza vipindi viwili. Akienda huku sasa, akiwa Mbunge, anafanyaje kama siyo Waziri Mkuu? Kwani kuna hoja gani? Mbona tumeona watu wengi tu! Tumeona Mzee Malecela, tumeona Marehemu Mzee Lowassa wanakuwa Mawaziri Wakuu na wanakaa humu ndani Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu arudi Bungeni. Habari ya vyeo, Mungu atajua. Yeye arudi Bungeni, ni mstaarabu mno. Mtu wa namna hii ambaye anafanya kazi usiku na mchana, amekuja kwangu pale mara tatu. Ameshaenda kila mahali na kila jimbo la Mbunge ameshaenda. Tunamwomba arudi Bungeni, tunamwombea huko anakotokea wamrudishe Bungeni, tukae pamoja naye ili asaidie hii nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu amepita vipindi vigumu sana. Alikuwa anafanya kazi na Marehemu Dkt. Magufuli, amekuja kwa Mama, amefanya naye kazi amemwonyesha kila mahali. Amemsaidia Mama kufanya kazi, nchi iko salama. Leo nchi iko salama kwa ajili ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia mimi sijui namfananisha na nani? Kwa sababu watu wengi mnajua mambo ya mpira humu ndani. Hakuna kitu kigumu duniani kama kupewa pasi halafu ukashindwa kufunga. Ma-forward wengi wanalaumiwa, wanapewa pasi hawafungi, lakini mama kapewa pasi ya Bwawa la Nyerere, kapiga goli; kapewa pasi Ikulu haijajengwa, kaijenga yote imeisha; kapewa Mji wa Magufuli, kapiga goli; kapewa madaraja, kapiga yote; kapewa ndege, zinaendelea. Hivi pasi gani ambayo hakufanya? Pasi zote alizopewa Mama, kafunga; sasa tunamtaka nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna nyingine alikuwa anajitangulizia mwenyewe na anaenda kufunga mwenyewe. Kwa mfano, sekondari za wasichana zilizojengwa kila mkoa kapiga pasi mwenyewe, kakimbia mwenyewe, kufunga. Anajijua Mama ametokana na jinsia ya kike, anatengeneza mazingira watoto wa kike waendelee kusoma. Kwa hiyo, kapiga pasi yeye mwenyewe. Katupa hela kwenye majimbo shilingi milioni 500; bilioni ngapi kwenye mambo ya TARURA; amefanya kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaweza kuwa Wabunge, unaweza kuwa Rais, unaweza kuwa kila mtu, lakini Mungu ndio anapanga mpango wake. Katika nchi yetu Mungu alimtoa Julius Kambarage Nyerere huko Musoma akampa Urais wa nchi hii akatuongoza miaka 24. Tukaungana na Zanzibar, Rais Nyerere alitoka upande wa pili wa nchi wa Tanzania Bara. Katikati hapa Mungu huyu huyu ametuleta Samia, huku tunamwita Mwalimu Nyerere Baba wa Taifa, Samia katokea upande wa pili wa Zanzibar amekuwa Rais na ni Mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nchi hii Mungu ndio anaipenda, kaleta baba akawa Rais, akaleta mama akawa Rais upande wa nchi. Sasa sisi ni nani kupingana na Mungu? Kwa hiyo, tukubali kwamba Mama miaka hiyo inayokuja ni ya kwake. Kwanza nashangaa, kwani ana upinzani? Maana yake ndiyo ameshapita. Sisi ndiyo atuhurumie huko aliko, lakini yeye tayari kura zilishajaa. Kwa hiyo, tunamwombea Mama, Mungu amlinde aendelee kuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mingi imeletwa Bunda lakini mradi wa Hospitali ya Wilaya ya Bunda juzi tumepewa shilingi milioni 680. Tunaomba Waziri Mkuu aje akafungue hospitali yetu ya Bukama angalau watu wetu waone kwamba hii hospitali sasa inafanya kazi vizuri. Kuna Bwawa la Skimu la Mariwanda, namshukuru sana Mheshimiwa Bashe, ametoa fedha za kwenda kukarabati lile Bwawa ambalo lilikuwa limebomoka, sasa ametoa fedha kwenda kulikarabati, wanaenda kulitangaza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Bwawa lingine ambalo ni jirani yetu, tunafanya kazi ya Bwawa Bunda Mjini na Bwawa linaitwa Kisangwa. Wametoa mkandarasi akaenda kulikarabati, tunashukuru wote walioshiriki katika kusaidia hilo jambo kuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwenye upande wa umeme. Huwa najiuliza sana, hivi kwa mfano mimi nina vitongoji 310 ambavyo vimebaki havijapata umeme, hatuna hela za kutosha za kupeleka vitongoji vyote. Hivi kwa nini tusiende Benki ya CRDB au Benki ya NMB au Benki ya Azania tukachukua ile tozo ya umeme inayotoka kwenye mafuta tukawapelekea CRDB au NMB tukawaambia tupeni fedha tujenge vitongoji vyote hivi, nyie mtakuwa mnalipwa na umeme?