Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii. Kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ndiye muweza wa kila jambo. Nitumie fursa hii kwa dhati ya moyo wangu kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa walizozifanya katika kipindi hiki chote cha uongozi wao. Mengi yametajwa. Mambo makubwa yamefanyika; yote hayo ni mafanikio ya Serikali yetu ya Awamu ya Sita na Awamu ya Nane ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upekee kabisa ninatoa pongezi za dhati sana kwa Serikali yetu katika Sekta ya Muungano. Tunaona na tunaelewa wote kwamba Muungano ni miongoni mwa tunu kuu za nchi yetu ambayo ni urithi kutoka kwa Baba yetu wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dkt. Samia Suluhu Hassan na timu yake ya Serikali pamoja na Mawaziri wote waliokuwa katika Sekta ya Muungano wameweza kuimarisha na kuudumisha Muungano kwa namna ya kipekee katika kipindi hiki. Wakati wanaingia madarakani kulikuwa na hoja 18 za Muungano ambazo zilikuwa hazikufanyiwa kazi, lakini ndani ya kipindi kimoja cha mwaka 2021/2022 hoja 11 za Muungano ambazo zilikuwa ni kero ziliweza kufanyiwa kazi ndani ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi tunazungumza mwaka jana 2024 katika hizo hoja 18, hoja 15 tayari zimepatiwa ufumbuzi. Hili ni jambo la kujivunia kwa sababu Muungano wetu ndio umoja wetu na ndiyo amani yetu. Hayo mengine yote yanayofanyika yanayoleta maendeleo katika Taifa letu bila umoja na amani vilivyopo tusingeweza kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze kwa dhati ya moyo wangu namna ambavyo Serikali imeweza kuimarisha Muungano kwa namna hii. Hizo hoja tatu ambazo zimebaki nina imani kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais kwa sababu ya uzoefu wake mkubwa alionao katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kipindi cha miaka 10 na vilevile akiwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais Tanzania kwa muda wa miaka mitano na pia Makamu wa Rais na sasa ni Rais, ninaamini kabisa kwamba tukimwongezea miaka mitano yeye na Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Muungano wetu utakuwa imara kuliko tunavyofikiria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, leo sitozungumzia kuhusu udhalilishaji wa watoto wala suala la madawa ya kulevya. Nimepata wasemaji wengi kuanzia Bunge la Kumi na Moja hadi sasa wakiwemo askari wamepaza sauti zao, kazi inafanyika, lakini bado changamoto ipo. Ninaomba Serikali iendelee kufuatilia, hasa suala la madawa ya kulevya. Ninashauri sana Serikali tukazane na wale ambao wanaleta na kuuza na siyo watumiaji wa chini kabisa. Huo ni ushauri wangu kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo kubwa la ushauri wangu kwa Serikali nitaanza kwenye suala la kujitegemea, dhana ambayo imetoka kwa mwasisi wetu wa Taifa letu. Dhana ya kujitegemea haitakiwi kwenda kwenye Serikali peke yake, inaanza na wazazi na walezi. Tunapowapa watoto elimu, tunapokuwa tayari kupoteza gharama kubwa kuwasomesha watoto wetu mpaka vyuo vikuu tusitegemee kwamba wale ndio watakaoleta utajiri katika familia zetu. Dhana hiyo tuiondoe katika vichwa vya Watanzania. Elimu ndio ufunguo wa maisha, elimu ni kuondoa ujinga na elimu ndiyo itakayotuwezesha kufanya kazi ya kuweza kujiletea maendeleo katika Taifa letu, lakini si kigezo pekee cha kuleta utajiri katika familia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili tuweze kwenda na maendeleo ya sasa ni lazima dhana hii ya kujitegemea iwe katika vichwa vya Watanzania. Kwa upande wa Serikali ninaomba nishauri na ninaomba nirudi kwenye maeneo mengi ambayo watu wameshauri, ambayo pia ni urithi wa mababu na mababu zetu; kilimo, ufugaji na uvuvi inaimbwa kila siku ni mali