Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha mimi kunipa afya njema na kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imesheheni matumaini makubwa kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo ameifanya kwenye nchi hii ikiwemo kutoa fedha nyingi sana kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo Wilaya ya Nyang’hwale ama Jimbo la Nyang’hwale, ambapo tumeweza kupokea fedha nyingi sana kwenye miradi ya maendeleo. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja na sasa nianze kusema yafuatayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameweza kutoa fedha nyingi sana kwenye miradi mingi, lakini nitaisema miradi michache ikiwemo Sekta ya Elimu. Wilaya ya Nyang’hwale tumeweza kupokea fedha nyingi sana kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari na shule za msingi pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu, matundu ya vyoo na miundombinu mbalimbali. Mama Samia ameweza kutoa fedha nyingi sana kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya kisasa yenye tiles, yenye madirisha mazuri ya ku-slide.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ameweza kutoa fedha nyingi sana kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo. Leo hii watoto na vijana wetu wanaenda kwenye vyoo vya kisasa. Kwa kweli tunampongeza sana kwa kutoa fedha nyingi sana kwenye miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali kwenye upande wa sekta ya elimu, iweze kutoa fedha za kuendeleza majengo ama maboma ambayo yalijengwa na wananchi, yamekaa kwa muda mrefu, vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na vyoo. Naiomba na kuishauri Serikali iweze kutoa fedha kwenye bajeti ya mwaka huu ili iweze kukamilisha hayo ambayo nimeyataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais aliweza kutupa fedha nyingi sana. Jimbo la Nyang’hwale tulikuwa na shida ya maji, Mama Samia ametupunguzia adha hiyo. Hivi nilivyosimama na kuongea hapa, ni zaidi ya 70% ya vijiji vya Jimbo la Nyang’hwale tunapata maji kutoka Ziwa Victoria na kwenye vyanzo vya visima virefu ambavyo tumechimbiwa kwa zaidi ya 70%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba Serikali itenge fedha kwenye bajeti hii iweze kutupatia. Tuliomba zaidi ya shilingi bilioni 4.5 ili tuweze kusambaza mabomba na kukamilisha zoezi la usambazaji wa mabomba kwenye kata 15 na vijiji 62 ndiyo tutakuwa tumekamilisha. Itupatie hizo shilingi bilioni 4.5 tuweze kukamilisha changamoto hiyo ya maji kwenye Jimbo la Nyang’hwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameweza kutoa fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali ikiwemo umeme. Hivi ninavyoongea Jimbo la Nyang’hwale lina vijiji 62. Vijiji vyote 62 vimeshafikiwa na umeme. Tuna vitongoji 273, mpaka sasa hivi ninavyoongea vitongoji 88 vina umeme na vitongoji 15 mkandarasi yuko site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, hawa wakandarasi wasimamiwe vyema na naishauri Serikali iweze kuongeza fedha ili sasa tuweze kupunguza vitongoji vingine ambavyo vimebaki ili tuweze kumaliza vitongoji vitakavyokuwa vimebaki angalau hata ndani ya miaka mitatu au minne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameweza kutoa fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa VETA. Tunao ujenzi wa VETA kwenye Wilaya ya Nyang’hwale, lakini ujenzi huu unakwenda kwa kusuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali na kuishauri iendelee ku-pump fedha ili tuweze kukamilisha kwa wakati majengo hayo ili vijana wetu waingie kwenda kujifunza ufundi stadi, kwa sababu vijana wengi sasa hivi wako mtaani hawana kazi na hawana ujuzi. Napenda sana kuishauri Serikali na kuiomba iweze kutoa fedha kwenye bajeti hii tuweze kukamilisha hayo majengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Kamishna wa Kupambana na Kadawa Kulevya. Kamishna huyu kwenye bajeti hii nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba anaendelea kupambana na wameweza kukamata madawa mengi. Tani za dawa za kulevya zimeshikwa na ameweza kukamata na kuchoma mashamba mengi ya bangi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hiyo anayoifanya ya kuokoa vizazi vyetu na vijana wetu na nguvu kazi, ni kazi kubwa, naomba aongezewe fedha ili aweze kupambana na kuzuia. Leo hii vijana walio wengi wanavuta bangi na kutumia dawa. Kwa kweli kazi kubwa anaifanya. Analalamika; mimi niko kwenye Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, alikuja Kamishana akaelezea kwamba ana upungufu wa fedha na vitendea kazi na nguvu kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kupitia bajeti hii Mheshimiwa Waziri Mkuu aweze kuidhinishiwa ili aweze kumpa Kamishna wa kupambana na dawa za kulevya aweze kupambana nazo vizuri dawa hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazidi tena kuipongeza na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri. Mimi nasema kama mwakilishi wa wananchi wa Nyang’hwale, Mama Nyang’hwale anatudai. Tunasema, Kazi na Utu, Tunasonga Mbele 2025 Nyang’hwale kura nyingi kwa Mama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Naunga mkono hoja. (Makofi)