Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi. Ninaomba na mimi nianze kwa kuanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kupata nafasi ya kuchangia, lakini ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na nguvu. Kipekee ninakupongeza Mheshimiwa Mwenyekiti kwa namna ambavyo unaendesha kikao chako leo. Ninaona tunakwenda kwa speed kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeonyesha mafanikio makubwa ya Serikali na kimsingi ninaomba nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali nzima kwa kazi nzuri ambayo Serikai inafanya, hasa katika maeneo mahususi ambayo nitakwenda kuyazungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeeleza namna ambavyo kazi mbalimbali zilivyoanza wakati Mheshimiwa Rais anachukua nafasi na namna ambavyo nyingine zimekamilika na nyingine zinaendelea. Kwa kifupi kabisa nizungumzie maeneo mawili ambayo mimi mwenyewe binafsi kama Mjumbe nimeshiriki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kwenye eneo la bwawa la umeme; mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini. Kazi kubwa sana imefanyika. Tulikwenda kule ikiwa 27%, tumekwenda ikiwa 98%, sasa hivi ukifika eneo lile unaweza ukafikiri umefika nje ya nchi. Tunaipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo imefanyika kwenye bwawa lenyewe, lakini kwenye maeneo ya miundombinu ambayo yanasafirisha umeme. Tumekwenda kwenye Kituo cha Chalinze na maeneo mengine ambapo line kubwa ya umeme inajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni eneo la Daraja la Kigongo – Busisi. Mimi ni sehemu ya Wabunge tulioomba sana Daraja lile lijengwe, kwa sababu wananchi wanaotoka Mikoa ya Kigoma, Geita na Kagera walikuwa wakifika pale wakakuta magugu maji yamejaa, wakakuta boti haipo, hata kama una mgonjwa anaweza akafia mikononi mwako unamwangalia ukiwa unampeleka Bugando. Kukamilika kwa Daraja hilo nii faraja kubwa kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa, lakini kutarahisisha biashara katika maeneo mbalimbali. Tunaipongeza sana Serikali kwa miradi hii pamoja na miradi mingine mingi ikiwemo ya reli, ikiwemo ya elimu na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ninataka kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Katika kipindi cha takribani miaka 10 ambayo nimekaa Bungeni, nilikuwa nikiomba sana Geita Mji iweze kupata manispaa. Nilikuwa ninaomba siyo kwa upendeleo, ni kwa sababu ya takwimu za mafanikio yaliyoko pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Geita kwa maana ya Geita Manispaa, tunakusanya takribani shilingi bilioni 20 kwa mwaka na ni moja ya halmashauri ambazo sehemu kubwa ya miradi ya maendeleo tunafadhili wenyewe. Pia, ni mji ambao tumeutengenezea Masterplan, tumeupanga na ni mji ambao unakua kwa kasi. Kwa hiyo, hoja yangu ya kuomba manispaa nilikuwa ninaomba nikiwa na takwimu, lakini na vigezo. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, kwa kulisimamia jambo hili na kuitangaza Geita kuwa Manispaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo dogo tu ambalo ninataka kuomba sehemu hii ni kwamba, baada ya Geita kuwa manispaa sasa tunaiomba Serikali ituongezee bajeti ya miundombinu. Kwa sababu, huwezi kuwa na manispaa ambayo ina barabara za lami chache na sehemu kubwa ni barabara za matope. Tunaomba sana Serikali kwenye eneo hilo iweze kutuangalia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo ninataka kuzungumza ni eneo la madini. Ninataka kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Madini na Serikali kwa ujumla. Kwenye takwimu inaonekana kwamba sasa madini yanachangia sehemu kubwa sana ya fedha za kigeni. Mchango huu haujaja wenyewe, umekuja kwa kazi kubwa iliyofanywa na Mawaziri na Serikali pamoja na Mawaziri waliotangulia. Kwa kweli sisi wananchi tuliotoka kwenye machimbo tunaona kabisa mchango wa Serikali kwenye kufanikisha mafanikio ya wachimbaji wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wachimbaji wadogo wadogo wanachangia zaidi ya 40% ya mauzo ya madini ambayo yanauzwa nje ya nchi. Siyo jambo dogo! Ninaipongeza Serikali kwa sababu imechukua hatua mahususi katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya eneo kubwa ambalo limefanya kazi kubwa ni kununua mitambo ya kuchoronga ili kurahisishia wachimbaji wadogo kuacha kuchimba kwa kubunibuni. Miaka ya nyuma huko tulikuwa tunasema ili mchimbaji mdogo aweze kujua hapa kuna dhahabu ama kuna kiasi gani, utamwona anakwenda kwa mganga wa kienyeji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ilipelekea mauaji mengi sana ya watu kwa sababu waganga wengi wa kienyeji walikuwa wanadanganya. Sasa tuna vifaa vya kuchoronga na tuna maabara nyingi nchini, kiasi kwamba wachimbaji wadogo wadogo wengi wanaweza kupata huduma hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee pia ninaipongeza Wizara hii kwa namna ambavyo miezi ya hivi karibuni baada ya mabadiliko ya maeneo