Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii, nami niweze kuchangia hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kwa kweli nianze kwa pongezi za dhati, Waziri Mkuu ametoa hotuba ambayo imetathmini angalau kwa miaka ya karibuni kuhusu utekelezaji wa Serikali na ametathmini utekelezaji wa mwaka huu wa fedha 2024/2025, lakini ametoa maono kwa utekelezaji wa mwaka ujao wa fedha 2025/2026. Nampa hongera sana, hotuba yake Watanzania wameipokea na kuielewa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Julai mwaka 2002 huko Durban Afrika Kusini, Wakuu wa Nchi za Afrika (AU) walipokaa walikubaliana kuwa na azimio moja kubwa la nchi zote za Afrika kuwa na utaratibu wa kujifuatilia na kujitathmini kuhusu utekelezaji wa demokrasia na utawala bora na pale Wizara ya Mambo ya Nje kiliundwa kitengo maalum chini ya Idara ya Afrika ambacho kilikuwa kinasimamia utekelezaji wa azimio hilo ndani ya nchi. Sekretarieti ya APRM ilianzishwa pale Mambo ya Nje ili kumsaidia Mheshimiwa Rais ambaye alikuwa signatory kwenye ule Mkutano wa Durban kufuatilia utekelezaji wa lile azimio - Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kweli kila mwaka tulikuwa tunaandaa taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa hilo azimio. Sasa nirejee tu kwamba AU iliandaa mwongozo kwa kila nchi kujitathmini, lakini huo mwongozo ulikuwa ni kitabu kikubwa sana chenye kurasa zaidi ya 300, kila nchi ilikuwa inatumia huo mwongozo ili kujitathmini kwamba imefikia hatua gani katika utekelezaji wa demokrasia na utawala bora wa kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia waraka wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, azimio hilo ameliboresha sana kwenye zile 4R’s. Kuridhiana, Kustahamiliana, Kufanya Mageuzi Muhimu katika Nchi na Kutoa Wito wa Kuijenga Nchi Upya kwa Kushirikiana, hizo ni 4R’s.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya kwamba Wabunge wote hapa pamoja na wananchi na viongozi wa chama tumekuwa tukimpongeza Mheshimiwa Rais kwa waraka ule ambao ni mwongozo na maono ya namna ya kuboresha lile azimio la mwaka 2002, utakubaliana nami kwamba maono hayo ya Mheshimiwa Rais yalihitaji sekretarieti ambayo ingeweza kumsaidia kufanya uratibu wa jambo hilo ambalo ni kubwa sana na linasifiwa Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekretarieti hiyo haipo, ninatoa wito kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu aongoze kuundwa kwa sekretarieti ya 4R’s ambayo itasaidia sana kuweka vizuri utekelezaji kwenye kila sekta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya Mheshimiwa Rais kunyoosha mkono wa upendo kwa vyama vyote vya siasa kupitia hizo 4R’s lakini na upendo wake kwa wananchi wa Tanzania wamejitokeza wananchi wenzetu ambao wamekuwa wanabeza kazi za Mheshimiwa Rais, na wanatumia maneno ya kejeli na ambayo hayana heshima. Wakati mwingine wamekasirika utafikiri wameudhiwa huko nyumbani kwao na mambo mengine mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani jambo hili ambalo linaenda kutaka kumomonyoa mshikamano wetu kama Taifa ni mambo ambayo inatakiwa tuwe serious katika kuyashughulikia. Siyo mambo ya kuangalia kwa kuyadharau. Katika nchi nyingine mambo yalianza kumomonyoka hivi hivi mpaka wakapata matatizo. Tusije tukakubaliana na msemo wa Kiswahili wa fadhila ya punda ni mateke, halafu tukaacha hapo hapo, lazima tuwe serious.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natoa wito, Wabunge na viongozi wote wa CCM tusimame imara katika kumtetea na kumlinda Mheshimiwa Rais dhidi ya njama za hovyo kama hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, siyo kwa hilo tu, ila kwa mambo ambayo ameyafanya kwenye jimbo langu na majimbo ya Wabunge karibu wote hapa. Mambo makubwa sana ya maendeleo yamefanyika kwenye sekta zote za miundombinu; barabara, usafirishaji, umeme, yote kwa ujumla kafanya vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya huduma za jamii, afya, maji, elimu, kafanya mambo makubwa sana. Watanzania wanayajua na dunia inajua. Tusimame imara kumtetea Mheshimiwa Rais. Vilevile, kwenye eneo la uchumi napo kafanya makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi yangu ya kijimbo ambayo ningependa Mheshimiwa Waziri Mkuu ayachukue na kuyafanyia kazi ni mambo kama manne tu. Kwanza ni barabara namba nane. Wakati zinapitishwa hizi barabara kuu mwaka 1964 zilikuwa 26 tu; 1964 zilikuwa barabara kuu 26, hatimaye sasa hivi tuna barabara zaidi ya 138, lakini barabara namba nane ambayo ilikuwa namba nane tangu 1964 haijakamilika. Hili jambo naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu alichukue ofisini kwake kwa ajili ya kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inatoka Mwanza, inapita Nzega, inapita Tabora, inapita Sikonge kwangu, inakwenda Rungwa, inakwenda Makongolosi, inakwenda mpaka Mbeya. Hii barabara ni kubwa sana, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aichukue aifanyie kazi, ili ikamilike. Vipande vitatu havijakamilika. Kipande cha kutoka Rungwa, cha pili ni cha kutoka Rungwa mpaka Makongolosi na cha tatu ambacho hakijakamilika ni cha Rungwa kupitia Itigi kwenda Mkiwa. Hivyo, vipande vitatu vikikamilika, barabara hii itakuwa imekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kukamilisha miradi ya maji ambayo ni mikubwa. Mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria kwenda kwenye miji 28, huu ni mradi mkubwa sana ambao naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu azidi kuuwekea nguvu ya kiutekelezaji. Pia kuna miradi ya umwagiliaji ambayo nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote, hasa Waziri wa Kilimo, waendelee kuiangalia kwa karibu na Wizara ya Fedha iendelee kutoa fedha kwa sababu, umwagiliaji ndiyo ukombozi wa kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila umwagiliaji tukategemea mvua tu za Mungu inawezekana kama Taifa, tukakwama. Kwa hiyo, ni jambo ambalo ni muhimu sana. Mradi wangu wa Uluwa ambao ulikwama tangu 2009, naomba nao upewe kipaumbele cha juu ili uweze kuanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, mimi huenda ndio naongoza, jimbo langu ni kubwa kuliko yote. Kuna tarafa ambayo tumeiombea iwe jimbo jipya. Hakuna kata yoyote ambayo inaweza ikafikika kule kwenye Tarafa ile ya Kiwele bila kutembea zaidi ya kilomita 200. Kwa hiyo, kokote utakakokwenda kwenye Tarafa ya Kiwele ni lazima utumie kilomita 200. Ni kweli kuna watu 100,000 lakini hao watu 100,000 nao vilevile wanahitaji uwakilishi mzuri, uwakilishi wa karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa ili nitembelee jimbo, ni lazima nitumie mafuta ya zaidi ya shilingi 2,000,000. Wapo wenzangu hapa wanaweza kutumia mafuta ya shilingi 200,000 wakatembelea jimbo likakamilika, hata wewe mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo lilikuwa la mwisho, na ninaomba sana haya niliyoyazungumza yawekewe kipaumbele. Nashukuru sana, Mungu azidi kumbariki Mheshimiwa Waziri Mkuu, azidi kumbariki Mheshimiwa Rais na Serikali nzima kwa ujumla wake. Ahsanteni sana. (Makofi)