ambayo tunayo na itaendelea kuwepo Tanzania haitokwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuweka mazingira wezeshi vijana wetu hawatokithamini kilimo, hawatouthamini ufugaji wala hawatouthamini uvuvi. Kwa hiyo Serikali tuna wajibu wa kuweka mazingira rafiki. Kwanza Wizara ya Ardhi; nipo mwenyewe kule Makamu Mwenyekiti, ninawashukuru sana kwa kazi inayoendelea kufanyika, lakini lazima tuweke mazingira na maeneo maalum kwa ajili ya wafugaji pamoja na wakulima; kila mmoja ajue yuko katika eneo gani ili migogoro iondoke. Migogoro itakapoondoka tutaweza kufika mahali ambapo tunataka kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo ni ushauri wangu kwa Serikali; tuna vijana wengi wako maeneo ya nje ya miji; wengine wamesoma na wengine hawakusoma sana. Bila kuwapa mazingira rafiki ya kuwatafutia masoko kwa mali zinazopatikana katika eneo husika kwa kuwawekea viwanda vya kuchakata mali au malighafi za mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi hatutoweza kuwashawishi vijana wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunaweza kutengeneza miradi mikubwa katika nchi yetu ya mabilioni tunashindwaje kuwezesha maeneo yanayoweza kufikika kwa kutengeneza viwanda vya kutengeneza juice? Tuna matunda mengi katika nchi yetu, tuna samaki wa aina nyingi katika maziwa na bahari zetu, au bahari yetu na mito mingine. Tunashindwaje kuwa na viwanda? Tunaagizia samaki wa makopo wanauzwa shoppers au madukani mengine, tunashindwa sisi wenyewe kuwanavyo. Kwa hiyo ninaomba sana Serikali, hata kama sisi wenyewe kama Serikali tutaona kuwa bado hali ngumu tutafute wawekezaji ili waweze kuja kufanya kazi hiyo; tuwawekee mazingira rafiki, tusiwawekee mlolongo wa mambo mengi na masharti ambayo yatawashinda waende nchi za jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mifugo mingi sana ambayo inatakiwa nje ya nchi, lakini tukiwa na masharti magumu ambayo hayana tija kwa Taifa letu wananchi wetu watashindwa kufanya kazi ya ufugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo eneo hilo tu, eneo la madini, Sekta ya Madini, ni sekta kubwa; na hii sekta tukiweza kuifuatilia tunasafirisha madini yetu ya dhahabu yanakwenda nchi nyingine. Kule wanachakata wanarudisha Tanzania tunakuja kuvaa wanawake ili turembeke, Hilo ni jambo ambalo Serikali yetu inapaswa kulitafakari. Kama sisi hatuwezi tumtafute mwekezaji kutoka Dubai aje hapa afungue kiwanda atengeneze malighafi ili tuweze kupata kutumia nchini kwetu, huo ni ushauri wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, mpaka sasa hivi ninaamini kabisa kwamba tukiwa na dhamira njema ya kutaka kuisaidia nchi yetu ni lazima turudi kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi. Taifa letu lina eneo kubwa sana kuliko nchi zote za Afrika Mashariki, Taifa letu lina eneo lenye rutuba, lina wanyama wa kutosha ukiacha mbali na Sekta ya Utalii ambayo ni hazina kubwa ambayo tumeachiwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, ninaiomba sana Serikali iweze kufikiria zaidi njia mbadala ya dhana ya kujitegemea ili vijana wetu waondokane na changamoto ya ajira. Hakuna hata Serikali moja duniani inayoweza kuwasomesha watoto wake wote na kuwapa kazi za Serikali. Hiyo tusijidanganye na haitowezekana, kwa sababu nafasi za Serikali ni chache kuliko wananchi wanaotegemea kupata ajira. Bila ya kurudi kwenye dhana ya kujitegemea ya Baba wa Taifa hatuwezi kuondoa changamoto ya ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ninawaombea kila la kheri Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Ninawaomba Watanzania tuendelee kuwaunga mkono ili mwaka huu warudi tena kwa ajili ya kuendeleza mazuri waliyoyafanya na kuendelea ushauri wetu. Ahsante sana. (Makofi)