Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na ninaungana na wenzangu kwa kukupongeza kuendelea kufanya kazi hiyo ya kuongoza Bunge letu kwa weledi na Mungu aendelee kukuangazia katika kila hatua zako na uchaguliwe kwa nyingi tena na wananchi wa jimbo lako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuanza mchango wangu ningependa kuitumia nafasi hii kama Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kutoa pole kwa Waziri wa Nishati na Serikali kwa ujumla kwa kumpoteza mwanamapinduzi na mfanyakazi hodari ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufuatia ajali ya gari iliyotokea. Mungu aweke roho ya marehemu mahali pema peponi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia nafasi hiyo ninampongeza Mheshimiwa Spika wetu kwa busara zake. Ametuelekeza na Mwenyekiti wetu sasa yuko njiani kwenda kushiriki mazishi ya kiongozi huyo kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na kwa niaba ya Bunge zima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii nyeti, ambayo ni Ofisi ya Waziri Mkuu inayokusanya taasisi nyingi na muhimu katika utendaji kazi na ambayo ndiyo Wizara inayosimamia kazi za Mawaziri wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kabla ya kuanza nichukue nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kusimamia vizuri uongozi wa nchi yetu na kumfanya Waziri Mkuu wake kuendelea kusimamia kazi za Serikali na za Mawaziri wote na kuweza kuleta tija kubwa sana katika maendeleo ya Watanzania. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ningependa nitumie nafasi hii pia kumpongeza Waziri Mkuu mwenyewe na Naibu Waziri Mkuu kama msaidizi wake wa karibu kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya; na sisi Wabunge tumekuwa ni mashahidi wa viongozi hawa kuwa viongozi wa mfano kwa tabia njema na kuwa mfano wa kuigwa katika kazi yao ya uongozi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaanza shughuli za Bunge niliji-address kama Mbunge ninayepiga vita sana riba kubwa katika mabenki na suala la mikopo ya kausha damu. Nilisema maneno haya kila eneo nilipokwenda na hapa Bungeni nilizungumza kwa kiasi kikubwa. Ningependa kuitumia nafasi ya leo kuishukuru Serikali; sauti yangu niliyopaza kwa kiasi wameisikiliza na hatua kadhaa zimechukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninazungumza riba za mabenki zilikuwa kati ya 16% mpaka 23%, leo riba za mabenki ziko kati ya 14% mpaka asilimia 21%. Kuna kiasi cha mafanikio ambayo tumeyapata katika kupaza sauti. Hata hivyo, leo ninasimama kuiomba tena Serikali kwamba bado na ninaiomba Serikali wakati na Serikali yenyewe mara nyingi ninaisikia ikilalamika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewahi kumsikia Mheshimiwa Waziri Bashe, Waziri wa Kilimo akisisitiza kuzitaka benki ziwakopeshe wakulima kwa single digit, maana yake kuanzia asilimia tisa kushuka chini. Nimepata kuwasikia viongozi mbalimbali wa Serikali wakizungumzia jinsi wanavyoona riba za benki zilivyo na athari kwa maendeleo ya wafanyabiashara na wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninataka sisitize tena kwamba bado Serikali ina kazi ya kujielekeza katika kuhakikisha kuwa riba za benki zinashuka. Katika jambo hili sijui mgogoro unatoka wapi? Kila ukiuliza unaambiwa kuwa hatutaki ku-disturb uchumi, tumewaacha benki ziwe huria. Sidhani kama hoja hii inakubalika. Uhuria huu unatoka wapi? Kwenye maji, kwenye umeme, kwenye nishati nyingine tumeweka EWURA kuwa regulatory authority ya kusimamia bei za mafuta, kwani kwenye mafuta hakuna wafanyabiashara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbona wafanyabiashara wa mafuta tunawapangia bei na wana-survive? Kwa nini benki tusizipangie riba zika-survive? Kwenye insurance tumeweka TIRA (Tanzania Insurance Regulatory Authority) ili kuhakikisha kwamba viwango vya bima vinasimamiwa, kwamba mtu asijipangie mwenyewe viwango vya bima; mbona hakuna kampuni za bima zinazotetereka? Kwa nini benki hatutaki kuziwekea mwongozo maalum wa riba? