Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii kukupongeza wewe kwa kazi kubwa ambayo unaifanya. Hili ni Bunge letu la mwisho, lazima tukupongeze wewe kwa sababu, tulikuchagua na umetuwakilisha vyema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa kazi wanayoifanya. Pia, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa miaka hii minne. Wote ni mashahidi tulianza naye, lakini Mungu amesaidia tunamalizanaye na kazi kubwa imefanyika Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimpongeze Waziri Mkuu wetu kwa kweli, umemsaidia vizuri sana Mheshimiwa Rais. Umekuja kwenye majimbo yetu, umemsemea vizuri Rais, umekitetea Chama Cha Mapinduzi, vilevile umetusemea sisi Wabunge wako vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hilo, Waziri Mkuu vilevile wakati anazunguka kwenye majimbo yetu kwa kweli, alitekeleza vizuri sana kazi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa sababu tuliona alikuwa akishughulikia mambo mengi ya Serikali, hususani kwenye matumizi ya fedha, miradi ya maendeleo na mambo mengine. Kwa hiyo, nimpongeze sana kwa kuwa mwakilishi mwema wa Mheshimiwa Rais na kwa kweli ameitendea haki nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maeneo machache ya kuchangia katika Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Eneo la kwanza ni upande wa SGR. Kwanza, niipongeze sana Serikali na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais ambaye alichukua ujenzi wa reli ya kisasa ukiwa takribani 30% kwa kipande cha kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma mpaka Makutupora. Ninyi ni mashahidi, kwamba Mheshimiwa Rais aliweka commitment kubwa na sasa hivi tumeshuhudia, wananchi wameshudia, ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma umekamilika na kazi imeanza kuonekana. Ninaomba tumpongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hilo data zinatuonyesha kuwa ndani ya miezi saba tangu SGR ilipoanza kufanya kazi wamekusanya si chini ya bilioni 54. Wastani wa wasafiri kwa miezi saba ni takribani milioni moja na laki nane na kwa mwezi takribani wasafiri laki mbili na nusu wanatumia usafiri wa SGR, haya ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hilo pia wote ni mashahidi, mbali ya usafiri wa ndege ambao wachache walikuwa wana uwezo wa kutumia sasa tumepunguza sana mwendo wa kukaa barabarani, kutoka masaa tisa hadi kumi hadi masaa matatu na manne. Haya ni mafanikio makubwa sana kwa Serikali ya Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna lots ambazo tulishasaini mkataba. Kipande cha Dodoma hadi Makutupora kipo zaidi ya asilimia 90 kuna lot ya kutoka Makutupora hadi Kigoma, lot ya kutoka Makutupora hadi Mwanza. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, tumetembelea tumeona kazi ambayo inaendelea na ni kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sasa Serikali kwa sababu tayari tumeona tija ya uwekezaji kwenye SGR ni vizuri sasa bajeti inayokuja ikaweka nguvu kubwa kwenye ujenzi wa SGR ili tukamilishe reli ya kwenda Kigoma na ya kwenda Mwanza; hilo niliona niishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni kilimo. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais na vilevile Mheshimiwa Bashe kwa kuweka nguvu kubwa sana kwenye kilimo. Sisi sote ni mashahidi bajeti ya kilimo ime-triple kwa hii miaka minne, vilevile bajeti ya umwagiliaji ime-triple kwa hii miaka minne. Katika Jimbo langu la Manyoni Mashariki tumepata miradi mikubwa ya umwagiliaji. Tuna Mradi wa Umwagiliaji wa Mbwasa wa bilioni 18 ambao tayari mkandarasi alishasaini mkataba, amekwishakabidhiwa site na wakati wowote ule ataanza kufanya kazi; haya ni mafanikio makubwa. Pia tuna miradi mingine ya umwagiliaji Manyoni, Mradi wa Udimaa pamoja na Ngaiti, Msemembwa na kwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu hapa ni kwamba, mwaka huu tumeona wenyewe Waheshimiwa Wabunge kwamba mvua hakuna. Sasa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ijikite kwenye kilimo cha umwagiliaji. Tuangalie nchi za wenzetu ambao wamejikita kwenye kilimo kama vile Australia, Ugiriki na maeneo mengine. Hawa hawategemei mvua na badala yake wanategemea kilimo cha umwagiliaji. Kwa sababu hiyo ningeshauri sasa Serikali iweke commitment kubwa kwenye bajeti hii na bajeti ya Wizara ya kuhakikisha kwamba tunapeleka fedha nyingi kwenye kilimo cha umwagiliaji ili wananchi wetu waweze kulima mara tatu hadi mara nne kwa mwaka. Kwa kupitia hilo tutakuwa tumemkomboa mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kama nilivyosema, kwamba mwaka huu ni mwaka wa ukame sana. Sasa je, Serikali imejipanga vipi kuhusiana na kuwasogezea wananchi mahindi ya bei nafuu? Kama mwaka jana tulivyofanya, Mheshimiwa Rais kwa kweli alitusaidia sana Waheshimiwa Wabunge; mahindi ya bei nafuu yalifika kwenye Majimbo yetu. Wananchi wanauliza Serikali imejipangaje mwaka huu kupeleka mahindi ya bei nafuu kwa kupitia NFRA kwa sababu mwaka huu siyo mwaka mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nirudie kuipongeza sana Serikali, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. Kwenye jimbo langu tumepata fedha nyingi sana; tuna ujenzi wa shule ya wasichana ya bilioni 4.5 ambayo imekwishakamilika na inadahili watoto, haya ni mafanikio makubwa sana. Tulipata pia 1.9 billion ya kujenga na kukarabati Hospitali ya Wilaya; ilikwishakamilika na inafanya kazi vizuri. Haya ni mafanikio makubwa; na kwa kupitia hili ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)