Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza ninachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri aliyoifanya katika nchi yetu. Ninampongeza Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imegusa kila eneo, na ninawapongeza pia Mawaziri wake wote na Manaibu wake wote na watendaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze katika Sekta ya Kilimo. Ninamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Bashe na Naibu wake Mheshimiwa Silinde. Kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Bashe kwa kukubali taarifa ya ukusanyaji upya wa data za wakulima katika Mikoa ya Kusini, lakini pia ninampongeza kwa ugawaji wa pembejeo. Kwa sasa hivi zimeanza kuingia katika Wilaya ya Masasi, hivyo zimefika wakati muafaka na tumeenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamkumbusha pia, Mheshimiwa Bashe katika Kilimo cha Korosho, mauzo yanapoanza Jimbo la Lulindi huwa ni la kwanza kupeleka mazao katika ghala, lakini malipo yanachelewa. Inafika mpaka mwezi Januari wengine hawajalipwa, wanashindwa kupeleka watoto shule wakisubiri ada. Ninaomba malipo ya korosho katika Jimbo la Lulindi yalipwe mapema sambamba na upelekaji wa zao hilo katika ghala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nizungumzie kwenye Sekta ya Maji; ninachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Aweso na Naibu wake Mheshimiwa Kundo, kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Sekta nzima ya Maji. Kuna changamoto chache ambazo ninapenda kuzielezea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, katika chanzo cha maji Lupaso; chanzo kile kimekufa katika Kata ya Lupaso ndani ya Jimbo la Lulindi. Maji yanatoka mara moja tu, yalitoka mwaka mmoja tu hayajatoka mpaka sasa hivi. Tunaomba chanzo kile kirekebishwe ili wananchi wa maeneo yale waweze kunywa maji safi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia,chanzo cha maji kutoka Mto Ruvuma. Mradi huu unasuasua; maji yanatoka kwa mwezi mara moja na yanatoka kipindi cha kiangazi. Hiyo ni kero kubwa inayowagusa wananchi wa Vijiji vya Mapili, Chikoropora, Mkalivata, Chipingo, na Mnyonyo, ndani ya Jimbo la Lulindi. Ninaomba mradi huo utengenezwe vizuri, wananchi wa maeneo hayo waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maji hayo ninapenda kuzungumzia maji kutoka kwenye chanzo cha Kijiji cha Njechele kinachonufaisha katika Kata ya Namwanga, Vijiji vya Namwanga, Mkoropora, Chipango, Nakalola, Nakachindu, na katika Kata ya Mijelejele ndani ya Kijiji cha Mijelejele, Nambunda, Tupendane, Mpwapwa na Toleani. Maji haya yanatoka mara moja kwa wiki. Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea maji yao, lakini tunaomba yawekwe dawa kwa sababu maji yale yanakuja yakiwa na rangi ambayo inakatisha tamaa hata kunywa. Tunaomba maji hayo yawekwe dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumzie katika Sekta ya Barabara. Ninampongeza Mheshimiwa Ulega na Naibu wake Mheshimiwa Engineer Kasekenya kwa kazi nzuri wanayoifanya katika maeneo yote ndani ya barabara. Barabara za Jimbo la Lulindi zinapitika japo ni za vumbi, lakini kwa mwaka huwa zinakwanguliwa mara mbili au mara tatu, hivyo zinapitika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ni vivuko au madaraja. Kuna madaraja mengine yamejengwa pale kimtegomtengo tu, yaani ukifika unasimama unajiuliza nipite au nirudi? Kwa mfano Daraja la Mpindimbi – Kanyimbi – Nakalola; Daraja hilo limekaa kimtego, ukifika pale unajishauri nipite au nisipite? Tunaomba marekebisho yafanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Daraja la Nakachindu kwenda Kata ya Mkululu halipitiki. Kijiji cha Nakalola kwenda Kipango halipitiki, Kijiji cha Nakachindu kwenda Lulindi hakipitiki. Tunaomba maeneo hayo yafanyiwe marekebisho ya haraka. Tunaingia kwenye uchaguzi, tuna nafasi ya kupita kwenda kuomba kura za wananchi kwa ajili ya Mama Samia, nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa. Tunaomba watutengenezee barabara tuweze kupita kuomba kura kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie vile vile kwenye suala la Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Hapa ninampongeza Mheshimiwa Jerry na Mheshimiwa Maryprisca kwa kazi nzuri. Vijijini simu tunaziona, tunazitumia, lakini kuna maeneo ambayo yana changamoto. Kwa mfano, kwenye Kata ya Mnavira, Kata ya Lipumburu na Kata ya Sindano, ndani ya Jimbo la Lulindi; kata hizi ziko mpakani na Msumbiji. Kwa hiyo, ukitaka upate mawasiliano vizuri uchukue Mtandao wa Movitel kutoka Msumbiji, ambako ndiyo unaweza kupata mawasiliano vizuri, lakini ya kwetu haya hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Jerry shuka, ashuke aje Lulindi; ashuke aje aone watu wanavyoongea juu ya mikorosho, aje aone watu wanavyoongea kwenye vichuguu. Kwa hiyo, tunaomba sana yeye na Naibu wake waje Jimbo la Lulindi waangalie mawasiliano jinsi yanavyokwenda. Ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie Sekta ya Michezo. Kwenye Sekta ya Michezo ninampongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Palamagamba na Naibu wake Mheshimiwa Hamis Mwinjuma, alimaarufu Mwana FA. Sekta hii ninaipongeza sana. Nimeshuhudia wakienda mpaka kwenye mechi za mpira chandimu; wanaenda kuongea wakiwa wageni rasmi. Tunaomba nguvu hiyo isiishie hapa, waendelee kushuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafasi hiyo pia, ninaipeleka kwa Wabunge na Madiwani wote ambao wanafanya michezo katika maeneo yao. Ninafikiri Chama cha Mpira wa Michezo wa Miguu kinaona jinsi Madiwani na Wabunge wanavyofanya mashindano mbalimbali kwa gharama zao kwenye maeneo yao ili kuboresha mchezo huo. Sisi bado tuko tayari kuendelea na michezo hiyo mahali popote ilimradi tuibue na kukuza vipaji vya Mpira wa Miguu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ,ninaunga mkono hoja na ahsante. (Makofi)