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi hii nayo inahitaji akili gani? Hatuna fedha, lakini tuna mapato ya kila siku. Kwa nini tusifanye hivyo? Sasa kwangu naomba mfanye pilot area, mtuletee fedha kutoka CRDB, watu wapewe umeme, walipe kwa kupitia mafuta? Kwa hiyo, naomba hili nalo lifanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zetu za msingi nyingi zimeoza na siyo nzuri sasa hivi. Tumefanya kazi kubwa sana kwenye sekondari, lakini shule za msingi, kwangu kuna shule inaitwa Masaba, yaani ni mbaya kuliko kawaida. Kuna Masaba, kuna Salama A na B, kuna Shule ya Nyang’aranga, kuna shule ya Songambele, kuna shule ya Chamtigiti; karibu zote na shule nyingine kama 15 nimeshapeleka TAMISEMI wazifanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga sekondari nyingi. Kuna sekondari ya Tingirima imejengwa, lakini bado kuna maabara ya Physics, maabara ya Kemia na maabara ya Biology hazijatengamaa. Jengo limejengwa, limepigwa paa, lakini ndani hamna kitu kinachoendelea, na Serikali imetoa shilingi milioni 870.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, watu wa TAMISEMI wanaohusika waende pale, walishafanya evaluation wakamalizie yale majengo ya sekondari ambayo tulitoa shilingi milioni 480 na majengo hayakukamilika. Pia, waongeze walimu kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Sekondari ya Sanzati wananchi wamechanga shilingi milioni 120, Serikali ika-double milioni 140, lakini sekondari ipo, majengo yapo, madarasa hayajaongezeka, jengo la utawala halipo, na vyumba vya maabara havipo. Tunaomba Serikali iende kwenye maeneo hayo isaidie kuleta maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunda ina barabara nyingi, lakini namshukuru Mheshimiwa Rais, Barabara ya kutoka Nyamuswa inaenda Bunda - Buramba imekamilika, ni ya lami. Pia, kuna Barabara ya Makutano - Butiama – Sanzati imekamilika, na ni ya lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Barabara ya kutoka Sanzati kwenda Nata imekuwa tatizo. Naiomba Serikali, haiwezekani mkandarasi akaenda akaweka lami kwenye mchanga tu halafu akapotea na imegharimu shilingi bilioni 46. Tunaomba wanaohusika tafadhali, tafadhali sana, nendeni mkamalizie ile barabara ambayo iko 50% na imebaki 50% kuimalizia. Naomba kwenye Serikali waende watusaidie kujenga hiyo barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mawaziri wote; nampongeza Waziri wa Fedha, kwa kweli tunamwona mara yuko Ufaransa, Ujerumani anahangaika. Jamani watu wanaofanya kazi tuwapongeze. Mawaziri wa sasa hivi, wengi wanafanya kazi wengi sana. Kwa mfano, ukimchukua Mheshimiwa Bashe anavyojitolea. Bahati nzuri Mama amewapa uhuru wa kutosha wa kufanya kazi zao, wakishindwa ni wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso sasa ndio usiseme. Yaani Mheshimiwa Aweso huyu basi tu, yeye anachoniudhi ni kwenda kuisimamia Simba inashinda. Hiyo ndiyo shida yake tu basi, lakini mengine anafanya mambo mazuri sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso amenipa mradi wa maji wa Ziwa Victoria kutoka Butiama kuja Nyamuswa na wananchi wanashukuru. Siku akifika Bunda ajiandae tu na gari ya zawadi, atabeba mbuzi, ng’ombe, na kila kitu. Tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru Mawaziri wote wanaohusika, wanaofanya kazi nzuri ya Serikali. Pia, namshukuru Mama, namshukuru Waziri Mkuu na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)