Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ENG. DKT. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ili nami niweze kuchangia hoja muhimu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa bajeti yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutuongoza vizuri hasa kwa kutumia falsafa zake za 4R’s. Vilevile, kwa kuratibu na kuhakikisha kwamba kuna maendeleo endelevu ya mipango ambayo tumejiwekea wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, napenda kumpongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uratibu mzuri wa shughuli za Serikali na kwa usimamizi mzuri wa mipango ya maendeleo ambayo ndiyo itakuwa msingi wa mchango wangu wa leo. Tatu, kwa kuandaa bajeti nzuri ambayo itahakikisha kwamba kuna uendelevu wa hiyo mipango ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, napenda kuwapongeza wasaidizi wa Waziri Mkuu kwa kutengeneza bajeti hii nzuri. Kwanza, Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko na Mawaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa William Lukuvi pamoja na Naibu wake na Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete pamoja na Naibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika uendelezaji wa mipango ya maendeleo katika hiyo hotuba yake ambapo rejea ya kwanza nakwenda kwenye Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2025/2026. Nikiangalia pale kwenye ukurasa wa 42 kuna vigezo vya kuchagua vipaumbele vya bajeti yetu ya mwaka huu ambavyo vimewekwa ambapo nikiangalia bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imevifuata kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nikiangalia katika mpango huo huo ukurasa wa 59, kuna kigezo cha kuendelea kutekeleza miradi ya kipaumbele katika sekta mbalimbali. Kuna Sekta ya Ujenzi ukurasa wa 59, kuna ya miradi yenye lengo la kuchochea maendeleo ya uchumi, pale kuna sekta ya uchukuzi, pia ukurasa wa 60 hivyo hivyo kuna sekta nyingi ambazo zimewekwa pale ambazo zimepangiliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana bajeti hiyo ya Waziri Mkuu kwa sababu imehakikisha kwamba kuna uendelevu wa mipango ya maendeleo. Mipango mingi imepangwa pale lakini nitatoa mifano michache ambayo itadhihirisha hilo na kuonesha ni wapi pa kutilia nguvu ili tuweze kuendelea zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aya ya 39, kuna orodha ndefu ya hiyo mipango ambayo itatekelezwa kulingana na bajeti hii, nami ninampongeza kwani orodha hiyo kama itatekelezwa kama ilivyopangwa, kweli tutakuwa tumesonga mbele sana katika mwaka huu ambao bajeti hii inakwenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kutoa mifano michache ambayo nitaisisitiza, nikiangalia aya ya 42 hadi ya 43 ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu hapo, amejadili reli yetu ya SGR. Ukiangalia katika vipande vyote ambavyo vimetajwa pale Dar es Salaam – Morogoro, Morogoro – Makutupora, Makutupora – Tabora, Tabora – Isaka, Isaka – Mwanza na Tabora - Kigoma utagundua kwamba maendeleo ni mazuri na hiyo yote inatokana na usimamizi mzuri ambao unaratibiwa na ofisi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika hilo tumpongeze na tunasema kwamba aendelee katika usimamizi huu mzuri ili katika mwaka husika malengo ambayo yamepangwa yaweze kufikiwa. Katika aya ya 44 mpaka 47 ameongelea uimarishaji wa huduma za bandari hasa ya Dar es Salaam. Ukiangalia pale kitu ambacho kimetajwa kwanza kuna uboreshaji ambao unaonesha dhahiri kwamba umezaa matunda na hiyo yote ni kwa sababu ya usimamizi mzuri wa hayo yaliyopangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye ubebaji wa makasha, ameorodhesha pale kwamba tumefika makasha 687,000 kutoka makasha 670,000 katika miezi nane ya mwaka huu ambalo ni ongezeko kubwa. Hii yote ni kwa sababu ya usimamizi mzuri unaofanywa na ofisi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, ukienda kwenye meli zinazosubiri nangani, zimepungua kutoka 30 hadi tatu. Ukienda kwenye muda wa kuhudumia meli, umetoka kwenye siku 10 hadi siku tatu. Ukienda kwenye mapato ya TPA, yamepanda kutoka shilingi bilioni 850 hadi shilingi trilioni moja katika muda wa miezi nane. Hii yote imetokana na usimamizi mzuri na bajeti hii ambayo imepangwa ilenge katika kusimamia maendeleo haya ili yaweze kuboreshwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye aya ya 48 mpaka aya ya 50, hapa ameongelea miundombinu ya ndege hasa ATCL. Hapa ameonesha kwamba ndege zimeongezeka hadi kufikia ndege 16 na nchi ambazo ndege zinakwenda mpaka sasa hivi ni 16. Huo ni uratibu mzuri kabisa, na tunakokwenda zinapangwa kuongezwa na ameonesha kabisa kwamba mwaka huu tunaweza tena tukaongeza destination nyingine tukaenda Kinshasa. Abiria wameongezeka na mizigo imeongezeka. Hivyo, bajeti inayopangwa hapa ilenge katika kusimamia maendeleo haya ili yasirudi nyuma, tuendelee kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, aya ya 51 ameongelea madaraja makubwa. Huko nyuma tulianza na madaraja makubwa Tanzanite, Wami na Kigongo Busisi. Unakuta haya yamekamilika na tunakoelekea hayajaisha mengine mapya. Tunaomba basi katika kitengo chake hiki cha usimamizi na ufuatiliaji miradi, bajeti hii iweze kusimamia maendeleo haya ili tuweze kuyaendeleza na tusirudi nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii imejaa miradi mingi ambayo inaonesha wazi kwamba ufuatiliaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu ni mzuri. Tukienda kwenye ujenzi na ukarabati wa meli tukianzia Ziwa Victoria, tulianza na MV Victoria na MV Umoja ambazo sasa hivi zinafanya kazi vizuri kule na hiyo yote ilitokana na usimamizi wake mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka hata wakati wanajenga kule chelezo walikuwa wanatembelea pale mara kwa mara. Kwa hiyo, sasa tuna MV Mwanza, Hapa Kazi Tu iko 98%. Nayo tunaomba basi isimamiwe vizuri ili katika hiyo mipango iliyopangwa iweze kwisha kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, katika Ziwa Tanganyika kuna mipango mizuri ya meli za kukarabati MV Sangara, MV Liemba pamoja na ujenzi wa meli mpya. Hivyo, tunaomba kitengo chake hiki cha usimamizi kiweze kujikita hapo twende vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mradi ambao unaonesha wazi kwamba usimamizi huo unakwenda vizuri ni mradi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere. Mwendelezo wa usimamizi umelipa, na sasa hivi bwawa hilo limekamilika, na huo ni mfano mzuri wa usimamizi ambao unaendeshwa na ofisi yake. Kwa hiyo, bajeti hiyo iende vizuri katika usimamizi huo. Sasa ukienda kwenye randama ya Ofisi ya Waziri Mkuu ukurasa wa 12.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Injinia muda wako umeisha, ninaomba uhitimishe.
MHE. ENG. DKT. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja nihitimishe. Katika Fungu 37, inaonekana kabisa kuna Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji Serikalini. Kitengo hicho ndicho ambacho ni jicho la kuangalia maendeleo haya. Hivyo, tunaomba kitengo hiki kiimarishwe na tuhakikishe kwamba bajeti inapatikana ya kutosha ili maendeleo haya yaweze kuwa endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)