Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026


MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na kumshukuru kwa utumishi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na kiukweli nchi hii tangu tumepata uhuru, tumekuwa na Mawaziri Wakuu takribani 14, mpaka yeye wa sasa hivi. Ukiachana na Mheshimiwa Daktari Frederick Sumaye, Waziri Mkuu mstaafu, miongoni mwa wale 13 aliyefuata kwa kukaa miaka mingi mpaka sasa hivi ni Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na kwamba ni jambo ambalo ameweka rekodi yake, pamoja na kufuata rekodi ya Mheshimiwa Frederick Sumaye, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu mimi binafsi kabla hata sijaingia huku Bungeni nimekuwa nikimfuatilia kama kiigizo chema. Kwa sababu, Mheshimiwa Waziri Mkuu watu wote wanaomfahamu hata ukiwa unazungumzanaye ni mtu mstaarabu sana, very humble. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunakushukuru sana baba yetu kwa utumishi wako, humbleness yako na namna ambavyo upo tayari kuwasikiliza watu, wote ni wako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka hata mara ya kwanza kabisa nimekuja, miongoni mwa watu ambao nilienda kusalimiana nao, alikuwa ni yeye. Tunasema hivyo kwa sababu, pia amemsaidia sana Mheshimiwa Rais katika majukumu yake kwa nafasi yake kama kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu bado ana nguvu, inawezekana bado akaendelea kutumika katika maeneo mengine, lakini sidhani kama kuna mtu ana wasiwasi na utendaji wa Mheshimiwa Waziri Mkuu na humbleness yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia sehemu chache sana kwa sababu, nawakilisha kundi la vijana katika Bunge hili, itakuwa siyo busara na hawatanielewa kama sitazungumza kuhusu tatizo la ajira kwa vijana kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Wajumbe wa Kamati wametoa maoni yao, nami nakubaliana na mapendekezo na maoni ya Kamati kuhusiana na suala la ajira, hususan katika ile mifuko ya kukopesha vijana. Pia, tunaipongeza Serikali kwamba wameamua warudishe utaratibu mpya wa kukopesha vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja specific, wakati sisi vijana wa nchi hii bado hatujatosha kwenye ajira za Serikali zinazotangazwa katika soko la ajira, bado kuna gap kubwa sana. Watanzania wengi vijana bado wana changamoto ya kujikimu kwa sababu, hawawezi kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati sisi tuko katikati ya lindi hilo, kumeibuka wimbi kubwa la raia wa kigeni ambao wanafanya kazi za wazawa, kinyume na Sheria ya Mwaka 2015 ambayo inaitwa Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni Nchini. Sasa, watu wanafahamu kuna maeneo ambayo raia wa kigeni, ambao wengine ni wachina na waturuki, wanafanya mpaka Uber na Bolt; wanafanya kazi ambazo tungeweza kufanya sisi Vijana wa Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hawa raia wa kigeni wamejaa pale Kariakoo kiasi kwamba, wanauza mpaka hereni za shilingi 3,000. Sasa sisi kama vijana wa Tanzania, mawinga wa pale Kariakoo, watafanya shughuli gani? Kwa hiyo, niliona ni busara sana tuliangalie hili jambo. Ni jambo ambalo kwa kweli, linaathiri shughuli za wazawa kama sisi, Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifuatilia pia, utafahamu kwamba, raia hawa ambao ni wa kigeni wanafanya shughuli mpaka za kwenda kugonga nyumba za watu, nyumba moja baada ya nyingine, wanakuwa wana kigari chao wamejaza vyombo mle, wanapita nyumba moja baada ya nyingine, wanakuwa na Mtanzania mmoja wamemtanguliza pale. Sasa tunakwenda wapi? Tunajua kuna utaratibu wa kuratibu ajira za wageni, lakini wamefika hatua ambayo mpaka sisi tunashangaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna mnyororo wa thamani kuichumi hapo katikati. Watanzania walikuwa wanaweza kwenda China wanafunga mzigo, wanakuja hapo Dar es Salaam, Kariakoo, wanawauzia wengine wa hapa ambao na wao watachukua, watapeleka pale Singida Mjini. Wengine wanaotoka Ikungi watakwenda Singida Mjini, watachukua mzigo watapeleka Ikungi, wakifika pale Ikungi kuna mwingine atachukua, atapeleka ndani ndani huko, Isuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa katikati kote wanakopita kuna hela ambayo inaachwa, ambayo hawa ni Watanzania walikuwa wanapata chochote katika huo mnyororo. Sasa hivi kama raia wa kigeni anaweza kutoka China moja kwa moja akachukua hela za katikati hapa, zote akachukua yeye, maana yake hapa sisi Watanzania twende wapi? Sisi kama raia wa Tanzania, vijana wa Tanzania, waende wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado siamini kabisa kwamba, imefika hatua tumeshindwa kufuatilia hili jambo na kulidhibiti. Naomba wakati Waziri anakuja kufanya hitimisho, Serikali itueleze wanachukua hatua gani kudhibiti wimbi kubwa la raia wa kigeni ambao wanakuja Tanzania? Wanakuja kwenye nchi yetu wanakwenda mpaka vijijini kufanya shughuli ambazo zingeweza kufanywa na vijana wa Tanzania na akina mama wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini tuna intelijensia ya kutosha kubaini ninavyovisema. Naomba msipige hoja rungu, nendeni mkafuatilie ili mjue kama hiki kitu kipo na kinafanyika kwa sababu, kinazungumzwa kila siku. Leo kulikuwa kuna uwezo, mama yule akaweza kwenda dukani, akanunua mchele kwenye duka la Mangi, halafu akarudi kwenye kibanda chake cha kupikia mama lishe akapika wali, akapika na vitumbua, asubuhi akauza vitambua kwa yule yule Mangi anayeuza duka…
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hanje, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jacqueline Msongozi.

