Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Liwale
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru wewe binafsi kwa kunipatia nafasi asubuhi hii ya leo niweze kutoa mchango wangu kwenye hii Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hii hotuba nzuri. Siyo hotuba peke yake na kazi kuwa anayoifanya kwa Taifa hili. Kwa nafasi yake kama Waziri Mkuu tunayo kila sababu ya kumpongeza na kumshukuru kwa namna anavyolitendea wema Taifa hili kwa nafasi yake kama Waziri Mkuu. Ninasema hili si kwa sababu tu ni Waziri ambaye ametoka Mkoa wa Lindi, lakini nyote humu ndani ni mashahidi kwamba, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli anafanya kazi inayotukuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba hii ninaomba nianze na Wizara ya Ujenzi. Kwenye Wizara ya Ujenzi ninaomba nianze na sera ya kuunganisha mikoa kwa barabara either ziwe za lami au changarawe. Huko nyuma nilishawahi kusema kama sera hii imekuwa ngumu kutekelezeka basi ni bora tuiondoe kwenye makaratasi kwa sababu mpaka leo hii Mkoa wa Lindi bado haujaunganishwa na Mkoa wa Morogoro. Hapa ninapotaka kuongea mwelewe kwamba Barabara ya Morogoro ninayoizungumza kwa kweli kama ingechukuliwa hatua ingekuwa ni barabara ya ukombozi kwa hali kama hii tuliyonayo leo Barabara yetu ya Kibiti – Lindi inavyoendelea kutusumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Watu wa Lindi na Mtwara wanaambiwa watoke Lindi, Songea, Njombe, Iringa, Morogoro, Pwani ndio wafike Dar es Salaam au waende Dodoma. Barabara ile ya Morogoro – Lindi ingetengenezwa ina maana mtu wa Lindi na Mtwara angepita Morogoro – Pwani yupo Dar es Salaam, ina maana inaingia mikoa miwili tu. Barabara hii kwanza siyo tu inapunguza gharama kwa watumiaji, lakini hata kwa Serikali kutumia mafuta kutoka Lindi – Songea – Njombe – Iringa – Morogoro – Pwani mpaka Dar es Salaam au Dodoma gharama ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuliko tungetoka tu Lindi unakuja Morogoro unakuja hapa Dumila upo Dodoma. Kwa hiyo, Wizara waone umuhimu wa back up ya hii barabara badala ya kutumia hiyo barabara ndefu ambayo kila siku tunaizungumza. Ninapoisema hii Barabara ya Morogoro sina maana kwamba nimeridhika sana na kile kizungumkuti cha ile Barabara yetu ya Nangurukuru – Liwale na Nachingwea – Liwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa napo ninaomba niipongeze Serikali kwa kuonesha nia angalau tupate hizo kilometa 10 za Barabara yetu ya Nangurukuru – Liwale na kilometa 50 ile ya Nachingwea. Kwa hiyo, kwa jambo hilo ninapendelea kuipongeza sana Serikali na iwe hivyo. Vilevile, Barabara ya Mogororo ni barabara muhimu sana kama umuhimu huo niliouonesha hapo nilivyoizungumzia hiyo barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niende upande wa TARURA. Kwa kweli katika taasisi tano au 10 katika nchi yetu ni TARURA. Shida kubwa ya taasisi hii ya TARURA ni upelekeji wa fedha. Mimi kama nipo sawasawa zipo fedha ambazo zimetengwa Kizungu wanaita ring fenced, lakini hizo fedha nazo mbona haziendi huko TARURA? Kwa sababu miradi mingi ya TARURA imekwama kwa sababu ya fedha. Leo hii TARURA wanadaiwa kila kona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi wa Liwale nilijaribu kumwuliza Mtendaji Mkuu wa TARURA na watumishi wengine; hivi ni wilaya gani ambayo ina barabara chache sana za lami kwenye nchi hii? Ndugu zangu, Liwale kama siyo ya kwanza basi ni ya pili kwa uchache wa barabara za lami, maana sisi tuna kilometa tatu tu za lami pale mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali ilione hili. Tunaposema walione hili, wawapelekee fedha TARURA waweze kutekeleza yale ambayo wameahidi. Niseme tu ukweli, Meneja wa TARURA Wilaya ya Liwale ni mtu msikivu, mwaminifu, na mchapakazi sana. Kila mipango tunayopanga, tunapanga naye, lakini tatizo linakuja kwenye fedha, hana fedha za kutosha. Kwa hiyo, ninaomba Serikali walione hili watuongezee fedha, TARURA wapate fedha ili waweze kutukwamua sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa hizo barabara ni mkubwa sana. Hizi barabara ndizo zinazotoa mazao haya ya wakulima kupeleka sokoni. Maana tukizungumzia Barabara za TARURA mnaweza mkazipuuza, mkaziona tu ni barabara ambazo zina umuhimu mdogo; hapana. Hizi barabara ndizo zinazotoa mazao ya wakulima kutoka mashambani kupeleka sokoni. Sasa, kama hizi barabara haziko sawa sawa, maana yake mazao ya wakulima yatakuwa hayawezi kufika sokoni na mazao ya wakulima yasipofika sokoni maana yake uchumi wa wakulima hawa utakwenda kuharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo ninaomba nijihamishe niende kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii. 60% ya ardhi ya Liwale inazungukwa na Hifadhi ya Selous pamoja na Hifadhi ya Mwalimu Nyerere. Suala la wanyamapori limekuwa ni kitendawili kisichopata majibu. Juzi nilizungumza hapa kwamba tumeshapotea zaidi ya watu wanne ndani ya mwezi mmoja. Kuanzia tarehe 20 mwezi uliopita mpaka tarehe 11 mwezi huu tumeshapoteza watu wanne ambao wamepoteza maisha kwa ajili ya kadhia ya wanyama (tembo).