mbalimbali, leseni nyingi ambazo zilikuwa hazifanyi kazi zilirudishwa na wamepewa wachimbaji wadogo wadogo. Katika Pori kubwa la Kigosi wachimbaji wadogo wadogo wamepata takribani leseni zaidi ya 2,000 na kuna nyingine zaidi ya 2,000 zinakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni kwamba, miaka michache ijayo uchumi wa madini Tanzania utakuwa ni uchumi mkubwa kuliko uchumi wa kitu kingine chochote kile. Sasa, hapa nina jambo ambalo ninataka Serikali inisaidie na inisikilize kwa makini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, Tanzania takribani katika kilometre square 945,000, tumefanya utafiti kwenye 16% tu. Kwenye lugha ya utafiti tunasema QDS (Quater Degree System) 16, lakini eneo ambalo lina madini inasadikika ni kubwa kuliko eneo hilo. Maana yake ni nini? Leo pale Nyarugusu ambapo inaaminika kuna millions of ounces za dhahabu kule chini, pale Rwamgasa kuna millions of ounces pale chini, pamegeuka kuwa miji. Sehemu zote hizi zinakuwa urbanized kwa sababu tumeshindwa kuzilinda, tumeshidwa kutengeneza mpango mahususi wa kulinda maeneo haya ili yaje kuwa na faida baadaye kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ombi langu ni kwamba, kwanza tuiwezeshe hii Wizara ikamilishe mpango wake wa kufanya utafiti kwa nchi nzima, utafiti ambao tayari mwaka jana tulipitisha pesa. Ninaamini kwamba, wakifanya utafiti nchi nzima tutasaidia kuyalinda maeneo ambayo kesho kutwa yatageuka kuwa makazi ya watu (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la pili, tulete mfumo wa kuwa na Mineral Land Bank. Maeneo ambayo tunagundua kwamba yana madini tusiruhusu yakageuka kuwa makazi. Kwa sababu, mwisho wa siku hatutaweza kuwaondoa wale watu na tukiweza kuwaondoa, tutawaondoa kwa gharama kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mifano mahususi. Pale Geita kuna eneo la Nyamarembo, eneo la Magema, eneo la Nyakabale; kuna madini mengi nchini, lakini mgodi umeshindwa kufanya maamuzi, either kuwalipa fidia au kuwaacha pale kwa muda mrefu kwa sababu tayari yamegeuka kuwa makazi. Kwa nini? Tulizembea kuyatenga maeneo haya na kuyalinda. Sasa, nchi yetu ni kubwa, maeneo ya madini ni mengi, lakini keshokutwa tutakuwa ni miji kila kona, tutashindwa kuchimba madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaaminika pale Nzuguni kuna dhahabu; inaaminika maeneo mengi ya Dodoma kuna dhahabu, lakini tayari ni miji, hatutaweza kuwaondoa. Jambo kubwa hapa Wizara hii iwezeshwe, kiwe ni kipaumbele maeneo haya yapimwe, maeneo haya yatunzwe, itungwe sheria yasimamiwe. Sheria hii ni muhimu kwa sababu kesho kutwa hayatakuwepo maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine; wakati tunafanya High Resolution Geophysical Survey, ni vizuri tukafanya mambo mawili. Tufanye maji, tuangalie maji pamoja na madini. Tulipata bahati ya kwenda Zambia; Zambia wana takribani square kilometre 740,000. Wako 95% ya kufanya survey ya nchi nzima na wanafanya mambo mawili. Wanaangalia wapi kuna maji mengi na wapi kuna madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu madini ni sehemu kubwa inayoleta forex kwenye Nchi ya Zambia, sasa tuna nchi kubwa uchumi wetu ni mkubwa ni vizuri tukawekeza kwenye eneo hili kwa bidii kubwa kwa sababu baada ya siku chache zijazo maeneo yote haya yatakuwa miji, yatakuwa vijiji na hatutaweza kuwaondoa na tutakuwa tumekula hasara kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tumeona juzi mafanikio makubwa sana kwenye uvuvi kwa maana ya cage, uvuvi wa vizimba, nami nilikuwa muumini sana wa kuhubiri uvuvi wa vizimba. Sasa hivi samaki wa Tanzania ni gharama kubwa, ni expensive kumla kuliko samaki anayetoka nje. Kwa nini, ni kwa sababu Ziwa Victoria namna linavyokwenda litakwenda kuwa redundant kwa sababu, maeneo yote ya mazalia ya samaki yamejaa magugu maji na magugu maji yanamaliza oksijeni chini, yanatengeneza siltation, kwa hiyo samaki kwenye griding area zote zitageuka kuwa matope na maeneo yote samaki watashindwa kuzaliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna uhaba mkubwa wa samaki, hata wanaokaa pembeni ya Ziwa Victoria hawana samaki lakini wanaokaa pembeni ya ziwa Victoria hawawezi kula samaki kwa sababu ni bei ghali ni bora ule samaki wa kutoka nje ya nchi kuliko wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu hapa ni tuweke nguvu kubwa kwenye kudhibiti magugu maji Ziwa Victoria, ukifika leo Busisi kuna kisiwa cha magugu maji na hapo ni Busisi, kule Nkome kuna kisiwa cha magugu maji lakini kule Igombe kuna kisiwa cha magugu maji. Inawezekana tunaliona tatizo hili ni dogo, lakini baada ya muda mfupi tutakuwa na Ziwa ambalo halitakuwa na maana tena, samaki wamepungua na samaki hawazaliwi katikati ya ziwa, wanazaliwa off shores. Huku off shores hawawezi kuzaa sehemu ambapo hakuna oksijeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti ninakushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)