TAARIFA

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa. Nataka nimpe Taarifa mchangiaji anayechangia sasa. Ni kweli kabisa anachokisema. Ukiangalia ndugu zetu wa nchi za jirani wamekuwa wakienda mpaka kwenye mashamba yetu huko vijijini wakati huu wa mavuno. Wanakwenda kule kuwarubuni wananchi kununua mazao kwa bei ya chini, wanapeleka mpaka mifuko kule mashambani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani ipo haja ya kuhakikisha kwamba, halmashauri zetu kule usimamizi uwe mzuri kwa sababu, mimi ninachofahamu huwezi kutoka hapa ukaenda nchi za jirani, za wenzetu, ukaingia mpaka mashambani kwao. Kwa hiyo, wanaona kuna loophole katika nchi yetu ya Tanzania ya kwenda huko na kufanya vitendo kama hivyo. Ahsante.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Hanje unapokea taarifa hiyo?

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, raia wa kigeni wanakopesha, mpaka ile ya kukopesha buku buku, kila siku wanaenda wanagonga, kama Waha. Waha wamerudi wote Kigoma kwa hiyo, napokea taarifa yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwenye hoja yangu ya pili. Nitazungumza kuhusiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Nchini, Jenerali Erasto Lyimo, nafikiri jina sijalikosea. Wanafanya kazi nzuri sana kwa sababu, najua waathirika wakubwa wa dawa za kulevya nchini ni pamoja na vijana. Kuna sababu nyingi, sidhani kama kuna muda wa kuzizungumza sababu ambazo zinasababisha watu waingie kwenye dawa za kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana kwa jambo moja. Mpaka sasa hivi wameweza kutumia teknolojia kwa ajili ya kubaini, kufuatilia na kudhibiti dawa za kulevya nchini. Tunapoteza vijana wengi sana kwa sababu ya matumizi ya dawa za kulevya. Ukienda kwenye zile sehemu za uraibu, unaweza ukaumia roho sana. Kwa hiyo, nawapongeza na ninawaomba wasiache kwa sababu, sasa hivi huko Dar es Salaam hakufai, yaani kuna hizo bar; wana shisha humo, hapafai kabisa. Tunaomba mwendelee kukazia hapo hapo na Serikali itawaunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa, siyo kwa umuhimu, niwaambie tu, hakuna mtu anayeweza kuzuia uchaguzi jamani. Kuna vitu vingine unaweza ukampa mtu jina bure. Kulikuwa hata hakuna haja ya kufanya naye jambo lolote, lilikuwa ni jambo la kuliacha lipite tu. Hakuna mtu mwenye uwezo wa kudhibiti uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA. Pale hakuna hata wapigakura 5,000,000. Huwezi ukawaambia watu wazunguke mikoani wakatafute signature milioni 15, ya nini? Automatically ni natural death. Kwa hiyo, hakukuwa na haja ya kutumia nguvu. Achaneninao, hawana hata fedha za kuzunguka kwenye mikoa kufanya mikutano ya hadhara huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri shughuli nyingine, Mheshimiwa Waziri Mkuu kama alivyoongeza bajeti, nimeona bajeti ya uchaguzi imeongezeka, hebu twende kwenye mambo ya msingi. Watu wengine wanafanya shughuli nyingine, wanaweza kuanzisha wakawa kikundi cha harakati kwenye nchi, viko vingi. Kuna NGO’s za harakati zimesajiliwa, lakini masuala ya uchaguzi nafikiri msiondoke kwenye focus, tuendelee kwenye masuala ya uchaguzi, watu watafanya uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkitaka kujua kama hakuna anayeweza kuzuia uchaguzi, kama kungekuwa kuna watu wa kuzuia uchaguzi, hata jana pale wakati wanamchukua, wasingemchukua. Achaneni na hizo habari, twendeni kwenye focus, uchaguzi upo.