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuatilia, nimejaribu kuzungumza na Wahifadhi, wanasema hawa tembo mahali walikozalia wanaona kama ndiyo nyumbani. Sasa, ninaomba nitoe taarifa kwamba tembo sasa wanazalia kwenye mashamba yetu. Sasa, sijui tuseme ndiyo wamehamia! Maana wanasema kwamba hawa wanyama wanapozalia ndiyo wanaona kama nyumbani. Sasa, tembo wa Liwale wanazalia kwenye mashamba yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ninaomba ndugu zangu wa Hifadhi, hebu jaribuni kuongeza juhudi. Mnawahamishaje hawa tembo hapa walikozalia? Kwa sababu mnasema hapa walikozalia hawa tembo wamefanya kama nyumbani kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo ninaliona pale, pamoja na kwamba juhudi kubwa za Serikali zinafanywa kusogeza tembo hawa Hifadhini, lakini wako watumishi wa TAWA na TANAPA siyo waaminifu. Wanaruhusu mifugo kupita kwenye hifadhi zetu. Liwale ni miongoni mwa maeneo ambayo tunapokea wafugaji, lakini inawezekanaje leo mifugo itoke Iringa, itoke Mbeya, itoke Morogoro, ifike Liwale kwa njia ya miguu? Maana yake wanapita Hifadhini. Wanawezaje kupita Hifadhini bila kuonekana na hawa askari?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini? Kwamba, sasa tembo wanaondoka hifadhini wanakimbia hawa mifugo, matokeo yake wanakuja kutubughudhi sisi. Ninaoimba Serikali idhibiti sana hawa watumishi ambao siyo waaminifu, ambao wanapitisha ng’ombe kwenye Hifadhi, matokeo yake ng’ombe wanakuja kutudhuru sisi kule kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni vitendeakazi. Vitendeakazi ni vichache mno. Sisi Liwale 60% kama nilivyosema, tunahitaji kuwa na askari wengi. Kwa sababu leo unapata ripoti tembo wametokea Ngongowele, askari wanakwenda, kesho wametokea Ndapata, askari wanatakiwa waende. Hao askari wenyewe ni wachache. Unakwenda pale hifadhini wanakwambia gari imeondoka imekwenda kijiji fulani au hatuna gari au mafuta hatuna. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali kuongeza vifaa vya kutendea kazi kuhakikisha kuwadhibiti hawa wanyama (tembo).
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwenye hili ni kuhusu kifuta machozi. Wilaya ya Liwale mara ya mwisho kupata kifuta machozi ni mwaka 2022. Kwa hiyo, kuanzia mwaka 2022, mwaka 2023, mwaka 2024 na leo mwaka 2025, wananchi wale waliopata madhara ya tembo bado hawajapata kitu kinachoitwa kifuta machozi. Japokuwa kifuta machozi chenyewe bado nacho ni kidogo, lakini bado tunadai kifuta machozi, bado hakijawafikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nishati (TANESCO). Sisi kule kwetu zamani ilikuwa umeme ukiwaka watu wanashangilia au wanashtuka. Sasa hivi kule kwetu sisi umeme ukiwaka ndiyo watu wanashangaa, kwa sababu mara nyingi tunakuwa gizani. Kwa hiyo, ninaendelea kuwaomba na nilishawahi kuongea hapa kwamba, shida kubwa ambayo tunaipata umeme kutoka Mahumbika mpaka Liwale, umbali ule ni mrefu. Tunaomba mtuongezee kituo cha kupoozea umeme pale Liwale au hata Nachingwea, ili tuweze kupata umeme huu kwa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulienda Mtwara wakatuambia kwamba kuna mashine imepelekwa kutoka Ubungo kwenda Mtwara megawati 20 na mahitaji ya Mkoa wa Lindi na Mtwara ni Megawati 18. Bado mashine ile pamoja na kwamba imefungwa, bado upatikanaji wa umeme kwa Mkoa wa Lindi na Mtwara bado ni kitendawili. Tunaomba sana Serikali muone namna ya kutuwezesha sisi watu wa Mkoa wa Lindi kutuingiza kwenye Gridi ya Taifa, ili sisi wote tufaidi keki ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, ninaunga mkono hoja na ninakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)