Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Boniphace Nyangindu Butondo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili kutoa mchango wangu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo kimsingi inabeba mambo makubwa. Kama tunavyofahamu Ofisi ya Waziri Mkuu kimsingi ndiyo ofisi inayoshughulikia masuala ya kila siku ama majukumu ya Serikali kama majukumu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kwanza kwa kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo anavyoiendesha vizuri na hasa katika mafanikio ya kimaendeleo nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sote kwa pamoja tunakiri kwamba, mabadiliko yapo makubwa ya kimaendeleo na hasa katika eneo la miradi yetu ya kimikakati ambayo inakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunaona SGR maendeleo yake ni mazuri na sasa imeanza kutoa huduma na bahati nzuri miradi katika maeneo ambayo kuna mikataba zaidi ya tisa inaendelea kutekelezwa katika nchi hii. Bahati nzuri si miradi hiyo tu, kwa pamoja na miradi mingine Mradi wa REA na ujenzi wa Daraja la Busisi. Hii ni moja kati ya miradi mikubwa ambayo inaendelea katika nchi yetu. Vilevile, Bwawa la Mwalimu Nyerere sote ni mashahidi kwamba lipo katika hatua ya mwisho kabisa na bahati nzuri sasa tunapata huduma ya umeme ambayo ilikuwa ni adha na kero kwa wananchi katika ubora unaotakiwa, kukatika umeme na mambo mengine hakupo tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi pia hii ya REA imekwenda vizuri, nchi nzima sasa inawaka na jitihada kubwa inaendelea kuhakikisha kwamba Serikali yetu inaanza kusambaza umeme katika ngazi ya vitongoji, ilimradi wananchi waendelee kupata hii huduma ya umeme ambayo ni muhimu sana katika kuchachusha maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo kwa kweli amekuwa akifanya kazi kubwa ya kuhakikisha anaisimamia Serikali vizuri na hasa shughuli za kila siku za Serikali. Tumeshuhudia ziara zake katika mikoa mbalimbali, lakini ufuatiliaji wa utekelezaji wa ilani, anafanya kazi kubwa sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Haya yote kwa kweli tunasema Mwenyezi Mungu aendelee kumpatia afya njema ilimradi mambo yaende kufanyika vizuri katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Lukuvi na Mheshimiwa Ridhiwani pamoja na Manaibu Mawaziri wao wote kwa namna ambavyo wanamsaidia sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nianze mchango wangu hasa katika eneo la vita dhidi ya madawa ya kulevya. Tunaye Kamishna Jenerali Lyimo ambaye kwa kweli ninaomba nitumie fursa hii kwanza kumpongeza kwa namna ya moyo wa uzalendo mkubwa anaouonesha kwa Taifa letu na Watanzania kwa ujumla. Kamishna Jenerali Lyimo ni Kamishna ambaye ambaye kwa kweli anatekeleza majukumu yake kabisa kwa usahihi chini ya Waziri Lukuvi; tunaona namna ambavyo anatoa ushirikiano mkubwa lakini tunaona matokeo chanya katika eneo hili la kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo suala zima la kuingiza madawa ya kulevya katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote ni mashahidi kwamba, tumeshuhudia kilo nyingi za dawa zikikamatwa katika hii Nchi yetu ya Tanzania hasa katika viwanja vyetu vya ndege na mipaka ya nchi yetu, jitihada ambazo zinafanyika ni kubwa sana. Tunaona jitihada kubwa inayofanyika katika uteketezaji wa mashamba makubwa ya bangi unaofanyika katika nchi yetu hii. Bahati nzuri katika kila hatua anayokuwa anaifanya amekuwa wazi kabisa na kwamba amekuwa akionesha Watanzania namna gani jitihada hizi zinafanyika pamoja na kuonesha rekodi zote na namna ambavyo Serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha kwamba mtandao huu wa dawa za kulevya unashughulikiwa kwa karibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiona shughuli nzima ya urekebu ikiwa inafanyika katika nchi hii. Pamoja na kwamba tumekuwa na waathirika kadhaa wa dawa za kulevya, chini ya Jenerali Lyimo upo usimamizi wa karibu sana kuona kwamba hawa waathirika wa dawa hizi wanapata huduma ipasavyo katika maeneo mbalimbali. Hii tumekuwa tukiona katika Jiji letu la Arusha, Dar es Salaam na hata hapa Dodoma. Jitihada ni kubwa kuhakikisha kwamba urekebu unafanyika kwa karibu sana, ili kuona kwamba jamii hii iliyokuwa imeangamia na dawa za kulevya inarejea na kuanza kuungana na wanajamii wengine kutekeleza majukumu ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa sababu tumekuwa tukitenga fedha katika eneo hili ili kuona kwamba wananchi hawa wanarudishwa katika hali yao ya kawaida, lakini wakati huohuo wakiwa katika urejeshwaji wa hali ya kawaida. Pia, zimekuwa zikitengwa fedha kwa ajili ya kuhakikisha tunawawezesha walau waweze kufanya majukumu yao wale walio na fani mbalimbali katika maeneo hayo ambayo urekebu umekuwa ukifanyika. Jitihada hizi kubwa zinazofanyika hatuna budi kwa kweli kumpongeza sana Jenerali Lyimo na Wizara kiujumla kwa namna ambavyo imekuwa ikiratibu mambo haya, na