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo ambapo Benki Kuu haitaki kutoa mwongozo wa riba inatoa mwongozo wa miamala. Imeweka viwango maalum vya kulipa kama ada ya miamala; sasa, inashindwa nini kuweka viwango maalum vya kulipa kama riba? Jambo hili limeathiri sana uchumi wa Watanzania, wafanyabiashara wengi wameumia na wengine wametoka katika mkondo wa biashara. Huku Serikalini wanachelewa kulipwa madai yao, huku benki zinaendelea kuwahesabia riba kubwa. Kwa hiyo, ninasimama tena kupaza sauti kuitaka Serikali ifike mahali iamue na kuhakikisha kwamba kwenye suala la riba inaipa nguvu Benki Kuu ili iwe na viwango elekezi vya riba kwa benki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni hili la hizi microfinances ambalo nimekuwa nikilizungumzia. Ninataka niipongeze sana Serikali na BOT kwa sababu wamefunga microfinances nyingi ambazo zilionekana kwa kweli zimekuwa mzigo mkubwa kwa Watanzania hata hivyo kazi bado. Nitatoa mfano, microfinance inakwenda kukopa kwenye benki mkopo ambao riba yake ni 14%, 15%, 16%, 17% na 18%, lakini riba hii inahesabiwa kwa mwaka. Wao wanamkopesha mfanyabiashara mdogo kwa riba ya 10% hadi 20% kwa mwezi. Kwa maana nyingine ni kwamba ukii-calculate kwa mwaka ni kama hawa wafanyabiashara wadogo wanaenda kutozwa riba ya 240% hadi 120% huu ni mzigo mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bado ninaitaka Serikali ihakikishe kwamba inaipatia nguvu kubwa BOT ili iendelee kusimamia hizi microfinances nazo ziwekewe viwango vya riba ambavyo ni himilivu kwa wafanyabiashara hawa wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ninaomba nimalizie ni suala la leseni za madereva wa bodaboda. Tumesema hapa, tunaishukuru Serikali, tulizungumza tukaieleza kwamba haiwezekani malipo ya faini ya makosa ya barabarani ya gari na pikipiki yawe sawasawa. Serikali hii sikivu ya Mama Samia Suluhu Hassan, ikateremsha kutoka shilingi 30,000 ikaleta shilingi 10,000 kwa makosa ya pikipiki ya barabarani, ninashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado pia tuna tatizo la leseni na nilisema hapa kwenye Bunge hili kwamba, mpaka leo hatuna leseni za waendesha pikipiki. Driving license ni kwa ajili ya magari lakini tunatakiwa tuwe na riding license kwa ajili ya waendesha pikipiki na hii iwe shilingi 20,000. Sasa hivi inakadiriwa tuna bodaboda 2,000,000 zinazofanya kazi, lakini kati ya hawa bodaboda 2,000,000 ni kama 15% ya waendeshaji wa bodaboda ndio wana leseni. Wengine 85% hawana leseni kwa sababu imekuwa ni mzigo kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali ishushe hizi leseni za bodaboda kutoka hiyo shilingi 70,000 hadi shilingi 20,000. Hawa 85% wakilipa ambao ni kama madereva bodaboda 1,700,000 tunaweza tukaingiza shilingi bilioni 34 za Kitanzania kwenye Mfuko wa Hazina ya Serikali. Tusing’ang’anie kiwango kikubwa ambacho hakikusanywi, tunaacha kuweka kiwango kidogo ambacho tutakusanya kwa wingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaendelea kuipongeza sana Serikali na ninaunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)