shughuli hizi zimekwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu nitoe mfano mdogo sana. Tumeweza kwa ujumla kukamata kilogramu milioni 4.3, ambazo zimekamatwa katika kipindi cha miaka miwili tu (2023 na 2024). Hii ni zaidi ya mara sita ya kiasi hicho kilichokamatwa katika mwaka 2021 na mwaka 2022. Unaweza ukaona ni jitihada kubwa ambazo kwa kweli idara hii imekuwa ikifanya kazi kubwa sana ya kuvunja mtandao mkubwa ambao umekuwa ukiingiza haya dawa ya kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada zinafanyika hapa kubwa sana. Tumeshuhudia mapapa na wafanyabiashara nguli wakubwa wakikamatwa badala ya kukamata vidagaa. Hii ni jitihada kubwa ambayo ni lazima tumpongeze Jenerali Lyimo kwa sababu anafanya kazi ya kiuzalendo kabisa. Tumeshuhudia jitihada hizi kubwa zikifanyika na sisi tunashukuru. Kama Kamati kwa kweli hili tuliliona na tunamtakia kila la kheri aendelee kufanya kazi kubwa kwa ajili ya kuwaokoa Watanzania ambao wamekuwa wakiathirika pakubwa sana na dawa za kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, operesheni kubwa hizi zimekuwa zikifanyika maeneo mbalimbali hata katika maeneo yetu ya mashamba ya bangi hasa kule Mara zaidi ya ekari 4,733 zimeteketezwa, hii ni hatua kubwa sana. Haya maeneo makubwa hasa ni huko Mkoa wa Mara pamoja na kule Morogoro. Hivi tumekuwa tukiyashuhudia mambo haya live kabisa katika vyombo mbalimbali vya habari. Hizi ni jitihada kubwa ambazo zimekuwa zikifanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala kubwa vilevile ambalo limekuwa likifanyika pakubwa sana la kuhakikisha jitihada zinatolewa hasa katika maeneo maalum ya mipakani na airport. Hizi ni jitihada kubwa ambazo zimekuwa zikifanyika na ndiyo maana sisi kama Kamati tumekubaliana kwamba ni lazima waongezewe fedha na zitolewe kwa wakati, ilimradi waweze kupata vifaa vya kisasa na hasa maeneo yale ya mipakani, waweze kufanya kazi vizuri. Kwa sababu kama hawana vifaa vya kuchunguza, kupembua na kuona wale watu wanaovuka na wanaoingia kwamba, wanatoka na nini na wanaingia na nini? Hatuwezi tukafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii pamoja na kuongeza bajeti yao ambayo imeenda takribani mara mbili katika upande wa maendeleo na OC, itakwenda kusaidia sana wafanyakazi waongeze ari na wafanye kazi ya doria vizuri, ilimradi kazi hii iendelee kufanyika sawasawa. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa ajili ya usalama wa nchi yetu, tunaomba sana Idara hii itazamwe kwa macho mawili, ili operesheni na kazi kubwa inayoweza kufanyika iende kukamilishwa inavyopaswa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nielekee eneo la miradi ya kimaendeleo ambayo imefanyika katika Jimbo la Kishapu. Ninashukuru sana Serikali yetu imetoa fedha nyingi sana Sekta ya Elimu, Afya, Miundombinu, Barabara na Maji, ni hatua kubwa sana iliyofanyika. Nitoe mfano tu, Wilaya ya Kishapu wakati ninaingia kuwa Mbunge mwaka 2020 ni kata nne peke yake zilikuwa zimepata maji safi na salama, lakini hivi ninavyozungumza kata 21 zinapata maji safi na salama. Hii ni kutokana na vyanzo mbalimbali, maji ya Ziwa Victoria kata 17, pia kata karibu sita zinapata maji kutokana na vyanzo vingine vya visima virefu na mito tuliyonayo. Hii ni jitihada kubwa sana ya Serikali na hasa ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Aweso kwa namna ambavyo ananipatia ushirikiano katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo machache ambayo yapo katika Tarafa ya Mondo yanahitaji maji na sehemu kame ni kubwa sana. Kata ya Mondo, Sekebugolo, Busangwa na Mwasubi, hizi ni kata ambazo zinahitaji huduma ya haraka ya maji na ninafurahi kwa sababu kuna bomba kubwa linalotoka Mwanza na kupita katika Wilaya ya Kishapu ambalo litagusa Tarafa hii ya Mondo. Nina hakika kwamba sasa kata hizi zitakwenda kupata huduma ya maji haraka iwezekanavyo. Ninaiomba Serikali wakati wa zoezi hilo ikumbuke kuweka matoleo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kata hizo zinapata huduma kwa sababu zipo ndani ya kilometa 12. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali kwa sababu barabara sasa katika Wilaya ya Kishapu zimeshafunguliwa vizuri, kata zote zinapitika. Yapo maeneo machache sana ambayo yamebaki yana changamoto, lakini tumepata fedha zaidi, kila mwaka tumekuwa tukipata shilingi bilioni 2.5. Ukilinganisha na kipindi cha nyuma, tulikuwa tukipata shilingi milioni 900 mpaka 950. Hizi ni jitihada kubwa sana za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niwaambie Watanzania na hasa wananchi wa Jimbo la Kishapu, Mama Samia tunaye na tunatamba naye. Ninaomba sana Watanzania tubaki na imani na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. Huyu mama atatuvusha, kwa sababu kazi anayofanya ni kubwa na ninaomba Watanzania miaka mitano inayokuja tumpe nafasi tena Rais wetu aendelee kupeperusha bendera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)